Vodacom kuhamasisha wanafunzi wa kike kupenda masomo ya Sayansi

03May 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Vodacom kuhamasisha wanafunzi wa kike kupenda masomo ya Sayansi
  • Ni kupitia programu ya Code Like a Girl...

KWA miongo kadhaa, kumekuwepo na pengo katika ya wanawake na wanaume kwenye sekta ya masomo yanayohusiana na sayansi, hisabati, uhandisi, na teknolojia (STEM). 

Kwa sasa TEHAMA imekuwa ikiwezesha masomo yanayohusiana na sayansi, ambapo upatikanaji wa vifaa vya kawaida vinavyotumika bado inaonyesha utofauti mkubwa uliopo baina ya jinsia mbili. 

Ripoti za hivi karibuni za GSMA zinaonyesha kuwa asilimia 86 ya wanaume nchini Tanzania wanamiliki simu za mkononi ukilinganisha na asilimia 77 ya wanawake. 

Pia inaonyesha asilimia 17 ya wanawake wanapata huduma ya intaneti, ambapo kwa wanaume ni asilimia 35. 

Utofauti huu wa ufikiwaji na mtandao wa intaneti unaonyesha changamoto kubwa kwa wanawake kwenye kupunguza pengo la ufikiwaji wa habari na mafunzo mtandaoni pamoja na maarifa ya kisasa ya kidigitali yatakayowawezesha kuwa washindani na kuendena na soko la sasa ambalo ni la kiuchumi wa kidigitali.

Suala hili lisipozungumziwa litabakia kuwa ndoto ambayo itaathiri uwakilishwaji zaidi wa wanawake kwa miaka ijayo katika masuala ya usimamizi na uongozi katika sekta zetu.     

Pengine inaweza kuwa ni hofu tu, ripoti ya 2022 ya UNESCO inayoangazia jinsia inaonyesha kwamba idadi ya wanawake waliojiunga na masomo yanayohusiana na sayansi kati ya wanaume 100 imeongezeka kutoka 31 mwaka 2000 na kufikia 84 mwaka 2020 nchini Tanzania, ikionyesha muelekeo chanya kuelekea kupunguza pengo lililopo.

Kwa mwaka huo huo wa 2020, idadi ya wanawake waliojiunga masomo hayo ilikuwa ni 39% ya jumla ya usajili wa masomo ya ngazi za juu. Hii ni ziada ya 5% ya nguvukazi ukilinganisha na taarifa za mwaka 2017 za Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambayo inaonyesha kwamba wanawake walikuwa ni 34% ya jumla ya nguvu kazi yote kwa wakati huo.

Wakati suala la kupata elimu iliyo rasmi likitegemea na gharama, ubora, na upatikanaji wa rasilimali, upatikanaji wa maarifa ya kidigitali pamoja na vifaa vya TEHAMA unaakisi kuzifikia taarifa lukuki zinazopatikana mtandaoni.

Pia inamaanisha uwezo wa kuunganisha na fursa chungumzima bila ya gharama zilizopo duniani zinazomwandaa na kumwezesha mwanamke. Ukiachana na kuwa na simu za mkononi, umiliki wa vifaa vya TEHAMA ni wa gharama zaidi na vinaweza kununuliwa hasa kwenye maeneo ya mijini.

Kuliangazia suala hili, Vodacom imekuwa ikitoa misaada ya vifaa vya TEHAMA na kuziunganisha shule za sekondari za umma nchini kote. Robo ya kwanza ya mwaka 2023 pekee, Vodacom imetumia takribani milioni 200 kusaidia kompyuta, vishkwambi, mashine za kutolea nakala, luninga, na vifaa vinginevyo kwa shule tofauti mikoani.

Mnamo mwaka 2018 Vodacom Tanzania ilianzisha programu ya ‘Code Like a Girl’ ili kusaidia kuhamasisha wanafunzi wa kike kujifunza masomo ya sayansi (STEM) na kujua taaluma zinazohusiana nazo. 

Programu hii imekuwa ikiendeshwa kwa miaka mitano na imewawezesha wanafunzi wa kike zaidi ya 1,700 wa kidato cha tano na sita kujifunza maarifa ya kutengeneza tovuti, applikesheni, kuandaa ripoti za uwasilishaji, pamoja na kutumia vifaa vya TEHAMA ili kuendana mahitaji ya soko la sasa la kidigitali. Programu inaendeshwa kwa kushirikiana na Tanzania Data Lab (dLab).

Kwa mujibu wa Vodacom, wakati matumizi ya teknolojia yamepelekea kuongezeka kwa kuzifikia huduma muhimu na kuboresha uzalishaji katika sekta tofauti, bado kuna uhitaji wa kuwawezesha wanawake na wasichana kunufaika kiukamilifu na mapinduzi ya kidigitali, bila ya kuzingatia umri, kabila, kipato, ulemavu, au sababu nyinginezo za kijamii ambazo zinaweza kukwamisha maendeleo yao.

Hii ilibainishwa mwaka 2021 wakati wa shughuli iliyoandaliwa na Ubalozi wa Canada nchini Tanzania, ambayo ilijikita kwenye kuendeleza maarifa ya kidigitali kwa wanafunzi wa kike.

Vodacom inaitumia teknolojia ipasavyo kuinufaisha jamii kwenye mikoa tofauti ya Tanzania, hususani kupitia jitihada zinazolenda kuwawezesha wanawake na wasichana. Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation imeshirikiana na wataalamu mbalimbali na kuwekeza katika miradi yenye dhamira ya msingi ya kuwawezesha wasichana na wanawake. Mpaka sasa, zaidi ya wasichana 5,000 wamenufaika na programu mbalimbali za kidigitali ambazo zinatolewa na kampuni.

Akizungumza wakati wa mahafali ya kwanza ya programu ya ‘Code Like a Girl’ ya mwaka 2023 mwezi Februari, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Vodacom Tanzania, Vivienne Penessis amesema kuwa, “programu ya Code Like a Girl mwezi wa Februari inasherehekea kuwezesha mafunzo kwa wasichana zaidi ya 1,700 kwenye mikoa tofauti ya Tanzania ikiwa ni sehemu ya malengo yake ya kuhamasisha kupenda masomo ya sayansi na TEHAMA, na kuwezesha maarifa ya kidigitali kwa wasichana wa umri kati ya miaka 14 mpaka 18 kwa siku nne. 

Programu ilihusisha watoa mafunzo mashuhuri ambao ni mfano wa kuigwa kwa wasichana, kuwatia moyo kupenda teknolojia na fursa zinazoambatana nazo”. Programu hii ilianzishwa ikiwa ni sehemu ya Vodacom kuhakikisha ujumuisha kwenye matumizi ya teknolojia na uunganishwaji katika zama ya kidigitali ambayo itakuwa ni vigumu kuwezekana kutokana na pengo la jinisia lililopo sasa, ukizingatia kwamba idadi ya wanawake ni wengi kuliko wanaume nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Taifa ya Takwimu imeonyesha kwama mwaka 2022 wanawake walikuwa ni asilimia 51 ya idadi ya Watanzania wote. 

Wakati pengo la kijinsia linaonyesha kwamba ufikiwaji wa mafunzo ya kidigitali na TEHAMA kwa kiasi kikubwa limedhibitiwa na kukaribia nusu ya idadi ya watu wote, hii inamaanisha kwamba itakuwa ni vigumu kufikia malengo yajayo ya mahitaji ya sekta nzima. 

Kwa wastani wa idadi ya usaili wa masomo ya elimu ya juu na chuo kikuu nchini kote ikiwa ni zaidi ya wanafunzi 524,000 kwa mwaka 2022, kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Elimu ya Juu Tanzania (TCU), ni asilimia 3.4 pekee ya idadi hiyo inajumuisha wanawake katika masomo yanayohusu sayansi na takribani mara mbili yake ya wanaume kwenye masomo hayo.  

Lakini hii sio changamoto kwa Tanzania au Afrika pekee kwa ujumla. Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2017 inayojulikana kama ‘Cracking the Code: Girls’ and Women’s Education in STEM’ ya UNESCO, inaonyesha kwama asilimia ya wanawake kwenye elimu ya juu wanaojifunza masomo ya sayansi ni asilimia 35 duniani.

Ripoti pia inaonyesha kuwa wasichana wadogo ni asilimia 25 pekee ya wanafunzi katika masomo ya uhandishi au teknolojia ya mawasiliano na habari (TEHAMA). Kwa mujibu wa kituo cha habari cha IoL News ya mwaka jana, nchini Afrika Kusini pekee ni 13% tu ya wahitimu wa masomo ya sayansi ni wanawake.

Serikali ya Tanzania imejikita zaidi kwenye maendeleo ya elimu ya masomo ya sayansi ili kujiandaa na Dira ya Taifa ya mwaka 2050. Hii itajenda uwezo wa kuhimili na kuendena na teknolojioa ambayo itaongeza uzalishaji katika sekta zote za uzalishaji ikiwemo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. 

Hili liliwekwa wazi na Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango wakati wa uzinduzi rasmi Dira ya Taifa ya 2050.

Kupitia programu ya e-Fahamu, Vodacom imesaidia vifaa vya TEHAMA takribani 600 kwa shule za sekondari za umma, ikiwa imewekeza kiasi kinachozidi shilingi bilioni 1.2 za Kitanzania, ikisisitiza kujizatiti kwake kutumia ushirikiano (lengo la 17 la Maendeleo Endelevu Duniani) kama njia ya kuwezesha maendeleo ya shughuli za kiuchumi na kijamii na mpaka sasa imesisitiza kuendelea kupanua ushirikiano wake na serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) pamoja na washirika wengine kama vile dLab na taasisi ya African Child Projects.