Maneno hayo yalielekezwa kwa baadhi ya wachezaji wao, kocha pamoja na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo.
Baada ya suluhu hiyo ya nyumbani ni kama vile wanachama na mashabiki wa Yanga wamekata tamaa ya kwenda kushinda ugenini, hasa wakikumbuka kwenye mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya Al Hilal ilikuwa kama hivyo, wakitoka sare ya bao 1-1 nchini na kwenda kuchapwa bao 1-0 nchini Sudan.
Ikasemwa na baadhi ya viongozi kuwa wamejifunza kutokana na makosa, lakini hali ikajirudia vile vile licha ya kuaminishwa kuwa kila kitu kiko sawa.
Nadhani hili ndilo lililowafanya baadhi ya wanachama na mashabiki wapandwe na hasira ya kuongea maneno mengi makali dhidi ya viongozi wao.
Hali hii imemfanya Rais wa Klabu hiyo Injinia Hersi Said kuibuka na kutengeneza kipindi cha kuongea na Wanayanga, akichukua fursa hiyo kujibu baadhi ya yale ambayo wanachama wa Yanga walikuwa wakiyapigia kelele.
Kwa kifupi yeye na viongozi wenzake wa chini, walisikika wakisema wameyasikia yote ambayo wanachama na mashabiki wameyasema, hivyo watayafanyia kazi.
Kwangu mimi binafsi naona kuwa hakukuwa na ulazima wowote wa Yanga kujitokeza na kujibu maneno ya hasira za mashabiki kwa sababu hakukuwa na jambo lolote baya ambalo limefanyika kwenye mechi ile. Yanga haikufungwa, ingawa haikupata matokeo kwenye mechi hiyo. Hili ni jambo la kawaida sana kwenye soka.
Hebu fikiria tayari viongozi wa Yanga wamejitokeza na kujibu maneno ya mashabiki, kama ikitokea bahati mbaya ikatolewa itakuwaje? Ina maana mashabiki wakichachamaa watakuja tena na kuwaambia tena mashabiki wamesikia malalamiko yao na watayafanyia kazi?
Moja ya malalamiko ya mashabiki wa Yanga ni kutaka kocha Nasreddine Nabi atimuliwe, je hayo ndiyo moja ya mambo ambayo viongozi watayafanyia kazi?
Mimi nadhani Wanayanga waliongea siku ile kwa sababu ya hasira tu ya kushindwa kupata ushindi kwa hiyo sidhani kama waliongea kitu chochote cha kujenga, zaidi ya jazba tu.
Ni sawa tu na wanandoa ambao wanapogombana maneno ya hasira zao ni kuachana na kupeana talaka, lakini siku ya pili ukimuuliza yoyote kuhusu hilo hawezi kukujibu. Kila mmoja hataki kitu kama hicho kitokee.
Viongozi wa Yanga ambao wengi wao ni vijana wajue kuwa wanaongoza taasisi kubwa yenye watu wengi na wenye tabia mbalimbali kwa hiyo wanatakiwa kuwa na 'ngozi ngumu' kama za wanasiasa hivi na si kila kinachosemwa basi viongozi wanajitokea haraka kukijibu. Mengine yanasemwa tu kwa ajili ya mihemko na baada ya siku mbili mawimbi yanatulia, maisha yanaendelea.
Hivi ndivyo walivyokuwa wanaishi viongozi wa klabu kubwa za Simba na Yanga wa zamani ambao wengi wao walikuwa wanachaguliwa wakiwa na umri mkubwa. Sababu yake ni kuweza kuhimili presha kama hizi.
Hili lililotokea kwa Yanga, viongozi wajue ni dogo sana na watakutana na makubwa zaidi ya haya kwa sababu timu haitoweza kushinda kila siku, lakini pia kuna mengine yanaweza kujitokeza hata walikotoka hakujulikani.
Kuna viongozi waliiongoza Yanga ikiwa na migogoro mikubwa, lakini bado waliweza kuhimili presha za wao wenyewe ndani kwa ndani, na hata nje kwa wapinzani wao.
Hebu tuangalie mfano wa wenzao Simba, kabla ya ligi kulikuwa na presha kubwa kutoka kwa mashabiki juu ya kikosi chao kuwa ni kibovu, lakini walikaa kimya. Baadaye likaja suala ya Selemani Matola. Baada ya mechi dhidi ya KMC sare ya bao 2-2 mashabiki wakitaka Matola atimuliwe, hatukusikia kiongozi yoyote wa Simba aliyejibu chochote, badala yake timu ilikwenda nchini Malawi ikashinda. Kila mashabiki wakisema Matola aondoke, husikii ufafanuzi wala kiongozi anayepata na kuongea kwenye vyombo vya habari. Hii inaonyesha kuwa wanaoongoza klabu hiyo tayari wana uzoefu kwenye soka na wanawafahamu vilivyo.
Rai yangu kwa viongozi wa Yanga mambo mengine wayaache yapite kama maji kwenye mkondo wake. Wakisema kila kitu ambacho mashabiki watalipuka nacho basi wajibu, watakuwa na kazi ngumu sana kwenye uongozi wao. Wajikite zaidi kwenye kuongoza klabu na si kuongozwa na maneno ya watu.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







