Timu hiyo ambayo awali ilikuwa haitarajiwi kufanya chochote au kuzungumzwa sana, iliwashtua wengi ilipotoa kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Timu ya Taifa ya Ufasansa kwenye mechi ngumu iliyochezwa Uwanja wa Fatorda, Goa nchini India inakofanyika michuano hiyo.
Kwa tulioangalia mechi hiyo, haikuwa nyepesi hata kidogo, badala yake ilibidi wachezaji wa Tanzania kupambana kuweza kuwazuia mawinga wenye kasi wa timu hiyo, wakiongozwa na mchezaji wao tegemeo alionekana kuwa mwiba kwenye safu ya ulinzi ya Serengeti Girls, Lucia Calba, ambaye ndiye aliyefunga bao la kufutia machozi.
Timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka hiyo, inaingia kwenye vitabu vya kumbukumbu ya soka la Tanzania na dunia nzima kuwa pamoja na kutinga fainali hizo, ilishinda mechi yake ya kwanza dhidi ya Ufaransa.
Pia, rekodi haitofutika kuwa mchezaji Diana Mnally ndiye Mtanzania wa kwanza kufunga bao kwenye michuano ya kombe hilo la dunia chini ya umri huo kwa Tanzania.
Inawezekana kama baadhi ya watu wanaona kawaida tu wala hawashtuki, lakini ukiangalia mazingira ya jinsi timu zetu Afrika zinavyojiandaa na wenzetu Ulaya ni vitu viwili tofauti.
Jinsi wachezaji wetu wanavyopatikana, kuvumbuliwa na utamaduni wetu na wenzetu Ulaya ni tofauti.
Kutokana na hali hiyo inabidi si tu kuipongeza Serengeti Girls kwa kuifunga Ufaransa, lakini kuwapongeza kwa kushinda dhidi ya timu na nchi ambazo zina skauti bora ya kutafuta, kukusanya wachezaji, kuwatunza na kuwatayarisha kuliko sisi.
Hata ukiangalia jinsi wanavyocheza, unaona kabisa kuwa wachezaji wa timu pinzani wameanza kucheza soka wakiwa bado wadogo sana kutokana na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kupiga pasi.
Wachezaji wetu wengi bado hawapatikani shuleni wakiwa bado wadogo, lakini wazazi wa Kitanzania ni wazito mno kuwaruhusu watoto wao wa kike tena chini ya miaka 17 kwenda kucheza soka, kukaa kambini au kwenye vituo vya soka.
Wengi wanaanza mpira ukubwani, na hadi anakubaliwa basi kunatokana na msukumo wa mtu au watu fulani ambao wamecheza soka kwenye ukoo au familia, vinginevyo ni marufuku.
Ndiyo maana nasema inawezekana bado kuna vipaji vya wachezaji wengi vipo mitaani, lakini vimefichwa na wazazi. Labda kwa ushindi huo wa Serengeti Girls na wazazi kuwaona watoto wa wenzao wanacheza Kombe la Dunia, wakiwaangalia kwenye luninga, wanaweza kulegeza masharti.
Pamoja na changamoto zote hizo, bado hazikuwazuia vijana hao kuonyesha kile walichojaaliwa nacho na kuweza kuifanya Tanzania kuwika na kuzungumzwa kila kona nchini India na kwingineko.
Ushindi huo pia unaweza kukuza utalii, kwani jana ilishuhudiwa baadhi ya Watanzania waliokuwa huko wakiimba na kucheza, watu wa mataifa mengine wakiwaangalia na kutabasamu.
Nchi yetu sasa itaanza kuzungumziwa vizuri, kila mmoja akitamani kuifahamu zaidi na hata kufika kuishuhudia.
Ni kama DR Congo, watu wanavyopenda kwenda kutokana na kuheshimishwa na wanamuziki maarufu wa huko, Brazil kwa ajili ya soka na wanasoka maarufu kama kina Pele na Jamaica kwa ajili ya Bob Marley.
Mbali na pongezi, tunaendelea kuiombea timu hiyo izidi kuiheshimisha nchi kwa kushinda mechi ijayo dhidi ya Canada ili mbali na kukuza utalii, lakini watu wa mataifa ya nje waanze kuvutiwa na wachezaji wa Kitanzania, wawachukue kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa kwenye nchi mbalimbali.
Nina uhakika baada ya michuano hii, kuna baadhi ya wachezaji hawatocheza tena soka hapa nchini.
%%%%%%