Ushindi huo wa Serengeti Girls umekuja baada ya kupoteza kwa mabao 4-0 dhidi ya mabingwa watetezi wa kombe hilo, Japan kwenye mchezo wao wa ufunguzi Jumatano iliyopita.
Kwa matokeo hayo sasa Serengeti Girls inahitaji kushinda mechi yao ya mwisho kesho dhidi ya Canada ili kujihakikishia nafasi ya kutinga robo fainali kutoka Kundi lao la D linaloongozwa na Japan ambayo yenye ponti sita ikifuatiwa na Tanzania yenye alama tatu huku Ufaransa na Wacanada hao kila moja ikiwa na pointi moja.
Kwa kiwango kilichoonyeshwa na Serengeti Girls juzi hadi kuifanya Ufaransa kupata bao lao pekee kwa mkwaju wa penalti, tunaamini kama ikikaza na kujituma vilivyo dhidi ya Canada, robo fainali inawezekana kabisa jambo ambalo itakuwa imeandika rekodi nyingine baada ya hiyo ya kushiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo.
Kama imeweza kuifunga Ufaransa ambayo mchezo wa kwanza ilitoka sare na Canada, tunaamini endapo benchi la ufundi litalofanyia kazi mapungufu machache yaliyojitokeza mechi mbili zilizopita, ushindi unawezekana bila tatizo.
Sisi tunaamini kikubwa kilichoisumbua Serengeti Girls katika mchezo wa kwanza ni homa tu ya kuanza michuano hiyo mikubwa duniani kwa umri wao, ambayo sasa imeshatoweka na kilichobaki ni kuonyesha tu uwezo wao ili kushinda mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi.
Aidha, kwa Kocha Mkuu wa Serengeti Girls, anapaswa kufanyia kazi zaidi safu yake ya ulinzi na kuitaka kuwa makini zaidi na ili kuepuka kufanya madhambi ndani ya eneo la hatari kama ambavyo imewagharimu katika michezo miwili iliyopita dhidi ya Japan na Ufaransa.
Hii ni kutokana na michezo yote miwili kusababisha penalti ambazo zimewanufaisha wapinzani wao Japan na Ufaransa kwa kupata bao, jambo ambalo linaweza kuwagharimu zaidi mechi ijayo kama lisipofanyiwa kazi kwa umakini zaidi.
Lakini hii ni fursa kwa wachezaji wa Serengeti Girls kuonyesha wanaweza kwa kila mmoja kupambana hadi tone la mwisho kwani si tu kwamba ushindi wao ni fahari kwa Tanzania, bali fainali hizo zinaweza kuwa mwanzo wa wao kutoka kimaisha endapo wataendelea kufanya vizuri zaidi.
Tunatambua uwapo wa mawakala wengi katika michuano hiyo, ambayo kwa Afrika ina wakilishwa na mataifa matatu; Morocco, Nigeria na Tanzania na timu hizo kila moja ikiwa imevuna pointi 3 katika michezo miwili ya awali.
Hivyo, kwa wachezaji ambao wataonyesha uwezo wa juu wanaweza kununuliwa na klabu kubwa Ulaya kwenda kucheza soka la kulipwa na kujipatia maslahi makubwa zaidi na kuinua maisha yao kwa ujumla.
Kwa mantiki hiyo, wachezaji wa Serengeti Girls, huu ni wakati wa kupambana na kuiwezesha Tanzania kufika robo fainali, nusu na hatimaye fainali, kwani kadri wanavyosonga mbele kwa kufanya vizuri kwenye michuano hiyo ndivyo wanavyotanua wigo wa kujitangaza zaidi na uwezo wao kuonekana.
Sisi tukiwa kama wadau namba moja wa michezo nchini tunaungana na Watanzania wote kwa ujumla kuwaombea na kuwatakia kila la kheri katika maandalizi yao ya mchezo wa kesho dhidi ya Canada ili kupata ushindi na kuitangaza vema Tanzania kwani tunachokitaka si tu kuona wakifika robo fainali, bali nusu, fainali na kisha kutwaa ubingwa huo.