Ikiwa nchini Morocco ambapo michuano hiyo inachezwa, juzi timu hiyo iliibamiza Green Buffaloes ya Zambia mabao 2-0 yaliyowekwa wavuni na mastraika wake wawili, Asha Djaffar raia wa Burundi na nahodha wa timu hiyo Opa Clement.
Ilikuwa ni siku ya furaha si tu kwa Watanzania, bali Ukanda wote wa Afrika Mashariki na kati. Ikumbukwe kuwa michuano hii inachezwa kwa washindi wa kanda saba za Afrika, hivyo Simba Queens ilikuwa ni bingwa wa Ukanda wa CECAFA, hivyo ilikuwa ikiziwakilisha nchi zote za ukanda huo.
Na hii ni mara ya kwanza kwa timu kutoka ukanda huu kufika hatua hiyo kwenye michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).
Cha kufurahisha ni kwamba wameifunga timu ambayo si tu Mabingwa wa Zambia, lakini ndiyo bingwa pia wa Ukanda wa COSAFA na mwakilishi wa kanda hiyo, kwani Mamelodi Sundowns Queens inashiriki kama bingwa mtetezi.
Si kazi rahisi na wala haikuwa kazi ndogo kufika hapo ilipofika kwani pamoja na viongozi wa klabu hiyo kabla ya michuano hiyo kubainisha kuwa lengo ni kufikia hatua hiyo, lakini haikufanikiwa.
Naandika hili ikikumbukwa kuwa kwenye mechi ya kwanza tu ya Kundi A ilichapwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji, Asfar ya Morocco na ikawa kama safari hiyo imewekewa kizingiti, hivyo kuhitaji ushindi kwenye mechi zote mbili zilizobaki.
Kwenye mechi iliyofuata iliifunga Determine ya Liberia mabao 2-0, matokeo ambayo bado yalikuwa hayaipi uhakika wa moja kwa moja kusonga mbele.
Kwa bahati mbaya sana kwenye mechi ya mwisho ilicheza na timu ngumu ya Green Buffaloes ambapo mbali na kuwa ina wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa, na asilimia kubwa wakiwa wanaichezea timu ya Taifa ya Zambia ambao walikuwapo kwenye michuano ya AFCON iliyofanyika nchini Morocco Julai mwaka huu na wakatolewa hatua ya robo fainali na Afrika Kusini.
Niliwaona zaidi ya wachezaji watano wa timu hiyo waliokuwa AFCON, kwa maana hiyo walicheza na timu ngumu, ambayo pia nayo ilikuwa inawania kufuzu hatua hiyo kwa hali yoyote ile.
Ikawa ni kama mechi ya fainali kwa Simba Queens, tena haikutakiwa hata sare kwa sababu isingefuzu zaidi ya ushindi.
Kutokana na uwekezaji wa Mohamed 'Mo' Dewji, na safu yote ya uongozi wa Bodi ya Wakurugenzi, benchi la ufundi yalifanyika maandalizi kabambe ambayo yamewezesha kufikia ndoto iliyokuwa inaotwa, tena kwa muda mfupi tu kwenye soka la kinadada.
Hongera nyingine ziende kwa wachezaji kwa sababu mbali na matatizo ya hapa na pale ya kiufundi, lakini walionekana kucheza kwa kujituma na ari kubwa ya upambanaji na ndiyo kwa kiasi kikubwa siri ya mafanikio.
Ukiangalia wachezaji wa Simba Queens wanaoshiriki fainali hizo za Ligi ya Mabingwa ni wale wale tu ambao walicheza hatua za awali ya ligi hiyo kwenye kanda na hakuna mchezaji aliyeongezeka.
Si kwa sababu haina wachezaji wengine wapya, bali walikataliwa na CAF kwa sababu ya kusajiliwa nje ya muda. Kwa mujibu wa Meneja wa Klabu ya Simba Queens, Selemani Makanga, wachezaji hao ni straika Jentrix Shikangwa na kiungo Ruth Ingotsi wote raia wa Kenya ambao waliongezwa kwa ajili ya kukipa nguvu kikosi, lakini ikashindikana.
"Hawa tuna mkataba nao, lakini kwa bahati mbaya tuliwasajili wakati dirisha limefungwa, tumejaribu kupambana sana lakini imeshindikana. Unajua walimaliza mikataba yao wakati dirisha likiwa wazi na walikuwa hawajapata timu, wakaja kupata wakati dirisha limefungwa.
FIFA inasema kama dirisha lingekuwa limefungwa kabla mikataba yao kumalizika, wangeweza kuwasaidia pale mikataba yao ingekuwa imekwisha, lakini mikataba ilikuwa imekwisha na dirisha liko wazi, hivyo hawaruhusu kitu kama hicho," alisema meneja huyo.
Kwa ninavyowajua wachezaji hao, hasa Shikangwa, kinara wa mabao wa Ligi ya Wanawake Kenya, pamoja na michuano ya CECAFA kwa wanawake mwaka 2019, na akafunga bao la pili kwenye mechi ya kirafiki hivi karibuni dhidi ya Yanga Princes, sidhani kama kuna timu ingeizuia kutwaa ubingwa huo.
Lakini hata hapo walipofikia akinadada hawa, wameiheshimisha nchi na CECAFA kwa ujumla, pia malengo ya klabu yamefikiwa. Hongereni sana na endeleeni kupambana kwani kutwaa ubingwa inawezekana.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







