Mvua za vuli zilizotarajiwa kuanza kunyesha kwa mujibu wa utabiri zitakuwa na uhaba kwenye mikoa 14.
Mikoa hiyo imetajwa kuwa ni Ruvuma, Rukwa, Mbeya, Iringa, Njombe, Katavi, Dodoma, Tabora, Mtwara, Lindi, Songwe na Kigoma huku maeneo ya Kusini mwa Mkoa wa Morogoro inatarajiwa kupata mvua chache katika kipindi cha msimu huu kitakachoanza Novemba na kumalizika Aprili, mwakani.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa Mamlaka hiyo, Dk. Hamza Kabelwa, inatoa tahadhari ya kukosekana kwa mvua hizo ambayo italeta athari katika sekta mbalimbali zikiwamo za kilimo, mifugo na nishati.
Athari za kukosekana kwa mvua zimeshaanza kujitokeza katika maeneo mengi nchini, hivi sasa mgawo wa maji umeanza katika baadhi ya mikoa na sehemu nyingine umeme kukatika mara kwa mara.
Taarifa hiyo ya mkurugenzi imefafanua upungufu huo wa mvua utasababisha kuathiri ukuaji wa mazao na chakula kupungua.
Upungufu huo hauathiri sekta ya kilimo pekee, bali pia kwenye sekta ya nishati ambako mabwawa na mito itapungua maji na kuathiri uzalishaji.
Viumbe pia vitaathirika ikiwamo mifugo ambayo inategemea majani kama chakula na maji kutokana na ukame.
Ukame husababisha hata kutokea kwa migogoro kati ya wafugaji na wakulima katika matumizi ya maji, lakini migogoro ya wanyama na binadamu inaweza kutokea wakati wa kutafuta maji.
Mamlaka hiyo imeshauri watu kuzingatia uvunaji na utunzaji wa maji ili kukabiliana na tatizo hilo.
Pia mamlaka hiyo imesema nusu ya kwanza ya msimu huu kuanzia Novemba 2022 mpaka Januari 2023 kunatarajiwa vipindi virefu vya ukavu lakini kunatarajiwa nusu ya pili ya msimu ambao ni kuanzia mwezi Februari mpaka Aprili 2023 kuwapo ongezeko la mvua zitakazoisha wiki ya nne ya mwezi Aprili.
Mamlaka imefafanua katika kipindi cha Novemba na Desemba upungufu mkubwa wa unyevunyevu kwenye udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi ya mikoa hiyo.
“TMA tunashauri sekta husika kutoa elimu kwa wakulima kulima mazao yanayohimili mvua ndogo na utunzaji wa chakula.”
Katika maeneo mengi ya mikoa hiyo 14, mvua zitaanza wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Novemba.
Tahadhari hiyo ilitolewa na TMA lazima ichukuliwe kwa umuhimu ili nchi iweze kuepuka janga la njaa kwa kukosa chakula cha kutosha.
Athari za mabadiliko ya tabianchi zimekumba mataifa mengi duniani na tumeshuhudia jinsi watu wanavyohangaika kwa kukosa chakula na maji. Hata mifugo imeathirika na kufa kwa kukosa malisho na maji.
Nchi yetu imejaliwa kuwa na mito, maziwa yenye maji mengi ambayo kama wataalamu watawezesha kutumika kwa matumizi ya nyumbani na umwagiliaji mashamba kutaokoa janga hili linalotaka kutupata.
Ni muhimu pia kumuomba Mwenyezi Mungu, atuepushe na janga hili.