Ushirikiano Tanzania na Uganda kudhibiti ebola ni wa kupongeza

13Oct 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ushirikiano Tanzania na Uganda kudhibiti ebola ni wa kupongeza

JANA nchi za Tanzania na Uganda zimeingia makubaliano ya ushirikiano mipakani mkoani Kagera, kudhibiti ugonjwa wa ebola.

Ushirikiano huo una lengo la kuhakikisha kuwa ugonjwa wa ebola hauingii nchini Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa nchi hizo ni majirani na kuwa rahisi kupenya.

Makubaliano hayo yalifikiwa jana katika mpaka wa Bugango, Wilaya ya Misenyi mkoani humo, kati ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dk. Issessanda Kaniki na maofisa afya nchini Uganda.

Katika ushirikiano huo walikubaliana kufanya ukaguzi kwa wasafiri, kuwapima maambukizi ya ugonjwa wa ebola, kutoa cheti na kuweka vifaa vya kuzuia maambukizi vikiwamo vitakasa mikono, sabuni na maji tiririka.

Walikubaliana kuwa maofisa afya wote wa mipakani watoe elimu ya tahadhari na kuchukua hatua za pamoja kutoa huduma na kutatua matatizo yoyote yatakayojitokeza kwa pamoja.

Hatua hiyo iliyofikiwa na nchi hizo mbili ni ya kutia moyo kwa sababu bila ushirikiano katika kudhibiti ugonjwa huo utasambaa na kuathiri nchi nyingine za jirani.

Magonjwa ya milipuko yanapojitokeza na serikali kuchukua hatua haraka, zinasaidia kudhibiti maambukizi kuenea kwa kasi.

Tanzania na Uganda zina ukaribu ambao watu wake hasa mipakani huingia kwa njia mbalimbali zikiwamo za kibiashara na hata katika shughuli zingine.

Undugu wa nchi hizo umetokana na mambo mengi kwani hata watu huoana na kutengeneza familia ambazo huimarisha udugu huo.

Hata lugha baina ya nchi hizo mbili watu wake husikilizana, hivyo makubaliano ya ushirikiano huo katika kudhibiti ugonjwa huo utaleta manufaa makubwa na kuondoa hofu kwa wananchi wake.

 Imeelezwa katika makubaliano hayo kuwa ni ya ujirani mwema katika kudhibiti tishio la ugonjwa huo usiingie nchini kupitia mipaka yote mkoani Kagera, nchini Tanzania.

Na kwa upande wa Ofisa Afya kutoka nchini Uganda, Mlekateka Jesca, alisema ushirikiano huo utasaidia kuwaelimisha wananchi wa pande zote kujikinga na ugonjwa huo.

Viongozi wa nchi hizo mbili waliwahakikishia wananchi kuwa ugonjwa wa ebola haupo Wilaya ya Mubende na Kampala na ushirikiano huo utatusaidia kuendelea kuudhibiti ili usiingie wala kuvuka kwenda Tanzania.

Katika makubaliano hayo ambayo pia yalihudhuriwa na watendaji kutoka Mkoa wa Kagera, ambao waliweka bayana kuwa tangu wamepata taarifa ya tishio la ugonjwa huo wanashirikiana na maofisa afya kutoa elimu kwa jamii kuhusu kujikinga na ugonjwa huo.

Wataalamu wa afya kutoka Kituo cha Mbale kwa upande wa Uganda na viongozi mbalimbali wa kata na vijiji, kwa upande wa Tanzania pia walikuwapo katika makubaliano hayo kuonesha kuwa nguvu inayotumika kudhibiti ugonjwa huo ni kubwa na kuhakikisha hauvuki kuingia Tanzania ili wananchi waendelee kufanya shughuli za kuzalisha mali bila hofu.

Magonjwa ya milipuko ni hatari kwasababu yanarudisha nyuma shughuli za maendeleo kutokana na gharama kubwa kutumika yanapokuwa yameingia kwenye nchi yoyote bila kuchukuliwa tahadhari.