Toleo hilo halikuvuka kwa ukimya hivi hivi, wenye zama zao wakafumuka kutoka walikotoka, tabasamu mbele na maelezo kibao, mengine yalishakuwa sandukuni na yanaoza.
Ama kweli soka hilo halitofautiani na vyama vya siasa vya maeneo hayo, nguzo ya burudani na kwa watoto wa mjini hizo klabu zao zilikuwa ni kama sehemu ya imani yao, katika sura ile ile ya Simba na Yanga. Na kama huamini thubutu kuivuruga timu hiyo, iliyotimia kuanzia wachezaji, mashabiki, mabaunsa wake na hata 'maofisa utamaduni' nao walikuwa si haba. Kama ukweli ndiyo huo, wanapishana nini wanapishana nini na klabu hizo kubwa za soka nchini?
Kama ni mzaliwa wa tarehe za karibuni, nikuonjeshe kipengele kidogo tu, zilikuwepo klabu za soka za Ashanti na Boom FC za Ilala, Dar es Salaam, ambazo nilizigusia kidogo wiki iliyopita. Timu hizo pinzani zilibeba wasifu wote wa mechi za Simba na Yanga, lakini kwa kipengele cha Ilala, wakipata na wageni wasafiri wa mbali kutoka maeneo kama Magomeni, Kariakoo, Kinondoni, na Temeke, wakimiminika uwanjani kushuhudia mechi nzito.
Mechi zao zote zilikuwa zinachezwa kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam na dalili kuwa siku hiyo kuna mechi zilianza kuonekana mapema asubuhi tu pilika pilika zake na ikifika jioni inakuwa ni hatari.
Mara nyingi wakati inachezwa, nje na ndani ya uwanja waliokuwa wakilinda si askari wa kawaida, bali ni kikosi cha mbwa na farasi kutoka Ukonga ndicho kilichokuwa kikifanya kazi hiyo. Na wakati mwingine mechi hiyo inakuwa haimaliziki salama.
Ipo siku nitakuja kuelezea mtiti, vioja na songombingo ya mechi za Boom FC na Ashanti, ambapo kwa Dar walikuwa wanashika nafasi ya pili ukiondoa Simba na Yanga.
Nikudokeze tu, kila mahali kulikuwa na upinzani unaoendana na 'big match' kama hiyo ingawa wa Ilala ulizidi utamu wake, lakini kwenye mechi nyingi kubwa za mchangani wachezaji wote maarufu wanaochezea soka la juu, zikiwamo timu za Simba na Yanga, siku hiyo wanaonekana kurudi walikotokea, na hilo ndilo likajidhihirisha katika 'big match', kati ya Bongoyo na Eleven Stars katika Uwanja wa Magunia Msasani, winga hatari wa Majimaji na timu ya taifa, Celestine 'Sikinde' Mbunga, wakati akisikika anatua Jangwani kujiunga na Yanga, mwanzoni mwa miaka ya 1980, akaibukia kwenye mechi hiyo, akiichezea Eleven Stars, huku kama kawaida timu hizo zikitambishiana wachezaji wenye majina makubwa kama vile Yassin Maarufu wa Sigara na Athanas Michael wa Mlandege ya Zanzibar.
Tusiongee sana, tuwasikie wenyewe wenye zama zao wakifunguka:
Wa kwanza kabisa ni mwanahabari mkongwe Daniel Mkate ambaye alinipigia simu na kuniambia aliisoma makala ile, lakini akasema kuna baadhi ya timu maarufu ambazo hazikuwepo kama Friends Rangers ya Manzese, ambayo imetoa wachezaji wengi mno kwenye Ligi Kuu, mahasimu wao Kagera Rangers na Magomeni Kagera, DC Nyarugusu.
Ni kweli kabisa hizi ni moja kati timu maarufu sana zilizowatoa wachezaji wengi kama kina Mohamed Hussein 'Tshabalala', Shekhan Rashid, Thomas Kipese, Abdul Ramadhani 'Mashine', na wengine wengi.
Mkazi wa Magomeni aliniandikia meseji kwenye namba yake ya simu 0735 695662 akafunguka maneno haya.
"Mjukuu wangu Adam, katika timu za miaka hiyo, umezisahau New Boys na Jamaica za Magomeni Makuti, Sheffield Mzimuni, Wonder Boys ya Kanisani Magomeni Baptist (ilinzishwa na padri), Fighters Army ya Magomeni Mapipa, Bongoyo ya Msasani, Villa Equad, Jembe Sports ya Kinondoni Mkwajuni, Nungu Sports.
Msomaji mwingine anayeonekana ni mkazi ama wa Manzese au Tandale, yeye aliuliza kama timu maarufu wakati huo iliyowatoa wachezaji kama Hanzuruni Hamisi aliyekwenda kuichezea Simba na Sekelo Barnabas ambaye alizichezea klabu zote za Simba na Yanga, National kama ipo.
"Nilikuwa nauliza, hivi National ya Tandale bado ipo au imeshakufa?" Aliandika akitumia simu namba 0692 939282.
Mwingine anaonekana kipindi hicho alikuwa Tanga, akazitaja timu kadhaa za maeneo ya Majani Mapana.
Mchangiaji huyo mwenye namba 0765 477615 aliandika maneno haya:
"Mimi nazikumbuka klabu za Vipegi na Raidini zote za Majani Mapana, hawa ni mahasimu kweli kweli ambao walikuwa wakicheza kwenye Uwanja wa shule ya msingi Majani Mapana, timu zingine Tanga Mjini zilikuwa ni Vasco Da Gama, Rawalpind, Mzalendo, CIC, na Saruji."
Kuna huyu mwingine ambaye inaonekana alikuwa mkazi wa Msasani, naye akatoa maoni yake.
"Pia Msasani kulikuwa na klabu ya Elleven Stars ambayo ilikuwa ni mahasimu wakubwa na Bongoyo, ikiwa na wachezaji wenye majina makubwa kwenye timu kubwa, kuna Kumbukumbu ya Kinondoni."
Msomaji mwenye namba 0743 817900 alikumbusha timu za maeneo ya Tabata enzi hizo, akaandika.
"Kuna timu umesahau kama Joto ya Jiwe ya Tabata Kimanga, Twiga FC ya Tabata Kisiwani, National Housing ya Tabata Mawenzi, Tabata Boys ya Tabata Shule na pia Segerea United ya Segerea, ukiuliza watu wa miaka ya 1990 watawambia."
Hii yote ni kuonyesha makala ya toleo lililopita iliwakuna wengi na nikatoa nafasi kwa wasomaji kunikumbusha timu wanazozifahamu, lakini hazikuorodheshwa, hivyo wakaanza kupiga simu na kumimina meseji zao, wakikumbuka timu zao wanazozifahamu ambazo hazikuwepo.
Tuma meseji 0716 350534










