Anasema katika shughuli zake, amelazimika kuweka kaulimbiu ‘panda mti penda mti ‘ili kuleta hamasa kwa jamii kupenda miti wanayoiona, iwe wameipanda au wameikuta, kwa sababu mtu akipenda kitu ni lazima akitunze
Ignas anahamasisha kuwa, ni aina ya kaulimbiu inayoleta maana katika utunzaji misitu na mazingira kwa ujumla kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Mkuu huyo anasema, kupitia mradi huo uitwao Agroforestry uliofadhiliwa na Taasisi ya Reforestaction kutoka Afrika Kusini, wamepanda miti ambayo jamii inapaswa kuipenda, mimea hiyo nayo inarejeshe manufaa ya kumtunza binadamu kwa faida za kuivuna, kuuza, huku wakipata hewa safi, upepo na kivuli.
Ignas anasema hadi sasa wameshapanda miti zaidi ya 7,000 katika vijiji vyote vya tarafa ya Mgeta mkoani Morogoro, ikiwamo kwenye eneo la hifadhi asilia ya milima ya Uluguru, katika kijiji cha Nyandira.
Hiyo ni sehemu ya mradi mkubwa wa upandaji miti unaohusisha kilimo mseto, kwa upandaji miti na mazao hasa kwenye mashamba ya wakulima ndani ya mipaka ya vijiji vya Nyadira na Chenzema.
MALENGO YALIVYO
Mkurugenzi huyo anasema taasisi hiyo iliyoanzishwa Agosti 2019 inatarajia kupanda miti 440,000 ifikapo mwaka 2025, ili kuboresha utunzaji wa mazingira na misitu kwa ujumla.
Anasema, kwa kushirikiana na wakazi husika, wameshapanda miti ya asili, matunda na ya mbao, kwa kuzingatia maeneo yamo hifadhini, wakulima na wadau wengine wa misitu.
Kwa mujibu wa Ignas, hado sasa wamejikita wilayani Mvomero tarafa ya Mgeta, akitaja kwenye vijiji 11, ambavyo ni; Pinde, Tandali, Nyandira, Chenzema, Langali, Maguruwe, Lukunguni, Kibaoni, Vinile, Bunduki na Kibigili na vijiji vya kata ya Lubungo.
Hapo anaeleza imani yake kwamba, kazi imeshafanyika na itaacha alama kubwa katika Milima ya Uluguru, ambayo haitafutika kwa vizazi vingi.
Ignas anasema, wanauendesha mradi sambamba na kutoa elimu kwa makundi ya kijamii, ikijumuisha wanufaika ambao ni wakulima, katika namna ya kuanzisha vitalu na kukuza miche hadi kufikia upandaji, sambamba na kuwaelimisha watoto na wanafunzi elimu hiyo kusaidia vizazi vijavyo.
Anasema lengo kubwa la kazi ya asasi hiyo, ni kueneza elimu na itikadi ya jamii, kuhusu umuhimu wa kupanda na kulinda miti, kazi ambayo imeshawafikia wakazi wanufaika 3000, kwa matarajio watakuwa wasimamizi endelevu wa misitu.
Matarajio ya Agriwezesha, inataja ni kuhamia wilaya nyingine za mkoa Morogoro, kueneza elimu hiyo ili kutimiza dhana ya utunzaji misitu na uhifadhi wa mazingira katika miradi mbalimbali ya umma, itakayosaidia jamii kushiriki kulinda na kuisimamia misitu waliko.
Mkurugenzi Ignas anasema, miti yote waliyopanda wameingiza kwenye mfumo wa ufuatiliaji na wataalamu wao wanafanya kazi na wakulima na wahifadhi misitu, kufuatilia changamoto zinazoweza kujitokeza, ili washiriki kuzitatua kwa wakati.
“Nawaasa vijana kujenga tabia ya kupenda mazingira na misitu, kwa kuzingatia kaulimbiu ya Agriwezesha inayosema ‘Panda Miti, Penda Miti.’ Kwa vijana naomba watambue ili tuweze kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, njia mojawapo ni kulinda misitu tuliyo nayo na kupanda miti zaidi.
“Tuondoe dhana ya kwamba, upandaji wa miti ni kazi ya wazee, vijana ni nguvu kazi ya taifa pia tuchukua hatua tuwekeze nguvu zetu kwenye utunzaji wa mazingira,” anasema.
OFISA MISITU
Ofisa Msitu Msaidizi wa Hifadhi ya Mazingira asilia Uluguru, Edson Jackson, anasema upandaji miti ni neema kwa jamii, kwenda kufaidi matunda ya ukuaji misitu baadaye.
Anaasema, hali ya uhifadhi msitu Uluguru iko vizuri, kwa sababu ya uangalizi bora na wa kila mara, sambamba na kuendelea kutoa elimu ya moto na utunzaji mkubwa wa mazingira, vyote vikifanya milima hiyo ionekane bora wakati wote.
“Usiridhike kumuona mtu ameingia msituni kukata mti. Huyo anakuharibia vitu vingi sana, kwa sababu kukata mti mmoja ni kuharibu oksijeni ya watu karibia 1,000, hivyo tuwe mabalozi, lakini tuhimize uhifadhi kwa maeneo yetu na vizazi vinavyokuja,” anasema.
WENYEJI WAFUNGUKA
Mzee Fridolin Kurunge (78), mkazi wa kijiji cha Nyandira, Tarafa ya Mgeta, anasema mazingira yameanza kubadilika na kuwa mazuri kwa sababu ya Agriwezesha kupanda miti katika tarafa yao, ambayo haikuwa na miti kabisa.
Anaeleza masikitikio yake kwa tabia za vijana kutojituma kupanda miti, badala yake wanaangukia kuzurura mitaani na kuvuna miti ya wenzao waliyopanda, hali inayorudisha nyuma mipango ya wenzao kimaendeleo.
Mzee huyo anaendelea: “Angalia hata sasa na uzee wangu huu, nimehusika kuingia kwenye kitalu hiki, kwa sababu nimeona uchungu sana, mti una faida kubwa sana na unaleta manufaa mengi sana. Vijana wapo badala ya kutunza wao ni mojawapo ya uharibifu wa mazingira.
“Nimepanda miti kwa kung’oa kutoka maeneo mbalimbali kabla ya ujio wa Agriwezesha. Vijana wamenivizia na kuiba kwenda kuuza, kwa sababu hawataki kujituma, vizazi vijavyo vitanufaika na nini sasa? Mbona wazee wetu walikuwa wanatuachia urithi wa kujituma na tunaitikia,” anahoji Mzee Kurunge.
Hapo anaiomba serikali kuhamasisha vijana zaidi kuiga mfano wa wazee walivyofanya zamani, ili kuwa na mwamko wa kupanda miti na kuipenda miti kama kaulimbiu ya upandaji miti ya Agriwezesha inavyotamka.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Wapanda Miti kwenye vitalu Kijiji cha Maguruwe, Maria Mkwama, analalamika kinamama wanahangaika kutafuta kuni za kupikia majumbani, nao sasa wamehamia kupenda mti, ili kujikwamua na magumu hayo.
Mama huyo anasema, mpaka sasa wamewachukua vijana wakiwamo wa kike, kuwaelimisha kwa kuwaweka karibu na vitalu, kutambua umuhimu wa upandaji, utunzaji na usimamizi wa mazingira.
Anaahidi kuendelea kupenda na kupanda miti kwa umoja, kwa sababu hata vijana zamani walipoharibu, shida kuu hawakuwa na uelewa sahihi, sasa wananuia ‘darasa’ la Agriwezesha, nao wataitumia kufanya makazi yao kuwaya kijani.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), usimamizi endelevu wa misitu ni muhimu mabadiliko ya tabianchi, pia kuhakikisha maisha bora ya baadaye.
Hivyo kutetea dhana hiyo, ndio maana kaulimbiu ya mwaka huu inahimiza; ‘urejeshaji misitu; sauti ya kupona na ustawi’. Umoja wa Mataifa umetenga miongozo mmoja kati ya 2021 na 2030, mahususi wa ikolojia kurejesha misitu.