Dk. Ngailo: TFRA tumeboreshwa kote kwa mbolea, viwanda hadi maabara

24Mar 2023
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Dk. Ngailo: TFRA tumeboreshwa kote kwa mbolea, viwanda hadi maabara

Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan alizindua mpango wa ruzuku ya mbolea mnamo Agosti 8 kwenye Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima,yaliyofanyika katika viwanja vya Mwakangale, jijini Mbeya.

Hapo akaitaka Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuanza utekelezaji wa mpango huo mnamo Agosti 15, 2022.

 

Hadi sasa, mbolea imeshatawanywa takribani mikoa yote nchini na kutoa nafasi kwa wakulima kuipata kirahisi, hiyo ikimaanisna ni kitendo hicho kimewaibua wakulima na kilimo nchini, kulingana na sehemu anayoishi.

 

Nipashe imezungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dk. Stephan Ngailo, anayesema mzizi unaanzia na kupanda  bei ya mbolea kwenye soko la dunia, hata wakulima wengi kutoweza kumudu gharama zake. Serikali ilitenga Sh. bilioni 150 kugharamia ruzuku kwa msimu wa kilimo 2022/2023.

 

Anasema kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na 2021/2022 gharama za mbolea zilipanda ghafla na wakulima walinunua bidhaa hiyo kwa bei kuanzia Sh. 100,000 hadi 150,000 kulingana na umbali anakonunua.

 

Dk. Ngailo anaeleza utoaji ruzuku umezingatia mahitaji halisi ya mkulima nchini, kulingana na taarifa za usajili na bajeti ya serikali na kubainisha kuwa mbolea zilizohusika katika Mpango wa Serikali wa Utoaji Ruzuku na zile za kupandia, zikiwa ni nusu ya matumizi yote ya mbolea nchini ;mbolea za kupandia na kukuzia za aina nyingine nazo zimehusishwa , kulingana na mahitaji ya soko.

 

Katika kuhamasisha matumizi ya mbolea za nchini, mbolea nazo zimeingizwa kwenye mpango wa

ruzuku, katika mwaka wa fedha

wa 2022/2023.

 

Dk. Ngailo anaeleza mfumo huo umetumia programu maalum kidijitali kuratibu utekelezaji, kuanzia utambuzi wa washiriki wa mfumo wakiwamo waingizaji na wazalishaji wake, wafanyabiashara na wakulima zitakazoratibu usambazaji; uuzaji mbolea kwa wakulima; na malipo ya ruzuku ya mbolea.

 

Anasema hadi kufikia mwezi uliopita, waingizaji wa mbolea 28 wamesajiliwa, wazalishaji watatu, wakala na wasambazaji mbolea 3,303 wanaotumika katika mikoa yote 26 nchini. Pia, anaeleza kuwa hadi tarehe hiyo,  kushirikiana na serikali za mitaa, imeshasajili wakulima 3,264,440 wenye vigezo vya kunufaika na mbolea za ruzuku.

 

HALI YA VIWANDA

Hali ya kuongezeka viwanda vya kutengeneza mbolea na visaidizi vya mbolea, Dk. Ngailo anasema kuna

jumla ya viwanda 16 vya kuzalisha mbolea na visaidizi vyake (chokaa na gypsum) ,ambavyo  ni vitatu vilivyoko mikoa ya Dodoma na Tanga, akiainisha, vipo viwanda 10 vya kutengeneza mbolea za maji na sita, hutengeneza mbolea za punje.

 

Dk. Ngailo anamsifu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuhamasisha wawekezaji binafsi nchini, akitaja mfano wa kutoka nchini Burundi, yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha ujenzi wa kiwanda, jijini Dodoma na kimeshaanza uzalishaji tani 200,000 kwa mwaka, lakini kitakapokamilika, kitazalisha tani milioni moja na tani 300,000 za chokaa.

 

WAPATA MAABARA

Anasema, itapunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje, huku ujenzi wa maabara kupima mbolea ya TFRA  ukiendelea, kwani imekuwa ikitumia maabara za taasisi nyingine kupima ubora wa mbolea, hali inayochangia ucheleweshaji wa kupata majibu, hivyo kupunguza kasi ya utekelezaji wa majukumu ya udhibiti.

 

Anasifu ndani ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, mamlaka yao ilitengewa bajeti  kuanza ujenzi wa maabara ya mbolea na hadi mwezi uliopita, ilifikia asilimia 95 na kwamba itawaongezea ufanisi katika kazi yao. Kwa mujibu wa Dk. Ngailo, maabara hiyo inatarajiwa kutumiwa na nchi jirani za Malawi, Zambia, DRC, Burundi na Rwanda, hivyo kuongezea nchi

mapato.

 

UPATIKANAJI MBOLEA

Kuhusu hali ya upatikanaji mbolea nchini katika miaka

miwili  iliyopita, Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja, Joseph Charos,  anasema kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ilikuwa tani 546,818 na matumizi tani 475,870.

 

Anafafanua, hadi kufikia Januari mwaka huu, upatikanaji wa mbolea nchini umeongezeka kufikia tani 678,528 sawa na asilimia 102 ya mahitaji nchini, matumizi yakikadiriwa ni  tani 667,730 ifikapo mwezi Juni mwaka huu,  msimu wa kilimo unapofika mwisho.

 

Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Happines Mbele anasema, mifumo ya udhibiti wa mbolea nchini imeendelea kuimarishwa na kuhakikisha inawafikia

wakulima kwa ubora, bei nafuu na kwa wakati. Anasema udhibiti tajwa umewezekana kutokana na kuongezeka idadi ya wakaguzi wa mbolea nchini, kusajili wafanyabiashara wa mafunzo ya kila mara kwa mfumo wa uendeshaji wa biashara ya mbolea.

 

Happiness anataja mgawanyo wao; kuanzia mwaka 2012 mpaka sasa kuna wakaguzi wa mbolea 140 katika Ofisi za Mamlaka na Halmashauri za Wilaya; na maofisa kilimo 59 kati ya 140 waliopata mafunzo ya ukaguzi, wakisubiri kutangazwa kwenye gazeti la serikali, ili waendelee na jukumu la kudhibiti ubora wa mbolea.

 

Mkurugenzi huyo anasema, hadi sasa idadi ya wafanyabiashara wa mbolea imeongezeka kutoka 1,691 mwaka 2020/2021 hadi 4,776 mwezi uliopita, akijinasibu ni mafanikio makubwa.

 

Anaeleza matumizi ya mbolea nayo sasa yako juu  maradufu, Happiness akisema yameongezeka kutoka tani 426,550.41 mwaka 2021/ 2022 hadi zaidi ya

tani 667,730 kwa msimu huu wa kilimo.

 

Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi , Victoria Elangwa anaeleza kwa miaka miwili sasa, Mamlaka ilikuwa na ofisi moja tu ambayo ndiyo makao makuu jijini Dar esSalaam, sasa imefanikiwa kufungua ofisi tano za Kanda, akizitaja: Nyanda za Juu Kusini (Mbeya); Mashariki (Dar Es Salaam); Kati (Tabora); Kaskazini (Arusha), na Ziwa (Mwanza).

 

KAZI KWA TEHAMA

Hapo anaungwa mkono na Meneja wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Robert Mtendamema, anayeeleza kufanikiwa kuboresha mfumo wa utoaji wa huduma kwa wadau wake, uitwao Mfumo wa Kimtandao wa Mbolea(FIS).

 

Anaeleza ni mfumo huo unaohudumia wadau, ikijumuisha wanaohitaji kujisajili kwa biashara ya mbolea, kusajili mbolea mpya, waingizaji wapya wa mbolea na wale wanaowasilisha maombi ya vibali vya kutoa na kuingiza mbolea nchini.

 

Anasema awali huduma zote zilitolewa kwa mfumo wa kawaida, unaotumia muda mrefu, ikihusisha kusafiri ili kukamilisha mahitaji ya wadau. Anataja iliyopo sasa ni sehemu ya ajenda kitaifa ‘Kilimo ni Biashara’.

 

Top of Form

Bottom of Form