Serikali inapaswa kufanyia kazi ushauri kuhusu miradi

21Oct 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Serikali inapaswa kufanyia kazi ushauri kuhusu miradi

WATAALAMU wa masuala ya ubunifu majengo na wakadiriaji majenzi, juzi walifanya mkutano wao wa tatu jijini Dar es Salaam ili kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazowakabili pamoja na kuzitafutia ufumbuzi.

Pamoja na mambo mengine, wataalamu hao kupitia Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Dk. Ludogija Bulamile, walianika suala la kukithiri kwa viwango duni katika miradi ikiwamo ile ya serikali.

Bila kuuma maneno, Dk. Ludogoja alisema chanzo cha tatizo hilo ni kutokushirikishwa wataalamu wa fani husika wakiwamo wahandisi, wabunifu majengo na wakadiriaji wa gharama za ujenzi.

Licha ya kuanika tatizo hilo, Dk. Ludigija kwa niaba ya wataalamu hao, alitoa ufumbuzi wa suala hilo ikiwamo kushirikishwa kwa wataalamu wa fani mbalimbali kwenye miradi inayohitaji umakini ili idumu na kutumika kwa muda mrefu. Miongoni mwa miradi ambayo aliitaja kuwa inapaswa kuwapo wataalamu wa fani husika ni pamoja na ujenzi uwe wa barabara, majengo, usambazaji wa maji na upanuzi wa bandari.

Ni ukweli usiopingika kwamba miradi mingi imekuwa ikitekelezwa kwa kiwango duni na matokeo yake kuharibika baada ya muda mfupi na mingine kama ya maji kushindwa kutumika kabisa kwa kushindwa kutoa maji.

Kwa muda mrefu imeshuhudiwa viongozi wakiwa katika ziara za kikazi mikoani au wakati wa mbio za mwenge kukiwa na taarifa za miradi kutekelezwa kwa viwango vya chini na hata viongozi kama vile wa msafara wa mwenge wakikataa kuizindua au kuipokea kwa sababu hizo.

Mbali na miradi hiyo, mara kwa mara imekuwa ikielezwa kuwa baadhi ya majengo katika miji mikubwa,  Dar es Salaam ikiwamo, yamejengwa kwa kulipuliwa au kutokukidhi viwango na ubora unaotakiwa. Yako majengo ambayo yaliwahi kuanguka kwa sababu ya vifaa vilivyotumika kutokuwa na uwiano wa majengo husika.

Wiki hii kwa mfano, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wiki hii alifanya ziara wilayani Namtumbo, Ruvuma na kukagua ujenzi wa hospitali ya wilaya na kuibua madudu ikiwamo milango iliyofungwa kutokuwa na ubora. Mtu aliyeulizwa kuhusu ujenzi huo ni mganga mkuu wa wilaya ambaye hahusiani kabisa na hana taaluma yoyote kuhusu ujenzi.

Kinachoonekana hapo ni kwamba aliyepewa fedha kwa ajili ya ujenzi huo ni mganga mkuu ambaye kitaaluma ni daktari kwa hiyo hata angedanganywa kuhusu vifaa vinavyotakiwa angekubali kwa sababu hana uelewa wowote kuhusu ujenzi. Laiti  wangeshirikishwa wahandisi katika mchakato mzima, ni dhahiri kwamba kusingekuwa na kasoro nyingi kama zilizoibuliwa na Waziri Mkuu.

Madudu katika hospitali ya Namtumbo ni mfano mmoja tu lakini kuna miradi mingi ya maji na barabara ambayo imekuwa ikijengwa kwa viwango duni na matokeo yake kuharibika baada ya muda mfupi. Kwa mfano, ziko barabara nyingi katika mkoa wa Dar es Salaam ambazo zimejengwa na kuharibika baada ya muda mfupi na kuwapo kazi za kuziba viraka kila uchao.

Kama ilivyoshauri AQRB, ni vyema serikali ikasikiliza ushauri na kuufanyia kazi hasa kuwapo kwa wataalamu wa fani husika ambazo zinahusiana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kama ni barabara, ni vyema wakawapo wahandisi, wabunifu na watu wa afya na usalama kazini badala ya kumwachia mkandarasi akaendelea na ujenzi bila kuangalia kama vigezo na masharti katika mradi vimezingatiwa.

Serikali inatumia mabilioni ya shilingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo hakuna budi kuhakikisha kuna usimamizi wa kutosha pamoja na thamani ya fedha katika kazi husika badala ya kulipuliwa na kutokudumu.