USM Alger ya Algeria ama Rivers United ya Nigeria.
Yanga imetinga hatua hiyo baada ya kuongoza Kundi D ikiwa na pointi 13 sawa na US Monastir ya Tunisia, lakini mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, wakiwazidi Watunisia hao kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Yanga imemaliza kundi ikiwa kinara na hii ni baada ya juzi usiku US Monastir kuifunga Real Bamako ya Mali mabao 2-1 huku yenyewe ikishinda 1-0 ugenini dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
Yanga inaongoza kwa tofauti ya bao moja, zote mbili zikiwa na pointi 13, ina mabao tisa, huku US Monastir ikiwa na mabao manane.
Kwa mujibu wa kanuni za michuano hiyo, mshindi wa kila kundi atakutana na moja ya timu tatu zinazoshika nafasi ya pili katika makundi mengine matatu, hivyo kuifanya Yanga kusubiri moja kati ya Pyramids, USM Alger ama Rivers United.
Hata hivyo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, ambaye juzi aliiongoza timu hiyo kuhitimisha hatua ya makundi kwa ushindi huo wa ugenini dhidi ya TP Mazembe, amesema hawaogopi kucheza na timu yoyote ambayo watapangwa nayo kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kaze alisema kwenye hatua ambayo wamefika huwezi kuchagua timu kwani zote ni nzuri na inabidi ucheze nazo.
"Ukifika kwenye hatua hii huwezi kuchagua mpinzani kwa sababu timu zote ni nzuri na hata ukichagua, ukipita ile ambayo hujaichagua utakutana nayo, kwa hiyo sisi yeyote yule tukikutana naye sawa tu, huu siyo tena muda wa kuchagua mpinzani," alisema Kaze.
Akizungumzia mechi hiyo, alisema hawakucheza vizuri dakika 45 za kwanza na dakika 10 za kipindi cha pili hasa eneo la katikati kwenye kiungo.
"Ni furaha kwenye klabu yetu ni kweli hatua ya makundi rekodi zinaonesha hatujawahi kushinda ugenini, lakini sasa tumefanya hivyo, na ushindi huu umetupatia kujiamini na mbinu ya nini tufanye kwenye mechi zijazo tutakapokwenda ugenini.
"Kipindi cha kwanza hatukuwa vizuri, na dakika 10 za kipindi cha pili, hasa katikati ndiyo maana tulimuingiza Farid Mussa aende kucheza namba kumi, halafu tukachezesha viungo wakabaji wawili kwa sababu tuliona pale mbele ya mabeki wa kati wanakosa watu wa kuwalinda," alisema.
Timu zingine zilizoongoza makundi yao ni Marumo Gallants ya Afrika Kusini ambayo ni kinara wa Kundi A, ASEC Mimosas (Ivory Coast) kinara wa Kundi B na FAR Rabat ya Morocco iliyokaa kileleni mwa Kundi C.
Kwa upande wa Marumo Gallants yenyewe hatua ya robo fainali inaweza kukutana na Pyramids, Rivers United ama US Monastir, wakati ASEC Mimosas ikiwa na uwezekano wa kukutana na Pyramids, USM Alger ama US Monastir huku FAR Rabat wapinzani wao wajao katika hatua hiyo wakitarajiwa kuwa USM Alger, Rivers United ama US Monastir.










