Singida Big Stars imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya FA baada ya kuitandika Mbeya City kwa mabao 4-0 katika mchezo wa robo fainali ya FA uliochezwa juzi katika Uwanja wa CCM Liti, hivyo inasubiri timu itakayofuzu hatua hiyo kati ya Yanga na Geita Gold FC.
Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa Habari wa Singida Big Stars, Hussein Massanza, amesema wamefurahi kufika hatua hiyo na kwamba wamejipanga kukutana na timu yoyote katika hatua ya nusu fainali ili kufikia malengo ya kutwaa kombe hilo.
"Tunashukuru Mungu tumepata matokeo mazuri sana, hatukutarajia kuifunga Mbeya City magoli manne, si kitu kidogo kuifunga magoli hayo hasa kwenye mashindano makubwa kama haya, ni ushindi mnono, hii inatokana na matokeo chanya ya kambi tuliyoiweka Dodoma.
"Tulijiandaa vya kutosha hata uchezaji wa leo 'juzi', ulionesha kwamba ni timu iliyojiandaa, hivyo tunaenda kwenye nusu fainali tukijiamini kwa kiasi kikubwa, hata benchi la ufundi linaona mafunzo wanayoyatoa yameeleweka kwa wachezaji, tupo tayari kwa nusu fainali.
"Hatua tuliyofikia hivi sasa tunaweza kukutana na Yanga ama Geita Gold, hivyo tupo tayari kucheza na timu yoyote ile, timu zilizoingia robo fainali zote ni ngumu na nzuri, tunaamini kila tutakayekutana naye atakuwa mpinzani mzuri, tunahitajia kufika fainali na hatimaye kutwaa taji hilo," alisema Massanza.
Hatua hiyo ya robo fainali iliendelea tena jana kwa Azam FC kuvaana na Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamanzi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ambapo mshindi wa mechi hiyo atakutana na mshindi kati ya Simba na Ihefu FC itakayopigwa kesho katika Uwanja wa Uhuru.










