Wazazi wenye kichwa kikubwa, mgongo wazi wanolewa ujasiriamali

28Oct 2022
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Wazazi wenye kichwa kikubwa, mgongo wazi wanolewa ujasiriamali

WAZAZI na walezi wa watoto wenye ulemavu wa kichwa kikubwa na mgongo wazi, wamekuwa wakitumia muda mwingi kukaa hospitalini kuhudumia watoto hao, huku shughuli zao za kiuchumi zikikwama.

Aziza Kasisiko (kulia) na mwenzake Sane Mashishanga, wakiwa na vifaa walivyotengeneza, baada ya kupata mafunzo ya ujasiriamali.

Sehemu kubwa ya watoto wenye ulemavu huo, wamekuwa wakilazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), jijini Dar es Salaam. Na kwingineko ambako hukaa hata kwa zaidi ya miezi sita. 

Hiyo ni kutokana na wanakaa muda mrefu hospitalini, shughuli zao za kuwaingizia kipato hasa kilimo, huwa zinalala, ambapo sasa umeanzishwa utaratibu ambao utawawezesha kukabiliana na ugumu wa maisha.Taasisi hiyo imeanzisha utaratibu wa kuwapa ujasiriamali, ili wanapoondoka kurudi kwao, wakautumie kwa kutengeneza vitu mbalimbali na kuviuza ili kujiongezea kipato kwa ajili kuendesha maisha. 

Utaratibu huo ni wa kuwapa mafunzo ya kutengeneza vitu mbalimbali umeanzishwa na taasisi hiyo baada ya kubaini kuwapo kwa changamoto ya ugumu wa maisha kwa akina mama hao ambao wengi wao wanatoka vijijini.

MKURUGENZI MOI

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface, anasema hayo kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kichwa Kikubwa na Mgongo Wazi yaliyofanyika kimkoa kwenye taasisi hiyo, jijini Dar es Salaam."Tulianza utaratibu huu tangu mwaka 2017 na tumeshatoa mafunzo kwa kinamama 135, Desemba mwaka jana tuliwapa mtaji akina mama 120 ambao walionyesha nia ya kufanya biashara," anasema Dk. Boniface. 

Katika ufafanuzi wake, Dk. Boniface anasema, wapo kinamama ambao kila mmoja alikabidhiwa Sh. 100,000 na wengine kila mmoja alipata 150,000 kulingana na biashara anayotaka kuifanya. 

"Wale ambao kila mmoja alipewa Sh. 100,000 waalipata pia vifaa vya kutengeneza bidhaa kama shanga au vikapu, wale wa 150,000 kila mmoja, ni wale wanaokwenda kufungua magenge au kununua pembejeo," anasema. 

MTAJI UNAKOTOKAOfisa Ustawi wa Jamii wa MOI, Theresia Jacob, ambaye pia ni mkufunzi wa ujasiriamali, anasema taasisi hiyo ina wafadhili watatu wanaoisaidia, inazidi kuboresha huduma kwa watoto hao. 

"Wafadhili hao Tema Traders, Yunis & Naomi na Mr & Mrs Gilbert Mrema ndio ambao pia wanatusaidia kwa kutupa mitaji tunayoigawa kwa wanawake wenye watoto wa ulemavu huo, ili ziwawezeshe kuanzisha biashara mbalimbali ili kujikimu kimaisha," anasema.

Theresia anasema, amekuwa akiwafundisha wanawake hao kutengeneza bidhaa kama shanga, vikapu, bangili, hereni na maua ya aina mbalimbali kwa siku mbili kwa wiki ambazo ni Jumanne na Alhamisi.

"Pia watoto wenye ulemavu ambao wanasoma katika shule mbalimbali za msingi na sekondari, huwa wana vipindi vya masomo mara tatu kwa wiki, yaani Jumatatu, Jumatano na Jumamosi," anasema. 

Katika ufafanuzi wake, anasema wanafanya hivyo ili isiwepo tofauti ya uelewa wa masomo kati ya watoto hao waliopo hospitalini na wenzao wanaoendelea na masomo shule, na kwamba wanatumia walimu kutoka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima. 

"Wadau wengine wanaotoa walimu ni Chama cha Maisha Mtoto na Foundation inayoitwa ‘Life for Give Him’, kwani watoto hukaa hospitalini kwa zaidi ya miezi minne na idadi yao hufika 37 kwa mwezi, hivyo tumeona ni vyema wawe na walimu wa kuwafundisha masomo ya darasani," anasema.

WANUFAIKA WANENAAziza Kasisiko, kutoka kijiji cha Nguruka wilayani ya Uvinza mkoa wa Kigoma ni mkulima ambaye hakuwa na ujuzi wowote, anapata mafunzo ya kutengeneza maua kwa kutumia nyuzi. 

"Ninashukuru kupata ujuzi huu kwani umeanza kunisaidia, nimekuwa nikitengeneza maua ya kutembeza mitaani kutafuta wateja ambapo kwa wiki ninaweza kuuza maua nane hadi 10," anasema Aziza. 

Anafafanua kuwa bei ya ua moja ni Sh. 15,000 na kwamba mtaji wake ukiongezeka, atapanua biashara yake hiyo na kuisambaza katika vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Uvinza. 

"Nilipata ujuzi mwaka jana, hivyo ninaamini kwamba kadri Mungu atakavyonijalia, nitazidi kuboresha biashara yangu, ingawa changamoto ni kutembea na mtoto huyu wa miaka mitatu mgongoni," anasema. 

Hata hivyo, anaongeza kuwa kufanya biashara hiyo akiwa na mtoto kuna unafuu kuliko kwenda naye shambani kulima, na kwamba atajitahidi kutunza fedha anazopata ili kuelekeza nguvu kwenye biashara hiyo.

Mnufaika mwingine, Sane Mashishanga kutoka Ikwiriri wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, anasema yeye amepata ujuzi wa kutengeneza vikapu ambavyo amekuwa akiuza kila kimoja kwa Sh. 45,000. 

"Binafsi sijauza sana kwani sina muda mrefu tangu nianze kutengeneza, ila nimefanikiwa kuuza vikapu viwili, ninaamini watu wengi watakapojua kuwa ninafanya kazi hii, watajitokeza kuniunga mkono,"anasema.

UBUNIFU ULIVYOAkizungumzia hatua hiyo, mtaalam wa saikolojia wa Taasisi ya Tanzania Suicide Prevention Coalition (TSPC), ya jijini Dar es Salaam, Mayasa Kalinga anasema, MOI imekuja na ubunifu mzuri kwa wanawake hao na watoto. 

"Unajua baadhi yao wanaathirika kisaikolojia na kukata tamaa hasa kutokana na kwamba huduma za matibabu ya watoto wenye ugonjwa huo ni kubwa halafu wengine wanakimbiwa na waume zao," anasema Mayasa. 

Mama huyo anaeleza kwamba, kitendo cha MOI kuwapa mafunzo ya ujasiriamali, kinawasaidia kufanya biashara mbalimbali na kupata kipato cha kuwasaidia angalau kuwahudumia watoto wao. 

"Ikumbukwe kuwa wengi wao hawana kipato cha kutosha halafu wanaachiwa kulea watoto wenye ulemavu huo bila msaada kutoka kwa waume zao, kisaikolojia ni lazima watakuwa na mwazo mengi vichwani," anasema Mayasa. 

Kwa mujibu wa mama huyo, kitendo cha kuwapa mafunzo na mitaji, kinaweza kuwafanya wakawa na matumaini mapya, katika malezi ya watoto hao, huku wakijitahidi kuhakikisha wanajiingizia chochote kupitia ujuzi waliofundishwa. 

Top of Form

Bottom of Form

Top of Form

Bottom of Form