Baadhi ya wananchi wanaohitaji huduma hiyo, wamekuwa wakilalamikia kutuma maombi yao ikiwa ni pamoja na kujaza fomu kama inavyotakiwa pamoja na michoro ya umeme kwenye nyumba mpya kuwa na muhuri wa mkandarasi aliyesajiliwa lakini inachukua muda mrefu kupata huduma hiyo ambayo ni muhimu kwa maisha ya kila siku.
Wananchi hao wanaohitaji huduma hiyo wamekuwa wakipigwa ahadi ya njoo kesho kila wanapofuatilia huduma na wakati mwingine wanapoambiwa ofisa fulani ndiye amepewa jukumu husika, basi naye hujifanya mungu mtu kwa kumzungusha mteja. Kwa kifupi, baadhi ya maofisa hasa mafundi, wanawazungusha wateja.
Mfano mmojawapo kuhusu malalamiko hayo ni wananchi wa Mtaa wa Iyela One katika Jiji la Mbeya, ambao wamedai kuwa shirika hilo limeshindwa kuwasambazia umeme licha ya kuomba huduma hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu.
Kutokana na kushindwa kupatiwa huduma hiyo, wananchi hao wamesema wanalazimika kusafiri kwenda kupata huduma zinazohitaji nishati hiyo kwenye mitaa mingine ya jirani. Kutokana na adha hiyo, wananchi wamesema wanashindwa kufanya shughuli mbalimbali zikiwamo za kuwaingizia kipato, jambo ambalo linakwenda kinyume cha ahadi za serikali katika kuwapatia wananchi nishati ya umeme.
Kwa mujibu wa wananchi hao, waliwasilisha maombi TANESCO tangu mwaka 2019 lakini mpaka sasa hawajapata huduma hiyo huku wakipigwa danadana na maofisa wa shirika hilo kila wanapofuatilia. Wamedai kuwa kila wanapofutilia kujua nini kinachoendelea, jibu ambalo wamekuwa wakipewa ni kuwa na subira.
Pia wamedai kuwa pamoja na kujaza fomu na kutimiza masharti yote, hakuna hata ofisa wala fundi wa TANESCO aliyethubutu kufika katika eneo hilo na pia hakuna hata nguzo iliyowekwa eneo hilo. Maofisa hao walichofanya ni kupima na mchezo uliishia hapo.
Kutokana na malalamiko hayo, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Elisha Kilimbo, alisema wanalitambua suala hilo lakini akajitetea kuwa kinachokwamisha kupeleka huduma hiyo kwa wananchi ni ufinyu wa bajeti. Jambo la kujiuliza ni je, miaka mitatu katika bajeti wala kuna mpango wa kufikisha huduma hiyo katika eneo lililoko ndani ya jiji?
Majibu kama hayo yamekuwapo kwa muda mrefu kwani hata katika mkoa wa Dar es Salaam tatizo hilo lipo na wateja wengi wanapigwa danadana kila uchao. Uhalisia wa danadana za maofisa wa TANESCO ni katika ofisi zao maeneo mbalimbali ambako kila siku wananchi wanafika na kupewa ahadi za nenda rudi.
Mteja mmoja kwa mfano, aliwasilisha taarifa za waya wa umeme kupita juu ya kiwanja chake tangu Agosti, mwaka jana, na kila anapofuatilia wanamjibu kwamba wako katika mipango ya utekelezaji! Mipango hiyo ya kuhamisha waya tu inachukua muda gani?
Kwa ujumla, uongozi wa TANESCO unapaswa kubadili mwenendo wa utekelezaji wa majukumu yake hasa kuwafikishia huduma wananchi pamoja na kushughulikia kero zinazowasilishwa katika ofisi zao. Wanapaswa kuachana na ahadi za kisiasa kwa kuwa wananchi wanachohitaji ni huduma na si maneno.