Hatua ya serikali itapunguza kilio wananchi uhaba wa maji

04Nov 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hatua ya serikali itapunguza kilio wananchi uhaba wa maji

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)  hivi karibuni ilitangaza kuwapo kwa mgawo wa maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kutokana na kupungua kwa kina cha maji katika Mto Ruvu, hivyo kuathiri uzalishaji wa huduma hiyo muhimu. 

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kamati za ulinzi na usalama za mikoa hiyo zikiongozwa na wakuu wa mikoa, kutembelea maeneo ya uzalishaji wa maji na kujionea upungufu mkubwa katika vyanzo hivyo. Katika kutekeleza hilo, DAWASA ilitoa ratiba ya mgawo ili kuhakikisha pamoja na upungufu huo, wananchi wanapata huduma hiyo muhimu kwa maisha ya kila siku.

Pamoja na kuwapo kwa ratiba hiyo, kumekuwa na vilio kutoka kwa wananchi kila kona wakilalamikia kutokufuatwa, hivyo makali ya upatikanaji wa maji kuzidi kuongezeka. Pia kumekuwa na ‘maandamano’ ya wananchi kusaka maji kila sehemu jambo linaloashiria kuwa shida ya maji inaongezeka.

Kuwapo kwa hali hiyo, kumesababisha serikali kuingilia kati ili kujaribu kupunguza makali ya ukosefu wa maji kwa wananchi wa mikoa husika kwa kutafuta vyanzo mbadala tofauti na kile cha Mto Ruvu ambacho kina cha mto kimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na ukosefu wa mvua uliosababisha pia ukame.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliingilia kati tatizo hilo kwa kutoa maagizo kwa Wizara ya Maji kushirikiana na sekta binafsi kutekeleza mradi wa kutoa maji Mto Rufiji ili kusambaza maji maeneo ya mikoa ya Pwani na Dar es Salaam. Sambamba na hilo, aliielekeza DAWASA kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya uchimbaji wa visima zaidi ili kuongeza uzalishaji wa maji.

Majaliwa alitoa maagizo hayo baada ya kuelekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha anasimamia uunganishwaji wa maji kutoka Kigamboni kwenda maeneo mengine ya Dar es Salaam. Majaliwa alisema visima vya Kigamboni vina uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 70 kwa siku, hali ambayo itasaidia kupunguza tatizo la maji katika mkoa wa Dar es Salaam.

Hatua ya serikali kuingilia kati kupunguza tatizo la maji mkoani Dar es Salaam imekuja wakati mwafaka hasa kutaka ushiriki wa sekta binafsi kutoa huduma kwa kutafuta vyanzo vya maji ikiwamo kutoa maji Mto Rufiji na kuyafikisha Dar es Salaam.

Ni imani kwamba ushiriki wa sekta binafsi katika uzalishaji maji utasaidia kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa maji badala ya kutegemea DAWASA pekee ambayo ni dhahiri inaonekana kushindwa kutimiza mahitaji. Hii inatokana na ukweli kwamba katika mkoa wa Dar es Salaam, mathalan, kuna ongezeko kubwa la watu lakini upatikanaji wa maji ni mdogo.

Suala la kutoa maji mto Rufiji ni la kupongezwa licha ya kwamba miaka nenda rudi kumekuwa na kilio cha kufanya hivyo kwa kuwa maji yanayotoka katika vyanzo mbalimbali na kuingia katika mto huo, yamekuwa yakiishia baharini huku wananchi wakiteseka.

Pamoja na hayo, ni vyema DAWASA ikaacha ukiritimba wa utoaji wa huduma ya maji huku ikiweka masharti magumu kwa watoa huduma binafsi wakiwamo wamiliki wa visima ambao kabla ya mtandao wa mamlaka hiyo kuenea, walikuwa wanawasaidia wananchi kupata maji. Baadhi ya wamiliki wa visima binafsi walikuwa wakiweka mtandao wa mabomba kwenye makazi ya watu, hivyo kufidia pengo lililokuwapo la upungufu wa maji.