Lakini linalosikika zaidi ni pale mtu anapolazwa na kufia hospitalini na kuibuka suala la gharama za matibabu na hifadhi ya mwili mochwari na jinsi uongozi wa hospitali unavyochachamaa kudai.
Watu wanaonesha kusikitishwa na hatua ya baadhi ya hospitali kuzuia miili mpaka hapo wafiwa wanapokuwa wamelipa gharama, ndipo waruhusiwe kuchukua mwili kwa maziko.
Wapo wanaofikia mahali kusema ni uonevu tu, kutokana na kwamba kabla ya mtu kufariki dunia amekuwa akilipa kodi kwa njia mbalimbali, ambayo ndiyo inawalipa madaktari na wauguzi mishahara yao lakini pia kununulia dawa.
Wanasema hivyo, baada ya kuona kwamba mtu akishapoteza maisha hubadilishwa na kuwa kama bidhaa ambayo wanauziwa ndugu ambao wanalazimika kulipia gharama za dawa, malazi, chakula na hifadhi ya chumba cha maiti.
Wanashangaa na kupendekeza kwa Serikali kuondoa dhana hiyo ya kudai gharama pale mtu anapokuwa amepoteza maisha, kwani anakuwa hana kazi tena kwa ndugu zake, ambao si tu wamempoteza, lakini wanatakiwa tena kuny’ang’anywa hata walichobaki nacho.
Mmoja wa wanaojadili hilo anafikia kutolea mfano wa gari bovu lililoharibika likapelekwa kwa fundi gereji, lakini likashindikana, anahoji mantiki iko wapi kwa mmiliki wa gari hilo kulazimishwa kulipia matengenezo wakati halikutengemaa.
Anasema ni sawa na binadamu, anaugua, analazwa hospitalini juhudi za madaktari zinagonga mwamba na anapoteza maisha, inakuwaje sasa ndugu kudaiwa kulipa gharama za kitu kilichopotea ambacho hata hivyo hakitawasaidia tena maishani!
Mwingine anakuja na hoja, kwamba ni bora Serikali ikajitazama upya na kulinganisha kati ya elimu na matibabu kipi kilipiwe na kipi kitolewe bure. Anahitimisha kwa kutaka bora wananchi walipie elimu na kupewa matibabu bure.
Hoja yake, ni kwamba siku hizi elimu haina maana kama zamani, kwa sababu zaidi ya kujua kusoma na kuandika na kukaririshwa, baada ya hapo mtoto akishahitimu hata chuo kikuu, atarejea nyumbani kusumbua wazazi wake baada ya kukosa ajira.
Anasema ni tofauti na matibabu ambapo mtu akiyakosa ndio unakuwa mwisho wa maisha yake, huku asiyekwenda shule akiweza kuishi kwa kujitafutia chochote cha kufanya na kujiingizia kipato. Mantiki iko wapi hapo? Unayesoma hapa tafakari nawe pia.
Nikiendelea kusikia mijadala hii inayofikirisha, kichwani inanijia taswira ya ile video iliyosambaa hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii, ikimwonesha mkazi wa Manzese, Dar es Salaam, Osam Milanzi, akizolewa na basi la mwendokasi karibu na makutano ya barabara za Jamhuri na Morogoro.
Kwa aliyeiona video ile, bila shaka akili ilimtuma kuwa pale alipokuwa amebamizwa Milanzi, lazima alibaki vipande vipande kwa kusagwa na basi lile ikizingatiwa ukubwa wa gari lakini pia mwendo lililokuwa nao na pale alipobananishwa.
Nilikuwa mmoja wa walioamini hivyo, lakini pia sikuamini niliposikia Milanzi yuko hai Muhimbili amelazwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) akiweza kutamka jina lake moja tu; Osam.
Nilithibitisha yuko hai, baada ya kumwona mkewe, Isha Mohammed na mdogo wake, Shaban Milanzi wakiwa Muhimbili kumjulia mpendwa wao na kusema anaendelea vizuri na anajitambua na kuzungumza! Sikuamini, nikasema kumbe Mungu mkubwa!
Lakini nikawapongeza wafanyakazi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa walichokifanya kupigania maisha yake na sasa huenda Mungu akamsaidia akarudi kwenye kibarua chake cha kujitafutia kula na familia yake.
Kilichoniuma na kunigusa zaidi, ni pale Isha alipofunguka na kusema mumewe ni masikini na hana bima ya afya na hivyo kutarajia gharama kubwa ya matibabu yake, na akaomba Serikali imsaidie kwa hilo, ili mumewe akipona wasiandamwe na madeni ya matibabu.
Alisema hivyo akizingatia kibarua alichonacho mumewe, ambacho ni cha kipato cha kijungujiko tu, ambacho kwa makadirio ya haraka haraka, hakitamwezesha kulipia gharama za matibabu hayo ya mumewe.
Naamini Serikali sikivu ilimsikia Isha ambaye alionesha uchungu dhahiri hasa baada ya kumtafuta mumewe kwa siku sita bila mafanikio na kujikuta ameangukia MOI. Watu aina ya Isha na familia yake ni wengi nchini, ni vema ukawapo utaratibu mbadala hata kama si wa bima ya afya kwa wote.
Naungana na wanaopendekeza kuwa ni bora kulipia elimu lakini matibabu yakatolewa bure, ili kuepusha kuyakosa na kuishia makaburini, kama inavyotokea kwa wengi wetu ambao hupoteza maisha kutokana na umasikini tu. Mwito kwa familia ya Osam, akitoka msimwoneshe ile video, mtamsumbua kisaikolojia! Alamsiki!










