Rais katika miaka miwili akibeba ushuhuda wa kukomboa mtoto

30Mar 2023
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Rais katika miaka miwili akibeba ushuhuda wa kukomboa mtoto
  • • Hatua za usalama, afya yake shule hadi nyumbani

HAINA siku nyingi kusikika agizo la Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ikitaka wanafunzi wa elimu ya msingi wa kuwa bwenini, ni kuanzia darasa la tano, agizo litakaloanza kutekelezwa Juni ijayo, sambamba na vigezo maalum kwa magari ya shule yanayosafirisha wanafunzi katika namna ya kuwahudumia.

Cap
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Sasha Joseph Mbilinyi, mtoto wa mwanasiasa ambaye ni msanii wa Hip-hop, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, katika tamasha la Dream Concert, lililofanyika Serena jijini Dar es Salaam. PICHA: MTANDAO

 

Inapoangaliwa kwa undani katika kutimiza miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, anataja hilo la kuzuia wanafunzi wadogo kuwa bwenini. Pia, anataja la kurejeshwa shuleni wanafunzi waliopata ujauzito.  

Ikirejewa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya Mwaka 2008, inaainisha haki tano za msingi za mtoto ambazo ni za kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushiriki na kutobaguliwa.

Mnamo Novemba mwaka 2021 aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, katika mafanikio ya miaka 60 ya uhuru wa nchi, chini ya uungozi wa Rais Dk. Samia, akatangaza wanafunzi waliokatisha masomo kwa kupata mimba, wataruhusiwa kurejea shuleni baada ya kujifungua.

"Hapa zege halilali…Watanzania wajue uamuzi unakwenda kutoa haki kwa wanafunzi ambao kwa sababu hizo walikuwa wamenyimwa fursa," anaeleza Prof. Ndalichako.

WADOGO MARUFUKU BWENINI

Kamishna wa Elimu, Dk. Lyabwene Mtahabwa, mnamo tarehe 5 mwezi huu, akaagiza shule zote zinazotoa huduma ya bweni kwa madarasa ya awali hadi la nne, kusitisha huduma hiyo ifikapo Juni ijayo. 

Ni waraka aliyoutoa kwa vyombo vya habari, ukifafanua; "Maendeleo ya kweli katika nchi yoyote ile, kwa kiasi kikubwa hutegemea ubora wa elimu, inayotolewa katika nchi husika, ingawa dhana ya ubora wa elimu hutofautiana kutoka nchi moja, hadi nyingine katika muktadha wa nchi yetu."

Anafafanua kuwa elimu bora ni inayomjengea mhitimu uwezo wa kuchambua mambo kwa ufasaha, ili kufanya uamuzi wenye tija, kuwa na maadili yanayoakisi mila, desturi na utamaduni, akijenga moyo wa kupenda, kuthamini na kufanya kazi ili kuleta maendeleo ya mtu binafsi, jamii na taifa kwa ujumla. 

Dk. Mtahabwa anasema kuna makambi mengi yamebainika kuwa na mazingira hatarishi kimaadili, usalama na afya za wanafunzi, pia yameanzishwa bila ya kufuata taratibu rasmi za kuanzishwa mabweni au makazi ya pamoja ya wanafunzi. 

Hapo anasisitiza kuwa malezi na makuzi ya mtoto mara zote yanategemea mchango wa familia kupitia wazazi au walezi, huku kukibainika kuwapo baadhi ya shule zinazopokea watoto wenye umri mdogo kuanzia darasa la awali hadi la nne, pasipo kuzingatia taratibu stahiki.

"Huduma za bweni kwa wanafunzi wenye umri mdogo ikiwamo wa elimu ya awali na darasa la kwanza hadi la nne, huwanyima watoto fursa ya kushikamana na familia na jamii zao, kujenga maadili na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya familia na jamii zao," anasema. 

Anarejea tafiti zinaonyesha kuwapo madhara ya muda mrefu, yatokanayo na kulaza watoto bwenini katika umri mdogo, wakikosa mapenzi ya wazazi na walezi, hata wanashindwa kuwa sehemu ya familia na jamii husika. 

Msomi Dk. Mtahabwa, anasema kilichoamuliwa ni utekelezaji wa mwongozo wa uanzishaji na usajili wa shule uliotolewa na wizara hiyo, Novemba mwaka 2020.

Anaainisha zaidi:"Hairuhusiwi kwa shule yoyote ile kuwa na makambi ya kitaaluma. Hatua hii inaakisi utekelezaji wa Waraka wa Elimu namba tatu wa mwaka 2007 kuhusu kukataza kambi za masomo katika shule za msingi."

Dk. Mtahabwa anatahadharisha kwamba shule yoyote itakayobainika kukiuka maelekezo ya waraka huo, itachukuliwa hatua za kinidhamu, kisheria au kufutiwa usajili.

KUFICHULIWA UKATILI

Mwaka jana, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, akawataka watoto kote nchini kufichua viashiria vya ukatili dhidi yao, maendeleo ya shuleni na majumbani.

Waziri Dk. Gwajima, amewasisitiza watoto wasihofie kuweka wazi, pale waonapo viashiria vya ukatili na kutoa taarifa kwa watu wanaowaamini, ikiwapo dawati la jinsia kwenye vituo vya polisi.

Anarejea takwimu za matukio ya ukatili kwa watoto katika kipindi kati ya Januari hadi Desemba mwaka 2021, kwamba, matukio yaliyoripotiwa kwa Jeshi la Polisi yalikuwa 11,499, ikilinganishwa na matukio 15,870 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

Ufafanuzi wake ni matukio 4,371 kupungua, sawa na asilimia 27.5

Mikoa iliyoongoza wakati huo ilikuwa; Arusha (808), Tanga (691), Shinyanga (505), Mwanza (500) na Mkoa wa Kipolisi Ilala (489) na aina ya makosa yaliyoongoza kwa idadi ni ubakaji; 5,899, mimba kwa wanafunzi 1,677 na ulawiti 1,114.

KUTOKOMEZA UKEKETAJI

Wizara tajwa kwa kushirikiana na wadau imeandaa Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji wa Mwaka 2020/21 kutokomeza ukeketaji ifikapo 2024/25.

Waziri Gwajima anafafanua kwamba, ukeketaji una madhara makubwa kiafya, kisaikolojia, kusababisha kuvunjika ndoa na watoto kukosa malezi. Mikoa yenye takwimu za juu za ukeketaji hadi wakati huo na kiwango chake kwenye mabano ni: Manyara (58%), Dodoma (47%), Arusha (41%), Mara (32%) na Singida (3%).

Waziri anasema katika vita kukabili ukeketaji kwenye mikoa mbalimbali, jumla ya ngariba 1,800 walioamua kuachana na vitendo hivyo, kati ya mwaka 2015/16 hadi Aprili, 2022.

MABARAZA YA WATOTO

Wizara hiyo ikatoa miongozo ya Mabaraza ya Watoto na kuanzishwa madawati ya watoto katika shule za msingi na sekondari, ikitajwa ni hatua muhimu kukabiliana na kadhia ya ukatili.  

Hadi sasa watoto nchini, wamekuwa wakipitia ukatili mbalimbali ikiwamo ya mitandaoni, hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau, imeshaandaa miongozo kwa wanafunzi, walimu na wazazi iwe msaada katika malezi na makuzi ya watoto.

Ni hatua inayoshuhudiwa na marejeo ya Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya Mwaka 2008, inayotambua haki tano za msingi za mtoto, ambazo ni haki za: Kuishi, Kulindwa, Kuendelezwa, Kushiriki na Kutobaguliwa, hivyo kuzinduliwa mwongozo wake, ni chachu muhimu katika kuongeza mapambano ya kumlinda mtoto huyo.

Hadi sasa, kuna miongozo inayopelekwa kwenye shule za msingi na sekondari, pia vyuo vya kati, kwenye madawati ya ulinzi wa mtoto na mabaraza ya watoto yanayoenda kuanzishwa nchi nzima, ili kuwa fursa kwao kujadiliana na kueleza madhila yanayowasibu.

Serikali na wadau baada ya tafiti zake, waliona umefika wakati watoto kupatiwa miongozo itakayowasaidia kuendesha wa mabaraza yao, huku wazazi na walezi kote nchini, wakitakiwa kuwaruhusu watoto kujiunga na kushiriki katika mabaraza yao, itakayowapa fursa kwao, kubainisha changamoto zinazowakabili.

 

 

 

Top of Form

Bottom of Form

Top of Form

Bottom of Form