Wauguzi hao ni wa Hospitali ya Mkomaindo, wilayani Masasi mkoani Mtwara.
Hatua iliyofikiwa na baraza hilo imetoka na maelezo yaliyotolewa na ndugu wa mjamzito aliyefariki na baraza hilo kuridhishwa na ushahidi huo.
Wauguzi waliofutiwa leseni zao ni Elizabeth Njenga na Pascal Mnyalu ambao walishtakiwa kwenye baraza hilo pamoja na wauguzi wengine watatu na madaktari wawili, wote wa hospitali hiyo kuhusika na uzembe uliopoteza maisha ya mjamzito Aisha Romanus.
Wauguzi wengine Joyce Nkane na Tumaini Milanzi walipewa onyo kali na mwingine Lucia Liababa, alifutiwa shtaka lake baada ya kuonekana kutohusika moja kwa moja na uzembe huo.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Lilian Msele, aliwatia hatiani madaktari wawili wa hospitali hiyo, Amina Mushi na Hashimu Chiwaya, ambao taarifa zao zitapelekwa kwenye Baraza la Madaktari ili hatua stahiki zichukuliwe.
Adhabu waliopewa wauguzi hao iwe fundisho kwa wengine wenye tabia ya kupuuza wagonjwa wanapokuwa na uhitaji hasa kwenye jambo la dharura.
Kilio cha wagonjwa wengi, hasa wajawazito ni unyanyasaji au kupuuzwa wanapokuwa kwenye hali ya uchungu na kujibiwa lugha zisizostahili au kuachwa wakihangaika wenyewe mpaka wengine kufikia hatua ya watoto kutoa bila kupata msaada wa muuguzi.
Katika hukumu iliyotolewa na baraza hilo, ilielezwa kuwa dada wa marehemu Agnes John, alilieleza Baraza kuwa Novemba mosi, mwaka jana, mdogo wake Aisha, alishikwa na uchungu wa uzazi na kuamua kumfikisha zahanati ya Lukuledi na muuguzi wa zahanati hiyo baada ya kumpima aliwaeleza waende Hospitali ya Wilaya ya Mkomaindo.
Hata hivyo alipopiga simu hospitali hiyo ya wilaya wauguzi walimjibu hawakuwa na mafuta ya kutumia kwenye gari la wagonjwa na kulazimika kukodi bajaji ambayo pia iliharibika njiani na baada ya matengenezo walifika saa moja usiku Hospitali ya Mkomaindo.
Agnes alisema baada ya kupokewa mgonjwa wake hakupata huduma haraka na kuambiwa aondoke jambo alilolipinga na muda mfupi alimuona mdogo wake akiomba msaada kwa wauguzi hao, lakini hawakumjali na ilipofika usiku wa saa tano akaaga dunia.
Wajumbe wa baraza hilo ambao waliwahoji madaktari na wauguzi hao walishangazwa na maelezo ya wauguzi hao kuwa tofauti kiasi cha mjumbe mmoja wa baraza kukerwa kutokana na maelezo waliyoyawasilisha awali baada ya kutakiwa kuandika taarifa kutofautiana na waliyokuwa wakiyatoa.
Baraza hilo liliamua wauguzi hao kutotakiwa kufanya shughuli zozote za kiuguzi kutokana na kukiuka kanuni na viapo vyao walivyokula, pia ililaumu uongozi wa hospitali hiyo kutokuwa na ufuatiliaji wa watumishi wake ambao kama ungekuwa mzuri maafa kama hayo yasingeweza kutokea.
Msajili wa Baraza hilo, aliwataka wananchi kufikisha malalamiko yao waonapo hawatendewi haki na wauguzi na madaktari ili wachukue hatua stahiki huku akibainisha kuanza kusikiliza kesi nyingine.