Serengeti Girls imeiheshimisha nchi, TFF mulikeni vipaji zaidi

24Oct 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Serengeti Girls imeiheshimisha nchi, TFF mulikeni vipaji zaidi

TIMU ya Taifa ya Wanawake wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Girls), imeaga Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini India baada ya kuishia hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Serengeti Girls ambayo tofauti na ilivyotarajiwa ilionyesha kiwango cha kuvutia katlka fainali hizo zilizoshirikisha mataifa 16, imeishia hatua hiyo baada ya kutolewa na Colombia kwa mabao 3-0 juzi hivyo kuwashuhudia wapinzani wao hao wakiungana na Nigeria, Ujerumani pamoja na Hispania hatua ya nusu fainali itakayopigwa keshokutwa, Jumatano.

Kabla ya kipigo hicho dhidi ya Colombia, Serengeti Girls ambayo ilikuwa Kundi D, ilipoteza mechi moja tu dhidi ya Japan kwa mabao 4-0, kisha ikashinda 2-1 dhidi ya Ufaransa na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Canada.

Matokeo hayo yaliifanya Serengeti Girls kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi D, nyuma ya bingwa mtetezi Japan, ambaye alishinda mechi zote tatu kabla ya kukutana na kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Hispania hatua ya robo fainali.

Kwa ujumla hatuna tunachopaswa kuidai Serengeti Girls ambayo ilishiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza katika historia yake, lakini ikiungana na timu ya Taifa ya Watu wenye Ulemavu (Tembo Warriors), kuwa timu pekee kutoka Tanzania zilizofanikiwa kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mpira wa miguu.

Ikumbukwe Tembo Warriors nayo imetoka kushiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu kwa Watu wenye Ulemavu nchini Uturuki na kuishia hatua ya robo fainali, jambo ambalo ni mwanzo mzuri kwa timu hizo za Tanzania.

Kwa mantiki hiyo, japo tulitamani kuona Serengeti Girls ikifika mbali zaidi na hata kutwaa ubingwa huo, kwa ilipoishia tuna kila sababu ya kuipongeza kwani tunatambua haikuwa michuano rahisi hata kidogo.

Tunaamini hivyo hasa tukizingatia timu Serengeti Girls ilizokutana nazo katika fainali hizo, ni nchi ambazo zinautaratibu mzuri wa kulea vipaji katika akademi maalum za soka tangu wakiwa wadogo zaidi ya umri huo, tofauti na Tanzania, ambapo ni vigumu kujua wachezaji hao walitokea wapi kisoka hapo kabla.

Ni wazi vipaji vya wachezaji wa Serengeti Girls vimeonekana wakiwa na umri huo ama wakiwa na miaka 14, hivyo kwa uwezo walionyesha, upambanaji mwanzo mwisho na hatua waliyofikia, tuna kila sababu ya kusema kongole kwao kwa kazi kubwa waliyofanya.

Lakini pamoja na kongole zetu hizo, tuna kila sababu pia kulitaka Shirikisho la Soka nchini (TFF), kuhakikisha inavilinda vipaji vya watoto hawa kwa kuviendeleza visipotee ili baadaye kuwa msaada mkubwa kwa timu ya Taifa ya U-20, U-23  na hatimaye ya wakubwa, Twiga Stars.

Tunachotamani kwa wachezaji hao ni kuendelea kuwaona wakiwika zaidi katika michuano ijayo ya U-20 na U-23 kwa kiwango cha juu na hilo litawezekana tu kama TFF itakuwa na utaratibu mzuri wa kuwaita mara kwa mara na kuwaandalia mechi mbalimbali za kirafiki ili kuendelea kuwa na muunganiko mzuri.

Tunaamini kwa kiwango walichoonyesha wapo watakaopata timu kubwa Afrika na nje ya bara hili, hivyo kwa kulitambua hilo ni wakati sasa kwa TFF kuelekeza nguvu zaidi katika soka la wanawake kwa kuwa wameonyesha wanaweza zaidi katika mchezo huo pendwa duniani.

Aidha, ni wakati sasa kwa wadhamini kujitokeza zaidi kuzidhamini klabu za soka za wanawake pamoja na Ligi Kuu na ile ya Daraja la Kwanza, ili kuongeza hamasa na ushindani zaidi jambo litakalochochea kukua na kuongezeka kwa vipaji katika soka la wanawake.