Hadi sasa wapo wananchi wanaotumia huduma hiyo pamoja na wanyama pori na wafugwao vijijini na hata mijini.
Ni vyema taasisi hizo za serikali kusaidia kudhibiti bei za maji hasa yanayochimbwa mitaani ambayo ‘cubic liter moja ni tangi la lita 1,000’ wateja huuziwa kwa Shilingi 4,000.
Kinachosikitisha ni kwamba maji hayo yana chumvi, hayajapimwa kufahamu usafi na usalama wake kwa kuchunguzwa kimaabara lakini yamekuwa yakisambazwa kila mahali kutokana na ukweli kuwa kuna fursa ya kuuza maji ya kuchimba kutokana na ukosefu wa maji ya umma na kwa Dar es Salaam na Pwani ya DAWASA.
Ulishaji watu maji ya kuchimba kutoka visima vya ardhini pengine unahitaji ukaguzi na kupimwa, kazi inayoweza kufanywa na RUWASA au Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira.
Wakazi wa maeneo ya Msumi jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa waathirika wa tatizo la maji kwa vile sehemu hiyo haina maji ya DAWASA, hivyo wakazi wake kutegemea maji ya mabondeni ambayo ni machafu lakini hayo ya kununua kutoka kwa wawekezaji wanaochimba maji ya chumvi.
Wengi wanaeleza katika mazungumzo na gazeti hili kuwa wanalazimika kununua mita, mabomba na vifaa vyote vya kuunganisha na kusambaza maji na kuvikabidhi kwa wawekezaji au wenye maji ili wawafikishie maji nyumbani kwao.
Wanasema maji hayo ni ghali na wengi huuza kipimo cha pipa la lita 1,000 kwa Shilingi 3,000 hadi 4,000 kila mwezi na wakati mwingine wanaouza huwauzia wateja Shilingi 150 kwa ndoo au dumu la lita 20.
Ukweli ni kwamba kama walivyosema watabiri kuwa vita vya tatu duniani vitakuwa ni vya maji, changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo hasa eneo la Msumi ni kubwa licha ya kwamba serikali inaendelea na juhudi za kufikisha maji maeneo hayo.
Kinachowaumiza wananchi hao ni ughali wa maji hayo ya chumvi ambayo huuzwa ghali kupindukia kwa kuwa si wote wenye uwezo wa kuyanunua na kulipa zaidi ya Shilingi 3,000 kwa pipa lenye ujazo wa lita 1,000.
Pamoja na kwamba DAWASA imeruhusu watu kuchimba visima na hata wenye magari kuuzia wateja na kuyasambaza hasa sehemu ambazo hazina maji ni vyema pia ikatazama upya eneo hilo.
Ni vyema DAWASA na hata RUWASA kushirikiana na wananchi hasa kwenye eneo la bei elekezi ya maji, kama wananchi wanavyojiuliza hivi ni sahihi kuuza maji ya chumvi kwa Shilingi 4,000 kwa pipa la lita 1,000?
Wana mawazo kuwa pengine ni wakati wa kuja na bei elekezi ya maji yanayouzwa mitaani kutokana na ughali wake pamoja na kuuchunguza ubora wa maji hayo kwanza.
Ni bora DAWASA ikazingatia kuwa wananchi wa kaya maskini hawana uwezo wa kununua maji hayo hasa kwa sababu walikuwa wanategemea maji mabondeni ambayo nayo yamekauka kutokana na upepo mkali na ukame unaotikisa karibu kila mkoa.
Pamoja na jitihada za kusambaza maji na kupanua vyanzo ili kuongeza kiwango cha maji yanayozalishwa na serikali, suala la kukagua visima vinavyochimbwa mitaani linahitaji jicho la serikali.
Pamoja na kuchunguza usalama wa maeneo na vyanzo yanapotoka maji hayo ili kazi zisifanyike kienyeji serikali itoe bei elekezi maana wakati mwingine wananchi wanalipia hata kuliko huduma wanayopata.
Wakati mwingine wananchi wanahisi kuwa iwapo DAWASA au RUWASA zitawaachia wafanyabiashara hao wenyewe bila udhibiti watazidi kuwaumiza wananchi hasa wakati huu wa janga la ukame linalotoakana na mabadiliko ya tabia nchi.


.jpg?itok=nfwjwDzv)







