Huyo ni mjasiriamali mwenye ulemavu wa viungo na baba wa watoto wanne kutoka eneo la Majengo kwa Mtei, mjini hapa, akiwa na umri wa miaka 60.
Anasema miongoni mwa ubaguzi aliokumbana nao ni pamoja kunyimwa hata nyumba za kupanga kwa kuhofiwa kushindwa kulipa fedha ya pango, kutokana na hali yake ya ulemavu.
"Niliumia sana bila kukata tamaa na badala yake, niliongeza jitihada za kufanya kazi na kujifunza zaidi ili nipate kuisaidia familia yangu, iliyokuwa ikinitegemea kwa hali na mali,”anaieleza Nipashe.
Lyimo anaeleza kwamba, licha ya matatizo mengi aliyopitia kila mara, hakukata tamaa na aliendelea kufanya kazi kwa bidii, huku akimuomba Mola.
Anasimulia kwamba amekuwa akikabiliwa na matatizo mengi kikazi na hasa ya ubaguzi, kunyanyaswa na hata wakati mwingine watu kumchonganisha na familia yake, waweze kuachana kwa miaka 20, sasa anajisifu kuvuka vikwazo kwa mafanikio, akiwa na ofisi yake.
Lyimo ni mjasiriamali wa bidhaa za ngozi, baba wa watoto wanne na mke, anayefanya biashara yake eneo la majengo kwa Mtei, akiwa na makazi alikojenga, Msaranga katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
"Mwanangu wa kwanza yupo chuo cha Ardhi jijini Dar es Salaam ameingia mwaka 2022 na namsomesha hivyo hivyo. Naamini Mungu hataniacha, hajapata mkopo kabisa na wa mwisho amemaliza VETA, nipo naye katika eneo langu la kazi akiwa kama ofisa masoko,"anasema.
ALIJIFUNZA UFUNDI
Lyimo anasema alijifunza fani hiyo, baada ya kuona maisha yamekuwa magumu na hana namna ya kuilisha familia yake, pamoja na kutimiza majukumu yake kama baba na wakati huo huo mume. Anaeleza, licha ya hali yake, bado akatambua wajibu wake.
“ Kiujumla mwanzoni sikujifunza sehemu yoyote ujuzi wa kushona tofauti na kuwaona mafundi viatu wakifanya hivyo, ingawa baadhi ya mafundi walikuwa wakinidharau na kuona siwezi chochote.
“Ilinilazimu kutumia nguvu kubwa kujifunza, ikiwa ni pamoja na kupita kwenye maeneo wanayofanya kazi mafundi na kuwatazama wanachokifanya bila ya wao kujua na ninaporejea najikuta katika kufanya majaribio hadi naweza,” anasimulia Lyimo.
Anasema kutokana na hali ya kutokubalika, kuna wakati alikuwa akifukuzwa kwa mafundi hao mara anapokuja mtu mwingine au mteja, akidaiwa kupisha eneo hilo au aondoke, ili wateja wasikose pa kukaa kwa amani kutokana na uwapo wake.
"Ninapokwenda kupiga stori pamoja na kuiba ujuzi, hukaa nikipiga stori mbili tatu, ingawa anapokuja mtu mwingine (mteja au rafiki wa fundi) mimi hulazimishwa nikae chini, au kutakiwa
kuondoka au kuhamishwa kwenye kiti nilichokaa,” anatamka, akiongeza”
“Ili kupisha binadamu au kutupiwa majina ya kejeli' huyu mlemavu amekuja kuniongezea tu nuksi nisifanye kazi', aondoke watu tukae na kadhalika.”
Anasema alivumilia akiendelea kuwaza malengo yake ni kuhakikisha anayafikia kwa kujifunza kila mara na kufanya majaribio.
ALIPOANZA KUTOKA
Lyimo anasema, baadaye alimudu kushona (kurekebisha) viatu vya watu na baadhi wakaanza kumuamini kutokana na ufanisi wake, hasa akiwatoza bei ndogo wateja wake.
“Ujuzi wangu ulikuwa na nikaanza kutengeneza viatu vya watoto wadogo vya ngozi, kwa ‘kuigilizia’ vile vinavyokuja kuripea na kuwashauri baadhi ya wazazi kubadilisha soli za viatu vilivyotoboka. Baada ya kupata jina, nilianza kutafuta ngozi kwenye Kiwanda cha ngozi Moshi kisha kutengeneza viatu vya ngozi.
“Sio kazi rahisi, ila kwa jitihada iliwezekana, nilikuwa mdadisi wa mara kwa mara hata kule kiwandani, walinipa maelekezo na wengine walinikatia ngozi kwa mashine na nikaanza kujitafutia riziki kwa kiwango hicho,” anasimulia.
Kwa mujibu wa Lyimo, hapo ndipo akaanza kushuhudia maisha na yaliendelea, hata akaweza kuwafundisha vijana wanne kazi, pamoja na kuwaajiri katika utafutaji wa masoko.
Kutokana na tabia yake ya kupenda kujifunza kila mara, anasimulia akakutana na asasi ya kimataifa ya kiraia ya ‘Solidaridad Network’ kwenye mradi wake wa kuongeza thamani ya mazao ya ngozi, Zimbabwe na Tanzania.
Hapo Lyimo ana simulizi nyingine kwamba, waliweza kuwapatia mafunzo ya kina kuhusu utengenezaji bidhaa za ngozi na hasa viatu, pochi na mikanda.
SHIDA ILIYOPO
Lyimo analalamika kwamba, kwa sasa soko limekuwa tatizo kubwa, kwani umma kwa sehemu kubwa ni wateja wa bidhaa za kigeni akiziita ni ‘bandia’ na watu hao hawana uzalendo.
“Bado kuna tatizo la ngozi bora, kwani katika mkoa wa Kilimanjaro kuna viwanda vitatu tu vya uchakataji ngozi, lakini kwa sasa, moja kati ya hivyo kimefungwa na kusababisha wengi kuhemea ngozi kwenye hivyo viwili, ambavyo wakati mwingine hupata ngozi zisizo bora,” anaeleza.
“Ombi langu binafsi ni wafadhili na watu wenye mapenzi mema, kunisaidia ili niweze kupata mashine za kisasa zitakazonisaidia kufanya kazi zangu kwa urahisi tu.
“Kwenye upande wa masoko, tunaomba serikali kuangalia uwezekano wa upandishwaji kodi za kuingizwa bidhaa bandia (zisizo ngozi halisi) na kuhamasisha Watanzania kuvaa zaidi bidhaa za ngozi,” anasema .
Agustino Kimario (27), ni miongoni mwa vijana waliopata mafunzo na kufungua ofisi yake, anasema mara baada ya kujifungua mtoto wake alikabiliana na matatizo yaliyomlazimu mara baada ya mtoto kuhitimu miezi miwili alianza zoezi la kutafuta kazi bila mafanikio ndipo alipoanza kushona malapa nje kidogo ya nyumba yake.
“Pitapita zangu za hapa na pale, nilimuona baba mmoja mwenye ulemavu (mshona viatu), niliongea naye, nikamuomba anifundishe, ili kujiingizia kipato kwa kile nilichokiamini kuwa kama yeye ni mlemavu anaweza, mimi siwezi kushindwa.
“Nilipoongea naye, alinifundisha, nilielewa na kupitia vikoba, niliweza kukopa na kufungua ofisi yangu kwa sasa najitegemea,” anasimulia
Pia anaeleza kuwa, biashara yao hutegemea msimu na mwisho wa mwaka hadi mwanzoni mwa mwaka watoto wanapoenda shule.
“Kwa sasa nimeweza kujitegemea kiuchumi, kuwasomesha wadogo zangu na kumlea mama yangu, ambaye mara nyingi hutembea kwenye masoko kuuza. Kwa siku unaweza kuuza shilingi 70,000 hadi laki moja, ikiwa biashara ‘imechanganya’, ingawa kuna wakati hali inakuwa mbaya zaidi.
Rai yake ni kwamba, serikali ijitahidi kuwawekea wajasiriamali fursa ya masoko ya uhakika, mitaji na kuongeza jitihada kuhamasisha Watanzania kuacha kutumia bidhaa za plastiki wazame katika ngozi.
“Nimewahi kusikia juu ya asilimia 10 (mikopo) ya halmashauri, lakini imekuwa na milolongo mirefu sana, kiasi kwamba unakata tamaa.
“Unaweza kurudishwa zaidi ya mara tano, sita kwa ajili ya kitu kimoja.”anasema
WADAU HUSIKA
Julius Fanuel, Ofisa Miradi kutoka asasi ya kimataifa ya kiraia ya Solidaridad Network, anasema mradi wao umeweza kukutana na wajasiriamali wa ngozi mbalimbali nchini Tanzania na Zimbabwe.
Anafafanua kwamba nchini kwa sasa wamejikita katika miradi ya maziwa, kahawa, chai, dhahabu na ngozi, hivyo anataja walikijikita kuwa “asasi hii inayolenga kujenga dunia ambayo vyote vinavyozalishwa na kutumiwa vinatosheleza mahitaji ya sasa na baadaye pasipo kuathiri mazingira hasa katika kuongeza mnyororo wa thamani.
“Kwa Tanzania, inashughulika na kusaidia kutatua matatizo ya uzalishaji masoko kwa mnyororo wa thamani wa bidhaa kama vile kahawa, chai, maziwa na ngozi, hasa kwa wajasiriamani wadogo.
“Solidaridad inatekeleza mradi wa kuendeleza sekta ya ngozi uitwao ‘Promoting a Competitive , Inclusive and sustainable leather sector in Tanzania and Zimbabwe’…”anasema Ofisa Mradi.
Anafafanua kuwa, ni mradi unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya, kupitia Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), ukitekelezwa mkoani Kilimanjaro, kwenye wilaya za Moshi, pia Manispaa ya Moshi .
Ni mradi uliozinduliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Tixon Nzunda mwaka jana, akihimiza halmshauri hizo kuwapa kipaumbele wenye ulemavu, nao waweze kujinyanyua kiuchumi










