Yanga malizeni kazi kwa Mkapa kufuzu shirikisho

31Oct 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga malizeni kazi kwa Mkapa kufuzu shirikisho

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, keshokutwa, Jumatano watatupa karata yao ya kwanza dhidi ya Club Africain ya Tunisia kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga ambayo itakuwa mwenyeji kwenye mechi hiyo ya kwanza itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, imeangukia hatua hiyo ya kucheza mechi ya mtoano kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, baada ya kutolewa katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1.

Hivyo, kwa mujibu wa kanuni za waandaaji wa michuano hiyo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF), timu zote zinazotolewa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa, hucheza mechi ya mchujo nyumbani na ugenini dhidi ya zilizopenya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho ili kuwania kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Kwa mantiki hiyo, Yanga inahitaji kupata matokeo ya jumla nyumbani na ugenini dhidi ya Watunisia hao, ili kufuzu hatua hiyo ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu Afrika.

Kikubwa Yanga inachotakiwa kufanya ni kuhakikisha keshokutwa inapata ushindi mkubwa wa magoli ili kurahisisha kazi katika mechi ya marudiano Novemba 9, mwaka huu nchini Tunisia.

Tunatambua ujanja wa timu za Mashariki, maarufu za Kiarabu, ambao huutumia zikiwa ugenini, huhakikisha zinapoteza muda kwa kujiangusha, kutoa presha kwa mwamuzi kwa kumlalamikia mara kwa mara, huku zikitumia mashambulizi ya kushtukiza.

Hivyo, Yanga haina budi kuwa makini katika ujanja huo na kuepuka kuingia mtegoni kwenye mbinu hizo za Waarabu kwani mara nyingi wanachotafuta ugenini ni sare na ikiwezekana ya mabao ili baadaye kwenda kunufaika na bao la ugenini.

Sote tulishuhudia namna Club Africain walivyocheza kwa mbinu hizo kwenye raundi ya kwanza dhidi ya Kipanga FC ya Zanzibar na kufanikiwa kupata sare tasa katika Uwanja wa Amaan visiwani humo.

Matokeo hayo yaliifanya Kipanga kuiona Club Africain ni ya kawaida na kuamini inaweza kwenda kuwachapa kwao, lakini ilipofika Tunisia, ilibebeshwa kitu kizito kichwani kwa kuchapwa mabao 7-0 na kutolewa kwenye michuano hiyo.

Hivyo, Yanga haina budi kukwepa mtego huo kwa kuhakikisha inapata mabao mengi nyumbani na kutoruhusu wapinzani wao kuziona nyavu zao, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya makundi katika mechi ya marudiano.

Tunatamani kuiona timu nyingine kutoka Tanzania ikifuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo ya CAF kwa ngazi ya klabu baada ya Simba kuwa klabu pekee kutoka nchini kutinga hatua hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Inafahamika wazi kuwa na timu zaidi ya moja kwenye hatua ya makundi katika michuano hiyo ya CAF, zinasaidiana kuiongezea nchi pointi na kuiweka katika nafasi nzuri ya kuingiza timu nne kwenye mashindano hayo msimu unaofuata.

Hivyo, tunaamini Yanga imefanya na inaendele kufanya maandalizi makubwa kuelekea mechi hiyo ya mchucho, lakini ikichukua tahadhari zote nje na ndani ya uwanja na katika hilo Nipashe tunaungana na wadau wote wa soka na Watanzania kwa ujumla kuwaunga mkono wawakilishi wetu hao wa nchi kimataifa ili kufanikisha lengo lao la kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushindwa kwenye Ligi ya Mabingwa.