COP27 imeanza Misri, Watanzania tufuatilie inatuhusu

06Nov 2022
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
Nawaza kwa Sauti
COP27 imeanza Misri, Watanzania tufuatilie inatuhusu

MOJA ya matatizo makubwa yanayoikabili dunia, Tanzania ikiwamo, ni kasi ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha madhara mengi kama sasa tunavyoshuhudia hakuna mvua za kutosha. Ukame uko kila mahali huku binadamu na wanyama wakipoteza maisha kwa kukosa maji na malisho.

Mabadiliko ya tabianchi hayasababishwi na eneo fulani pekee bali mchango wa dunia kwa ujumla, huku nchi za Afrika kwa ujumla wake zikichangia hewa ukaa chini ya asilimia nne na nchi zilizoendelea zikichangia kwa kiasi kikubwa.

Kwa Tanzania, mathalan, mtu mmoja anachangia gesi ukaa kwa asilimia 0.22 kwa mwaka huku China na Marekani zikichangia asilimia 26 kwa kipindi hicho hicho. Hii ni kutokana na shughuli za viwanda na nyinginezo ndiyo maana nchi hizo zinatoa fedha za kusaidia kukabili kwa nchi zilizotunza mazingira.

Hadi sasa hakuna mpango kwa nchi hizo kupunguza viwanda na ndiyo  kwanza vinaongezeka na ziko tayari kuendelea kutoa fedha kwa nchi zinazochangia kupunguza hewa ukaa kwa kutunza mazingira.

Kwa sasa kila eneo linakabiliwa na ukame huku maji ambayo ni muhimu kwa kila kiumbe yakiendelea kupungua, migogoro baina ya binadamu na binadamu; wanyama na binadamu inaongezeka kwa sababu raslimali hiyo inapotea katika maeneo mengi.

Ukisafiri kwa anga utaona hali ilivyo ardhini, lakini kasi ya kupaa kwa bei ya nafaka kulikochagizwa na kupaa kwa bei ya mafuta ni udhihirisho kwamba ukame ni tishio. Pia unaona mito na maeneo mengine yalivyokauka.

Hivi karibuni, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ilieleza kuwa mikoa 14 inayopataga mvua za vuli hazitakuwepo na kwamba ukame utaendelea kutamalaki.

Mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi COP27 ulioanza leo jijini Cairo, Misri, unawaleta pamoja wakuu wa nchi 100 na washiriki wengine 35,000 ikiwa ni mwaka mmoja tangu COP26 ifanyike Scotland iliowaleta pamoja wakuu wa nchi 120 na washiriki wengine 40,000.

Katika mkutano huu, Afrika itawasilisha mambo sita ambayo ni kutotimizwa kwa ahadi ya kutoa Dola bilioni 100 kila mwaka hadi mwaka 2020 kwa nchi zilizoathiriwa na mabadiliko ya tabinchi ikiwa ni ahadi ya nchi zilizoendelea tangu mwaka 2009 ambazo zinazalisha hewa ukaa kwa wingi.

Pia zitatoa fidia ya uharibifu uliosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, kwamba Afrika imechangia uharibifu kwa asilimia 0.04 lakini ndiyo inayobeba mzigo mzito licha ya kwamba jambo hilo halijapewa kipaumbele na sasa litasukumwa zaidi kwenye mkutano huu.

Ahadi nyingine ni kupunguza hewa ukaa kwa nyuzi joto 1.5 hadi mwaka 2030, lengo ambalo halionyeshi dalili hasa kwa nchi zilizoendelea ambazo zina viwanda vingi vinavyozalisha hewa ukaa.

Lingine ni kuhama kutoka matumizi ya nishati chafu kwenda kwenye nishati safi, kuacha kutumia makaa ya mawe na kuhamia kwenye gesi,jua na joto ardhi.

Hadi sasa tunaona uhaba wa nafaka huku ikizidi kupanda bei, ongezeko la migogoro baina ya binadamu na wanyamapori ambao wanatoka maeneo yaliyohifadhiwa kwenda kutafuta malisho, huku binadamu nao wakivamia maeneo ya hifadhi kupata mahitaji ya Wanyama wafugwao.

Kwa sasa maji ya bahari na maziwa yanaingia kwenye makazi ya watu kutokana na kuongezeka kwa kina cha maeneo hayo. Maeneo yaliyokuwa yanafaa kwa kilimo hayafai tena kwa sababu maji ya chumvi yameharibu ardhi, pia majisafi hayapatikani tena.

Aidha, mito na maziwa yanakauka huku mabwawa yakikosa maji kabisa. Hivi  karibuni, kwa mfano, wananchi wa Monduli waliiomba serikali kuwapelekea maji kwa kuwa hali ni mbaya sana.

Jitihada nyingi zimefanyika ikiwamo kuhamasisha wananchi kutunza mazingira, kupanda miti kwa wingi na kuachana na matumizi ya nishati ya kuni, ingawa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kwa kuwa mkaa unatumika zaidi kutokana na kupaa kwa bei ya gesi.

Hali ya upatikanaji wa chakula ni ngumu sana kwa sasa, nafaka zimepanda bei hali ya maisha inakuwa ngumu kutokana na visababishi vingine kama kupanda kwa bei ya mafuta kutokana na vita ya Ukraine na Russia  pamoja na UVIKO -19.

Mabadiliko ya tabianchi si jambo la kulichukulia kirahisi, hivyo ni lazima nchi iendeleze mikakati yake ya kusaidia wananchi wake kuishi na hali hiyo ambayo haiwezi kuisha leo wala kesho kutokana na kasi ya ukuaji wa maendeleo.

Lazima jamii yetu iendelee kuelimishwa namna ya kutumia fursa katikati ya matatizo, mathalani kwa sasa kuna biashara ya hewa ukaa kwa wananchi waliotunza misitu ya asili, misitu ya kupanda na binafsi ambayo wanauza duniani kwa nchi zinazoharibu mazingira.

Misitu hiyo inasaidia kupunguza hewa ukaa kwenye anga na kukabili hali iliyopo sasa ya vipindi vya mvua kutoeleweka, ukame wa muda mrefu, joto na baridi kali kiasi cha kuathiri binadamu na viumbe wengine kama tunavyoona sasa maeneo mengi yana joto kali hadi misitu inawaka yenyewe na kwingine baridi sana.

Usalama wa chakula kwa sasa uko hatarini kwa kiasi kikubwa. Wananchi  hawana uhakika wa mlo kamili kutokana na kutokuwa na uhakika wa chakula chenyewe ili waendelee kuwa hai.

Kwa mantiki hiyo, kupambana na mabadiliko ya tabianchi ni lazima kwa kila mmoja lakini wananchi kutumia mbinu zao na za jumla kukabili hali hii ili dunia iwe salama kwa kila mmoja anayestahili kuifurahia.

Tunasikia migogoro baina ya wanyama na binadamu inashamiri, wanyama wanatoka kwenye maeneo yao ya asili kutafuta malisho na binadamu anapeleka mifugo maeneo yaliyohifadhiwa kutafuta malisho. Hii inafanya maisha yasiwe na amani kwenye maeneo mengi.

Mabadiliko ya tabianchi ni tishio lazima tuwe na mbinu zinazotekelezeka, kubuni namna ya kuendelea kupata maji ya mahitaji ya nyumbani na kilimo cha umwagiliaji kwasababu cha mvua hakijaonyesha manufaa chanya.