Yanaweza kuwa malezi nyumbani, shuleni, kazini na ndani ya jamii, ili kuelekeza binadamu atende namna ambayo inamjenga pamoja na jamii nzima.
Maadili yanajumuisha kanuni na imani bora zinazokubalika na jamii. Leo si jambo la kuficha kusema kuwa dunia inaishi katika jamii ambayo sehemu kubwa inaumizwa na mmomonyoko wa maadili kupindukia.
Mmomonyoko huo si tu upo kwa baadhi ya watoto na vijana, lakini pia hata baadhi ya wazazi na walezi, ambapo kimsingi ndiyo walipaswa kuwa kielelezo kizuri cha kuwalea watoto katika misingi ya maadili mema na taratibu zinazokubalika na kila mmoja.
Kutokana na mmomonyoko wa maadili uliopo kwa sasa, jitihada za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kunusuru kikazi cha sasa na kijacho. Hofu ya Mungu, upendo na undugu vimepungua mno badala yake ukatili, chuki, visasi vimechukua nafasi kubwa.
Hapa kuna tatizo kubwa. Vyombo vya habari kama vile runinga, mitandao ya kijamii, magazeti na redio vimekuwa vikitoa taarifa za mauaji, ubakaji, wizi unaofanywa katika maeneo mbalimbali hapa nchini na hata nje ya mipaka ambazo zimekuwa zikisababisha vifo vya watu, ulemavu na hata kurudisha nyumba jitihada za kimaendeleo zinazofanywa na watu binafsi na serikali.
Kujenga maadili kunagusa wadau wengi, lakini msingi mkuu wa ujenzi wake maadili ni katika familia. Hapa kunanikumbusha mwimbaji wa nyimbo za Injili Daniel Thomas, alipotunga wimbo uitwao “Ibada Njema” ambao katika wimbo huo anasisitiza kuwa mambo mazuri yanajengwa na kuanzia nyumbani yaani familia kwanza.
Mwimbaji Daniel katika wimbo huo anasisitiza kujenga kwanza mambo ya nyumbani kabla ya kuanza ya sehemu nyingine. Kushindwa kujenga maadili bora katika ngazi ya familia ndipo kunapoleta ugumu kwa walimu shuleni, viongozi wa dini kwa waumini wao na viongozi wa serikali kwa watumishi na wananchi wao kuwajenga katika maadili mema wakati watu hao wakiwa wamekosa msingi bora wa maadili katika ngazi ya familia.
Hata maandiko matakatifu mfano yanapokumbusha kuhusu malezi bora yakisema: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”. Maandiko na maelekezo hayo yanaweka kielelezo cha kujenga tabia na maadili mema kwa watoto katika ngazi ya familia ambapo wazazi na walezi wanawajibika moja kwa moja kufanya jukumu hilo.
Wanasaikolojia wanaamini kila mtu anazaliwa akiwa na tabia njema, hivyo anahitaji mwendelezo wa kulelewa katika malezi na maadili mema ili kuendelea kuwa na tabia na maadili mazuri. Ugumu uliopo wa kujenga tabia na maadili bora unaweza kupungua au kumalizika kabisa kama wazazi na walezi watatimiza kikamilifu jukumu la kulea watoto wao katika maadili bora.
Ni wajibu wa wazazi na walezi kuwafundisha watoto tabia njema na madili mema nyumbani kukawa sehemu muhimu ya mafunzo kwa watoto.
Ukatili, ubakaji, mauaji ya kutisha, wizi na ujambazi ni matokeo ya mmomonyoko wa maadili. Kama watoto watafundishwa maadili mema katika hatua za mwanzo na za awali za ukuaji wao wakiwa nyumbani kuna uwezekano wa kujenga jamii yenye maadili na heshima.
Wanaojiita ‘panyarodi’ wanaofanya uhalifu na ukatili tena wakati mwingine mauaji ya watu mitaani baada ya kuvunja milango nyumbani hawatakuwepo ikiwa watoto watalelewa katika maadili hofu na kumcha Mungu huku juhudi hizo zikianzia ndani ya familia.
Jukumu jema la kuwafundisha watoto na vijana maadili na tabia njema lianzie nyumbani kwanza, ndipo baadaye liendelee katika nyumba za ibada, shuleni na sehemu nyingine za kijamii.
Gharama za kujenga maadili bora kabla mambo hayajaharibika ni ndogo kuliko kazi za kujenga maadili baada ya mmomonyoko wa maadili kutokea. Jamii ibadilike ili kufundisha na kuimarisha familia, jamii na taifa lenye upendo, amani, utulivu na maendeleo badala ya uhalifu na upotevu ambao ni ulegevu na kukosa bidii kutawala maisha ya watu.