Ni habari za mauaji, kubaka na kujeruhiana badala za kutia matumaini na za maendeleo ya taifa letu.
Mara usikie, baba kambaka mtoto wake, mwingine kamuua mkewe, mke naye kamchoma moto mumewe, mama kamuunguza mtoto wake kwa kudokoa mboga au kuiba pesa na mengine yanayofanana na hayo.
Na katika hali ya kuogopesha ni kwamba kwa jinsi zinavyoendelea kutokea na kusomwa, zinaanza kuwa ni za kawaida sana kiasi kwamba watu wanaonekana kuanza kuzizoea.
Vifo vinavyohusiana na mambo ya mapenzi ndiyo kabisa, watu wanafumaniana na kuuana. Kuna baadhi ya watu wanasema kuwa matukio haya hata zamani yalikuwepo lakini yanaonekana mengi sasa kwa sababu tu kuna vyombo vingi vya habari.
Inawezekana ikawa ni kweli, lakini ukiangalia kwa upande wa pili kuna tatizo lingine nyuma ya pazia ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi.
Wapo wanaoshauri kuwa taarifa hizi zisiwe zinatangazwa kwa sababu zinasababisha watu wazichukulie 'poa' na wengine wakaanza kuiga.
Binafsi naona hii wala si dawa, kama hivi vitendo vya mauaji vingi vikihusiana na mapenzi, ukatili wa kijinsia na unyayasaji wa watu vipo basi viripotiwe tu hata vikiwa vingi kiasi gani na hata kama tunahofia watu wanavizoea, lakini ukweli utabaki kuwa ukweli.
Hii ni sawa na kuficha maiti ndani halafu unapuliza pafyumu ili watu wasijue kama ndani kuna mtu amekufa.
Vitu kama hivi vinapotokea kwa wenzetu ndiyo tunaanza kuona wasomi wakiingia kazini na kuanza kufanya utafiti kujua sababu hasa ni nini?
Tanzania ina wasomi wengi, lakini baadhi yao wanabaki na usomi kwenye makaratasi lakini nchi hainufaiki na usomi wao.
Kwa wenzetu ili kupata tiba au kukomesha mambo haya, wataalamu wanaanza kuchunguza ni kitu gani kwa miaka ya hivi karibuni kinachosababisha watu wanauana kwa sababu ya mapenzi?
Ni kwa sababu wamekuwa na hasira sana kuliko wale wa zamani? Hasira zao zinatokana na nini? Wana wivu sana kuliko baba na babu zao? Kwa nini wao wana wivu sana?
Kuna aina fulani ya vyakula ambavyo kwa sasa watu wanakula vinavyosababisha hawana huruma, au hasira na wivu zaidi kuliko vizazi vilivyopita? Ni vyakula gani hivyo?
Ina maana kizazi cha sasa ndicho kinawagharamia sana wanawake kiasi kwamba wakigundua kuna watu wengine wanaingia penzi lao wanaona uchungu sana?
Je kwa nini watu wengi kwa sasa siyo wale wa kama umepata mwingine, basi na mimi natafuta wangu nitakayeishi naye, badala yake watu wanaanza kutafutana kwa bastola na mapanga?
Tukiondoka huko, tuangalie ni kwa nini hata watu wazima wa sasa wamekuwa 'watu wazima ovyo' kwa kupenda wasichana wadogo?
Mtu mzima wa zamani anaweza kuachwa na mjukuu wake nyumbani kutwa nzima wakacheza, kucheka na kutaniana, lakini kwa sasa wazazi wamekuwa wakijiuliza mara mbili mbili maana unaweza kukuta amebakwa hata na babu wa miaka 70 mpaka 75.
Wapo wengine wanaobaka watoto hata wa miaka mitano, na hawa wanaonekana kabisa kuwa wana imani za kishirikina.
Wataalamu wetu wanatakiwa kufanya utafiti ili kugundua waganga hao huwaambia nini watu wao, na kama wakifanya hivyo watapata nini kiasi cha kujitia hamnazo na kufanya uhayawani?
Kifupi ni kwamba hakuna dawa yoyote inayoweza kupatikana kama hujajua mgonjwa anaumwa nini.
Ndiyo maana mgonjwa anapopelekwa hospitali hawezi kupewa tiba yoyote hata kama akikaa wiki nzima, badala yake wataalamu watadili kwanza na matokeo ya ugonjwa kama vile kutuliza maumivu na mengine, lakini ni mpaka kwanza wamfanyie uchunguzi na vipimo ndipo atakapoanza kupata dawa ya kutibu chanzo cha ugonjwa.
Haya yote yanayotokea yana chanzo chake. Hivi sasa mambo yameenda mbali zaidi tunaanza kuona mpaka watu wa dini ambao wanategemewa wao wakemee waumini, na wao wanafanya mambo hayo hayo wanayokataza.
Jeshi la Polisi linafanya kazi yake nzuri tu ya kutuhabarisha pamoja na kukamata wahusika. Kwa namna ya pekee niwape pongezi kwani sijasikia hata ripoti moja ya aina hiyo ikisema mtuhumiwa amekimbia bila kukamatwa, labda awe amejiua.
Hata hivyo, kukamatwa watuhumiwa ni kama kutibu matokeo ya ugonjwa, lakini unahitajika uchunguzi wa kina kutoka kwa wataalamu waliobobea kama vile Ustawi wa Jamii, Madaktari, Vyakula na Lishe, uchumi na hata watu wa saikolojia ili watuambie ni kitu gani kimetokea sasa kumekuwa na mmomonyoka mkubwa wa maadili, ukatili, mauji na mambo mengine ya kushangaza ambayo miaka ya nyuma yalikuwa yanatokea kwa nadra sana.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







