Makala hii inaangazia wakazi wa kisiwa kidogo cha Ikaria nchini Ugiriki wanaishi maisha marefu, kwa wastani wa miaka 10 zaidi ya watu wengine wa Ulaya Magharibi.
Na swali kubwa linabakia kuwa hili kuna siri gani katika kisiwa hiki cha maisha marefu?
Kwa mujibu wa mtandao wa euronews, mwaka 2021, wastani wa kuishi Ulaya Magharibi ni miaka 80.1, hivyo wakazi wa kisiwani hapo wanaishi zaidi ya miaka 90 na wengi hufikia 100+.
Inawezekana ni kuwapo kwa hewa safi, inaweza kuwa mboga safi zisizolimwa kwa mbolea na kemikali za viwandani na maziwa ya mbuzi?
Lakini pia kila sehemu ya kisiwa hicho ni kukavu, hivyo kutembea kunaweza kuchangia kujenga mwili wenye afya. Aidha, inaweza hata kuwa mionzi ya asili ya miamba ya mawe ya granite?
Lakini mkazi wa kisiwa cha Stamatis Moraitis anadhani anajua sababu ya maisha marefu ya watu wa kisiwa hiki.
"Ni kinywaji tunachotengeneza hapa," anasema, akiwa na glasi ya kinywaji juu meza ya jikoni kinachotokana na zabibu, majira ya asubuhi. "Kinywaji safi, hakuna kilichoongezwa ndani yake. Vinywaji vya kibiashara vimeongezwa vitu vingine visivyofaa kwa afya. Lakini hiki ni safi na tunakitengeneza sisi wenyewe."
Stamatis alisherehekea siku yake ya kuzaliwa akitimiza miaka 98, Januari 1 mwaka huu. Anasema ni mzee kuliko kinavyoeleza cheti chake cha kuzaliwa, kwamba alizaliwa Januari 1, 1915.
Nje ya nyumba yake kuna mizaituni, miti ya matunda na mizabibu, hutengeneza takribani lita 700 za juisi ya zabibu kwa mwaka.
"Unakunywa peke yako?" Anapoulizwa na BBC anasema hapana!"
Anasema na kushangazwa na swali na kueleza kuwa anakunywa na marafiki zake na kwamba hunywa zabibu na kupumzika na marafiki na familia.
KUPONA SARATANI
Mzee huyo ni alama ya uponyaji kisiwani hapo, miaka 45 iliyopita, alipokuwa akiishi Marekani, aligunduliwa na saratani ya mapafu na kuambiwa ana miezi tisa pekee ya kuishi.
"Wakati huo ilikuwa ghali sana kufanya mazishi huko Marekani," anakumbuka. "Kwa hiyo nikamwambia mke wangu, 'nakwenda nyumbani kwetu Ikaria walikozikwa wazazi wangu.'
Ni hadithi ambayo ameisimulia mara nyingi, na hajachoka kuisimulia. "Niliwakuta marafiki zangu kijijini nilikozaliwa na tukaanza kunywa juisi ya zabibu. Nikifikiri nitakufa kwa amani."
"Kila siku tulikusanyika, tukanywa pamoja. Muda ulipita na nilihisi nguvu. Miezi tisa ilipita nilihisi afya zaidi, ikaja miezi 11 nayo ilipita - nilihisi niko vizuri. Sasa ni miaka 45 baadaye, bado niko hai,” anasema.
Anaongeza: "Miaka michache iliyopita nilirudi Marekani na kujaribu kutafuta madaktari wangu. Lakini sikuweza kuwapata. Wote walikuwa wameshakufa." Anaeleza.
Kwa ujumla kuna hadithi nyingi kama hizi katika kisiwa hicho na miaka ya hivi karibuni wanasayansi na madaktari wamekwenda kwenye kisiwa ambacho si mbali sana na pwani ya Uturuki ili kujua ukweli wa maisha marefu.
WANACHOGUNDUA
Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo wa Chuo Kikuu cha Athens, Dk. Christina Chrysohoou, ambaye aliwachunguza watu wa kisiwa hicho, anasema, ‘wanakabiliwa na magonjwa ya saratani na matatizo ya moyo sawa na watu wengine, lakini wanayapata magonjwa hayo katika sehemu ya mwisho ya maisha yao, hayawahi kama ilivyo kwa wengine.
"Ikaria inatupa fursa ya kujifunza kwa nini watu hawa wanafurahia faida hizi, hatuwezi kuepuka magonjwa haya, lakini wanafanikiwa kudumisha ubora wa maisha yao kwa miaka mingi. Wastani wa umri wa ugonjwa wa moyo ni kati ya miaka 55 hadi 60. Lakini Ikaria watu hufikia hata miaka 70 kabla ya kupata tatizo hilo."
Pia kuna utafiti wa vinasaba unaowalinganisha watu wanaoishi kisiwani humo na waliozaliwa kisiwani humo lakini wakahama na hivyo kuishi maisha tofauti na ya watu ambao bado ni wazawa wanaishi Ikaria bila kuhama au kuondoka.
Anasema kukutana na baadhi ya wakazi wakongwe wa kisiwa hicho kutakufanya uvutiwe na maisha yao marefu.
Mama mwenye miaka zaidi ya 100, anasema meza ya chakula imejaa vyakula vya Ikaria. "Ni vitafunio," anasisitiza Voula, mke wa George Kassiotis mwenye umri wa miaka 102,”
Anapotoa kitambulisho chake kinachoonyesha tarehe yake ya kuzaliwa ni 1910 na kusimulia maisha yake ya utotoni.
Kwenye ukuta mmoja kuna picha yake akiwa katika kikosi cha wapanda farasi cha Ugiriki mwaka 1931 na kwamba alipigana nchini Italia dhidi ya Albania katika Vita vya Pili vya dunia, kisha akasaidia kujenga barabara ya kwanza ya chuma kisiwani humo kabla ya kustaafu mwaka wa 1970.
"Sili chakula kilichosindikwa, sivuti sigara, sina wasiwasi," George Kasiotis anasema. "Sina wasiwasi na kifo. Najua sote tutakufa."
UTAMADUNI WAO
Aidha, ainabainika kuwa kizazi cha vijana hujaribu kushika mila. Wanapata mlo mwingine nyumbani kwa Nikos Karoutsos, mmiliki wa mgahawa mwenye umri wa miaka 50, na kuona marafiki na familia nyingi wakija kwenye kwake kwa ajili ya vinywaji na chakula.
"Hatuna vilabu vya usiku wala sehemu za kucheza," anasema, huku watu wakigonganisha glasi zilizojaa juisi ya zabibu nyekundu kutoka kwenye chupa kubwa za plastiki. "Mlango uko wazi kila wakati, hakuna haja ya kupiga simu na kuuliza ikiwa uingie."
Wakiwa njiani kuelekea nyumbani wanampita Stamatis Moraitis mwenye umri wa miaka 98, akiwa anapanda ngazi hadi kwenye mzeituni wake mmoja ili kuchuma matunda.
"Nimefurahi bado ninaweza kufanya hivi," anasema huku akicheka. "Ninahisi afya zaidi hapa." Anaongeza.










