Ikiwa ni miaka 23 imepita tangu kiongozi huyo mwasisi aliyejitolea maisha yake kwa ajili ya kupigania uhuru wa Watanzania na maendeleo yao kijamii na kiuchumi, kuna mambo mengi ambayo bado ni ya kujifunza na ya kujivunia.
Nyerere ambaye aliiongoza nchi kwa miaka 24, atabaki kuwa Rais pekee aliyekaa madarakani muda mrefu kuliko waliomfuatia na watakaoshika nafasi hiyo kwa kizazi cha sasa na kijacho. Hiyo inatokana na ukweli kwamba baada ya kumaliza muda wake na kutokana na kuanza kwa mfumo wa demokrasia, alipendekeza Rais akae madarakani kwa miaka 10 kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano ikibidi.
Wakati leo Watanzania wanaadhimisha kilele cha kumbukumbu ya kifo chake kukiwa kumetanguliwa na mihadhara na warsha, yako mambo mengi ambayo kutokana na aliyoyafanya au kuyasema bado yanakumbukwa na yatabaki katika historia ya nchi kwa vizazi vingi vijavyo.
Licha ya kuleta uhuru na baadaye Tanganyika na Zanzibar kuungana na kuzaliwa taifa la Tanzania, jambo kubwa na la msingi ambalo ni la kukumbukwa ni uthubutu alioufanya wa kuitisha Halmashauri Kuu ya TANU na kutangaza Azimio la Arusha ambalo lilitoa dira na mwelekeo wa uchumi na siasa za Tanzania. Ni azimio ambalo lilileta usawa miongoni mwa Watanzania na kuondoa ubaguzi na unyonyaji.
Kadhalika, Nyerere alipigania hali bora za maisha ya Watanzania huku akisisitiza watu kufanya kazi ili kujiletea maendeleo. Alisisitiza uzalishaji mashambani na viwandani sambamba na elimu kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania kujikomboa kifikra, kuyatawala mazingira na kutoa mchango katika jamii zinazowazunguka kwa kutatua changamoto zilizopo.
Mwalimu pia hakuwa na msalie mtume dhidi ya rushwa. Alikemea waziwazi na kuwafukuza waliokuwa wasaidizi wake waliobainika kujihusisha na vitendo hivyo pamoja na kufungwa jela na viboko juu.
Nyerere alitamka wazi kwamba rushwa ni adui wa haki na hata ikawekwa ndani ya ahadi za mwanachama wa TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wakati huo huo akisema maudhui hayo yakitanguliwa na maadui wakuu watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.
Ili kupambana na maadui hao, Nyerere alisimamia kikamilifu katika ujenzi wa shule na vyuo ili watanzania kuondokana na ujinga pamoja na kuanzisha elimu ya watu wazima. Pia aliongoza kwa vitendo ufanyaji kazi kwa bidii kwa ajili ya kuondokana na umaskini.
Kwa upande wa maradhi, vituo vya kutolea huduma za afya vilianzishwa vikiwamo vya taasisi binafsi na mashirika ya dini. Hayo ni mambo machache ambayo ni mifano hai na inayoishi kuhusu maisha ya Nyerere kwa aliyofanya kwa ajili ya Watanzania.
Kwa mantiki hiyo, wakati leo ni kumbukumbu ya miaka 23 ya kifo chake, ni vyema Watanzania wakamuenzi kwa vitendo kwa kuunga mkono mambo aliyoyafanya kwa ajili ya maendeleo sambamba na kupiga vita maadui rushwa, maradhi, ujinga na umaskini ambao bado wanaitafuna Tanzania.










