Wakulima changamkieni fursa ya CPB

18Oct 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wakulima changamkieni fursa ya CPB

NI habari njema kwa wakulima baada ya Bodi ya Mazao Mchanganyiko nchini (CPB) kufungua milango kwa ajili ya kununua mazao mbalimbali ya wakulima yakiwamo ya chakula.

Habari hiyo njema ilitangazwa na bodi hiyo ikiwa na  lengo la kusaidia kuondoa tatizo la ukosefu wa masoko linalowakabili wakulima wengi hapa nchini.

Tatizo la wakulima kukosa masoko ya mazao yao ni kubwa. Wanatumia nguvu nyingi kutayarisha mashamba hadi wakati wa mavuno, lakini ukija upande wa soko wanasumbuka na wengine mazao yao kuharibika au kuuzwa kwa bei ya hasara.

Bodi hiyo sasa imesema imekuja na mkakati wa kununua mazao hayo na wao kuyaongezea thamani ili yaweze kuuzika ndani na nje ya nchi.

Wakulima wengi nchi wamekosa elimu ya kuyaongezea mazao yao thamani na matokeo yake yanapokosa soko mapema huishia kuharibika.

Kwa wanaosafiri kwenda mikoa mbalimbali, barabarani wanashuhudia inapokuwa msimu wa matunda kama machungwa, maembe na mananasi, wakulima wanapata hasara wanapokosa wateja wa uhakika na kubaki kuoza na kuwa chakula cha wanyama.

Hali hiyo hutokea pia kwa mazao mengine yanayoharibika haraka kama nyanya. Wakulima wengine kwa kuona uchungu wa kupoteza mazao hayo, huwaomba wateja kuchukua hata kwa mkopo ili mradi tu aone mazao yake yamechukuliwa na mtu badala ya kutupa.

Kama kungekuwa na viwanda vya kutosha vya usindikaji, mazao hayo yangeweza kuongezewa thamani kwa kusindikwa na kufungashwa vizuri kwa kupata soko la ndani na nje kwa kipindi cha muda mrefu.

Taarifa ya Bodi hiyo kununua mazao kwa wakulima itawaletea faraja kwa kuwa imesema bei wanayonunulia mazao hayo ni ile inayotumika sokoni.

Bodi hiyo imegundua imefungua milango ya kununua mazao hayo ya wakulima baada ya kuona wengi wanalalamika kukosa soko baada ya kuvuna, na hata lile linalopatikana ni la kulanguliwa kwa bei ya hasara na wafanyabiashara wakubwa.

 

Katika kuwasaidia wakulima ili wapate motisha ya kuendelea kulima mazao hususani ya biashara bila kukata tamaa wameona wasaidie kununua mazao yao baada ya kushuhudia wengine wakiishia njiani.

Baadhi ya mazao wanayonunua wateja kuwa ni mpunga, mahindi, maharagwe na ya jamii ya kunde na yanayotumika kwa ajili ya chakula na lishe.

Vigezo wanavyovitumia katika kununua mazao hayo ni pamoja na kuhakikisha hayana uchafu. Mfano kama ni mchele ni lazima uwe hauna uchafu kama wa mawe.

Pia, bodi hiyo imefungua matawi ya kuuza mazao hayo katika nchi zote za Afrika Mashariki na kuwataka wakulima kuendelea kulima mazao ya biashara.

Lengo lao ni kuhakikisha mkulima ananufaika, anapatiwa fedha ambayo inalingana na bei ya sokoni. Lengo ni kuondoa tatizo la wakulima kufanyiwa udalali na wafanyabiashara wakubwa wasio waaminifu ambao hupendelea kuwaonea ili wao ndiyo wapate faida zaidi.

Fursa hii iliyotolewa kwa wakulima itumike vizuri na kama ilivyoelezwa, mazao hayo yanapopelekwa kuuzwa yawe katika ubora unaotakiwa.

Fursa isitumike kuharibiwa wengine kwa kujaza uchafu ili kuongeza kilo kwenye vipimo.