Maafande hao ambao waoliteremka msimu wa 2020/21, walipata ushindi huo juzi kupitia wafungaji wao Maka Edward dakika ya 14, Edward Songo akifunga mawili dakika ya 35 na 55, pamoja na Edson Katenge dakika ya 44.
Kutokana na ushindi huo, JKT Tanzania sasa wanafikisha pointi 59, ambapo wanahitaji alama tano tu kufikisha jumla ya pointi 64 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote kwenye Ligi ya Championship msimu huu.
JKT Tanzania imebakisha mechi nne tu ambapo kama itashinda michezo miwili iliyobaki moja kwa moja itakuwa imerejea Ligi Kuu Tanzania Bara.
Timu ya Kitayosce inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo, ililazimishwa suluhu na Pamba FC katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza na kuzifanya timu hizo kuwa kwenye vita kali ya kuwania kupanda Ligi Kuu.
Kitayosce imefikisha pointi 50 ikibakisha mechi nne ambazo ikishinda itafikisha pointi 62, Pamba FC iko nafasi ya tatu kwa pointi zake 48, lakini yenyewe imebakisha mechi tano na kama ikishinda zote itakuwa na pointi 63.
Kwa maana hiyo kati ya timu hizo tatu, mbili zitapanda na moja itatakiwa kubaki kwenda kucheza mechi za mchujo.
Mbali na mechi hizo, kwenye Uwanja wa Majimaji Songea, Mbeya Kwanza ililazimishwa suluhu dhidi ya Green Warriors, Fountain Gate ikaiadhibu African Sports mabao 2-0 kwenye Uwanja wa CCM Gairo mkoani Morogoro, KenGold ikilazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Ndanda, Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga na kwenye Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara, Biashara United, ililazimishwa suluhu dhidi ya Transit Camp.










