Kwa sasa hakuna mkoa ambao haujakumbwa na tatizo hilo kwa kuwa kila wakati matukio hayo yanaripotiwa katika vyombo vya habari.
Kwa ujumla, ajali hizo zimekuwa zikisababisha baadhi ya watu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa au kupata ulemavu wa kudumu. Baadhi ya sababu ambazo zimekuwa zikitajwa kuwa chanzo cha ajali hizo ni mwendokasi unaosababishwa na madereva, kukosekana kwa umakini wakati wa uendeshaji wa vyombo vya moto, hitilafu au kasoro katika magari na matumzi ya vileo kwa baadhi yao madereva.
Kutokana na ongezeko la ajali hizo, serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali zikiwamo kuagiza madereva wanaosababisha ajali kuchukuliwa hatua za kisheria, kufutiwa leseni na kufumua uongozi wa kikosi cha usalama barabarani ambacho ndicho chenye dhamana ya kuhakikisha ajali zinadhibitiwa.
Hivi karibuni, kwa mfano, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Camillus Wambura, alifanya mabadiliko ya makamanda wa jeshi hilo makao makuu na mikoa ambayo pia yalikigusa kikosi hicho. Aliyekuwa Mkuu wa Kikosi hicho, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Wilbroad Mtafungwa, aliondolewa na kwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, SACP Ramadhani Ng’anzi, kupewa wadhifa huo.
Mabadiliko hayo ndani ya trafiki, yameongeza chachu zaidi katika utendaji wa kikosi hicho kutokana na baadhi ya wakuu katika mikoa, kuonekana wakichukua hatua mbalimbali katika kupambana na madereva wanaosababisha ajali ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu.
Mmoja wa wakuu hao ni yule wa mkoa wa Iringa, Mrakibu (SP) Mossi Ndozero, ambaye wiki iliyopita, kikosi chake kiliwapeleka madereva wa mabasi makubwa waliokamatwa kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani katika wodi za majeruhi wa ajali kuona wanavyoteseka kutokana na uzembe unaofanywa na baadhi yao. Madereva waliopelekwa katika wodi hizo ni wale waliokamatwa na wengine kufutiwa leseni kwa makosa mbalimbali ikiwamo kuendesha kwa mwendokasi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Ndozero alisema waliamua kufanya hivyo ili madereva hao wajionee namna majeruhi wanavyoteseka kutokana na ajali za barabarani. Alisema madereva hao walipelekwa katika wodi za wanaume na wanawake za majeruhi hao ikiwa sehemu ya mafunzo kwa kundi hilo.
Kwa jumla, uamuzi wa kuwapeleka madereva hao ulikuwa mzuri kwa sababu wengi wao, pindi ajali zinapotokea wamekuwa wakikimbia na kuwatelekeza abiria na magari, hivyo kushindwa kutambua ni namna gani waathirika wanateseka.
Ni uamuzi wa kuungwa mkono pia mfano wa kuigwa kwa sababu madereva hao wamejionea kwa macho yao ni jinsi gani ajali zinavyosababisha matatizo mbalimbali vikiwamo vifo na majeraha. Pia wamejionea madhila wanayoyapata watu ikiwamo kupoteza muda wa kuzalisha kwa sababu ya matibabu au kuuguza ndugu zao.
Uamuzi huo pia unaonekana ni mzuri kwa sababu utakuwa umewapa mwanga madereva hao kwamba wana dhamana kubwa ya kulinda uhai wa watu, hususani abiria wanaopanda kwenye vyombo vya moto wanavyoviendesha.
Licha ya uamuzi huo, baadhi ya watu walisema madereva hao wangepelekwa kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti ili waonyeshwe watu waliopoteza maisha kutokana na ajali. Lakini itoshe tu kusema kupelekwa katika wodi hizo ni funzo kubwa kwao ili kutambua maumivu wanayoyapa waathirika wa ajali za barabarani zinazochangiwa kwa kiasi kikubwa na madereva hao.









