Kila la kheri Simba Queens Ligi ya mabingwa Afrika

29Oct 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kila la kheri Simba Queens Ligi ya mabingwa Afrika

MICHUANO ya soka la Ligi ya mabingwa Afrika kwa Wanawake inatarajia kuanza kesho Jumapili jiji Rabat nchini Morocco.

Michuano hiyo inashirikisha klabu za soka za Wanawake ikiwa ni mara ya pili tangu kuanzishwa kwake. Mara ya kwanza ilifanyika nchini Misri mwaka jana na klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ndio iliibuka kuwa mabingwa.

Simba Queens imepangwa katika Kundi A na itafungua pazia la mashindano haya Jumapili kwa kuwavaa wenyeji ASFAR Queens mchezo utaanza majira ya saa 4:00 usiku kwa saa za Tanzania.

Kikosi cha Simba Queens kilitua salama jijini Rabat mapema wiki hii tayari kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo na Meneja wa timu hiyo, Selemani Makanya, alisema wachezaji wote wako katika hali nzuri na wanasubiri kuanza kupeperusha vyema bendera ya klabu na Tanzania.

Kwa mujibu wa Makanya kikosi kilianza mazoezi juzi usiku na wanashukuru hali  ya hewa kwa sasa jijini humo ni nzuri na inafanana na ile ya Dar es Salaam.

Meneja huyo aliongeza anafurahi kuona kila mchezaji aliyesafiri kwenda huko anashauku kubwa ya kutimiza kile ambacho mashabiki, wanachama na viongozi wa Simba wanachokisubiri.

Naye Ofisa Habari wa Simba, Ally Shatry 'Chicco' alisema kwa upande wa utawala maandalizi yote kuelekea mashindano haya yamekamilika na wamejipanga vizuri.

Tukiwa kama wadau wakubwa wa michezo hasa soka, tunachukua nafasi hii kuitakia kila la kheri Simba Queens katika mashindano hayo ambapo ni moja ya sehemu ya kuitangaza tanzania kupitia mchezo huo duniani kote.

Tuna imani na wachezaji hawa wanawake kwamba wanaweza kufanya vizuri na hata kulibeba taji la michuano na kutua nalo Tanzania kwa mara ya kwanza katika historia yake.

Wakati tukiwa na kumbukumbu nzuri ya timu ya nchini India, basi tuna matumaini makubwa kwa Simba Queens.

Ikumbukwe baadhi ya wachezaji hao wa Serengeti Girls wapo katika kikosi cha Simba Queen, tunaamini watatumia vizuri zaidi uzoefu walioupata kwenye michuano ya kombe la dunia kwa kushirikiana na wachezaji wenzao kufanya vizuri.

Serengeti Girls ilifanikiwa kufika robo fainali ya mashindano hayo, huku ikiwafunga wababe wa Dunia Ufaransa katika kinyang’aniro hicho.

Hivyo, Nipashe tunaamini kabisa kwamba, Simba Queens wanaweza kuiga mafanikio waliyoyapata Serengeti Girls na kufika mbali zaidi katika mashindano haya ya Klabu bingwa Afrika.

Wito wetu kwa benchi la ufundi ni kuhakikisha wanawapa mbinu za kutosha wachezaji hao ili kuhakikisha kwamba, wanafanya vizuri zaidi kama sio kulibeba taji hilo.

Kwa upande wa wachezaji, tunaamini watatumia vizuri maelekezo ya benchi la ufundi chini ya kocha mkuu kuhakikisha wanacheza kwa bidii na maarifa ili kuibuka na ushindi katika kila mchezo.

Kufanya vizuri kwa Simba Queens kwenye mashindano hayo tutaipa nafasi nzuri zaidi Tanzania kuendelea kutambulika kisoka duniani na pia kuwapa nafasi nzuri zaidi wachezaji kuonekana  kusajiliwa na klabu mbalimbali kubwa duniani.

Taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 17, Serengeri Girls namna ilivyotubeba kwenye michuano ya kombe la Dunia

Tunawatakia kila la kheri Simba Queens.