Ni mradi ulioko katika Hifadhi ya Selous wilayani Rufiji, mkoa wa Pwani, unaandaliwa kuwezesha utoaji umeme mkubwa nchini na mpaka sasa, maendeleo ya ujenzi yanatajwa kufika asilimia 85.06 chini ya Rais Dk. Samia, kutoka asilimia 37 alizopokea mtangulizi wake, Dk. John Pombe Magufuli.
Waziri wa Nishati, January Makamba, anaiambia Nipashe, kuwa zimebaki mita za ujazo 13, kufikia 163 kutoka usawa wa bahari, bwawa lianze kuzalisha umeme na hadi sasa maji yamefikia mita za ujazo 150, akipataja ni penye matumaini.
“Pia, linatarajiwa kuwa na lita za ujazo bilioni 30 na mpaka sasa ambazo tayari zimeshajaa ni bilioni sita sawa na asilimia 20 tangu kuanza kujaza maji,” anasema Waziri Makamba, anayetumia takwimu kutathmini kiwango cha maji yaliyoingia wiki mbili zilizopita ni mengi kuliko yaliyoleta mafuriko nyuma 2019/2020, ikiashiria ujenzi wa tuta unadhibiti mafuriko kwa asilimia kubwa.
Hadi sasa mradi una thamani ya shilingi trilioni 6.5, ukitarajiwa kuchangia uzalishaji umeme megawati 2,115, hata kuondoa adha ya mgawo wa umeme nchini.
Wakati hitaji la umeme kitaifa likitajwa kuwa megawati 2000, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linazalisha megawati 1,601 na matarajio ya mradi utakapokamilika na kuanza kazi, utazalisha megawati 3,716.
“Sisi watu wa wizara (Nishati) kwa kushirikiana na kila mmoja wetu, tunaona fahari kubwa kuona sasa ujazaji wa maji umefikia mita za ujazo (cubic meters) bilioni sita. Haya ni mafanikio makubwa kwa serikali na Rais wetu (Dk. Samia) kwa sababu nguvu yake aliyoweka na jinsi anavyotusimamia, imesababisha mradi wote kwa ujumla kufikia asilimia 86, kutoka asilimia 37 alizokuta wakati anapewa madaraka,” anasema Makamba.
Pia, anaeleza binafsi kuridhishwa na kazi ya mkandarasi wa mradi, akisema zimebakia mita 13 za ujazo kwa mitambo ya kufua umeme ianze kuzungushwa na maji kuzalisha umeme.
Kiwango hicho anakitaja kimepita matarajio na malengo ya Rais Dk. Samia aliyoweka, wakati anaenda kushuhudia ujazaji maji bwawa hilo kwa mara ya kwanza, kati ya Desemba 2021 na mwaka 2022.
Anataja ujenzi wa matuta eneo la mradi wenye thamani ya shilingi trilioni 6.5, umeleta ahueni kudhibiti mafuriko jirani yaliyoshuhudiwa. Matarajio ni kuzalishwa umeme megawati 2,115.
Kimsingi, taifa lina uhitaji wa umeme megawati 2,000, huku likizalisha umeme megawati 1,601, matarajio ni kuwapo megawati 3,716, pale utakapomilika kuanza kazi kama inavyokusudiwa.
Wakati Rais Dk. Samia alipotembelea Bwawa la Mwalimu Nyerere, akaonyesha shauku kuona serikali inafanikisha wazo lililoanza tangu zama za Mwalimu Julius Nyerere, akiwa madarakani.
“Nchi yetu chini ya uongozi wa hayati Dk. John Pombe Magufuli katika awamu ya tano, tulisema liwalo na liwe, lakini wazo la mradi huu lazima tulifanikishe kwa vitendo kwa sababu tunajua utatuletea umeme wa uhakika na endelevu.
“Mradi huu utaimarisha na kufungua fursa nyingi za utalii katika eneo la Kusini mwa Tanzania, hususani katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, hivyo kutoa ajira moja kwa moja na nyinginezo,” anatamka Rais Dk. Samia, ambaye akaanza kushughulikia mradi huo katika tafsiri ya kimkakati, akiweka nguvu kubwa kufanikisha kwa wazo la waasisi wa nchi.
Kwa mujibu wa Waziri Makamba, mradi huo unachukua asilimia tatu ya sehemu hiyo ya hifadhi ya wanyama, yenye ukubwa wa kilomita za mraba 50,000.
MANUFAA YAJITOKEZA
Waziri Makamba ana ufafanuzi ziarani wiki iliyopita, akasema mradi JNHPP kwa kiasi kikubwa umezuia mafuriko kwa wakazi wanaoishi jirani, mikoa ya Pwani na Morogoro hasa kipindi cha mvua.
“Tunafurahi kwamba tayari tumefikia mojawapo ya malengo makubwa ya kuanzishwa kwa mradi huu, ikiwamo kuwakinga wananchi na madhara yatokanayo na mafuriko,” anasema.
Vilevile, waziri anaeleza kiasi maji ya mvua kilichoingia kwenye bwawa mwezi Aprili mwaka huu, kinafanana na cha mvua zilizonyesha kati ya Desemba 2019 hadi 2020, hata kusababisha mafuriko katika mikoa hiyo miwili.
“Kwa mvua hizi zilizonyesha katika kipindi cha wiki mbili zilizopita na hasa siku hizi mbili hadi kufikia leo, tungesikia taarifa za vifo na uharibifu, lakini kutokana na mradi huu, jambo hilo halijatokea mwaka huu…
“Wakati Rais Samia Suluhu Hassan anachukua madaraka, ujenzi ulikuwa asilimia 37, mradi ameenda nao ametoa pesa, ametusimamia na ametuhimiza na sisi tumesimamia walio chini yetu na wao wamesimamia wa chini yao na kufanikisha kuwapo hapa tulipo leo,” anasema Makamba.
Hapo, pia anaelekezea pongezi TANESCO, akiwasifu wafanyakazi wale kushirikiana na Mhandisi Mkazi, Lusajo Mwandambo, wanaohakikisha kazi inafanyika usiku na mchana.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande, anamwahidi Waziri, mradi kukamilika kwa wakati, ili kupunguza kero ya ukosefu wa umeme nchini.
“Mtanzania yeyote, kushiriki ujenzi wa mradi huu,” anasema na kuongeza: “Wito wangu kwa wafanyakazi wenzangu wa TANESCO ni kwamba, tusianze kuzembea kwa sababu tunaona kazi inakaribia kumalizika, huu ndio wakati wa kuchapa kazi bila kuchoka.”
Mhandisi Mkazi wa Mradi, Lutengano Mwandambo, anasema wanaanza kujaza maji bwawa hilo litakalokuwa na uwezo mkubwa kuzalisha umeme, akitaja kiwango kinachotakiwa kujaa katika bwawa hilo ni mita 184 kutoka usawa wa bahari.
Kwa sasa anataja kazi zinazoendelea katika mradi, ni usimikaji mageti saba katika njia zitakazoruhusu maji yanapokuwa mengi na kuzidi kiwango cha juu mita 190 kutoka usawa wa bahari.
Anasema ujenzi wa tuta kuu unaenda sambamba na mahandaki matatu ya kupitisha maji, ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 98.47 hadi kufikia Februari 28, mwaka huu.
MHANDISI MKAZI
Mhandisi Mwamdambo anataja kingo nne za kuzuia maji zenye urefu wa kilomita 17.4, ambazo kazi yake ni kuzuia maji yasitoke eneo lake, akiendelea: “Ujenzi wa bwawa la JNHPP unaenda sambamba na ujenzi wa kituo kikubwa cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme mkubwa kilichoko Chalinze, kituo hicho kitapokea umeme mkubwa wa kilovoti 400 kutoka katika mradi huu.
“Kituo hicho kitapooza hadi kufikia kilovolti 132 na kuuingiza kwenye gridi ya Taifa, tayari kusambaza katika kituo cha Kinyerezi Dar es Salaam, Tanga na Dodoma, pia tayari transfoma kubwa sita zenye uwezo wa megavolti 250 kila moja zimeshawasili eneo la mradi.”
Anafafanua kuhusu transfoma hizo sita, nne ni za kupoza umeme mkubwa wa kilovolti 400 hadi 220 na mbili, zina uwezo wa kupoza umeme kilovoti 220 hadi 132.
“TANESCO inaishukuru serikali inayoongozwa na Rais Samia kwa jitihada za kuwezesha kufikia hatua ya kuanza kujaza maji ndani ya bwawa la Julius Nyerere na kuendelea kutoa fedha za mradi huu,” anahitimisha Waziri Makamba.










