Yanga inayoiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, iliikaribisha Al Hilal ya Sudan katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na mechi kumalizika kwa sare ya bao 1-1, hivyo inahitaji ushindi ama sare yoyote ya kuanzia mabao mawili ili kutinga hatua ya makundi.
Kwa upande wa Azam FC, ikiwa ugenini nchini Libya, ilikumbana na kipigo kikubwa cha mabao 3-0 dhidi ya Al Akhdar kwenye mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo kuwa na mlima mrefu wa 'kupindua meza' katika mchezo wa marudiano mwishoni mwa wiki hii utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
Ushindi wa mabao 4-0 na kuendelea, ndio utakaoiwezesha Azam kusonga mbele kwenye michuano hiyo, wakati Kipanga FC ya Zanzibar iliyoikaribisha Club Africain ya Tunisia katika Uwanja wa Amaan visiwani humo, yenyewe ikilazimishwa sare tasa, hivyo ushindi wowote ama sare yoyote ya mabao itaiwezesha kusonga mbele kwenye hatua inayofuata ya kinyang'anyiro hicho.
Wawakilishi wengine kwenye michuano hiyo ya kimataifa kwa ngazi ya klabu ni Simba, ambayo jana jioni ilikuwa ugenini nchini Angola ikipepetana dhidi ya Primeiro de Agosto kwenye mechi ya Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kurudiana Jumapili wiki hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Hivyo, ingawa matokeo kwa Yanga, Azam na Kipanga hayakuwa rafiki sana, bado tunaamini hakuna kinachoshindikana katika mchezo wa soka na lolote linaweza kutokea kwa wawakilishi wetu hao kupata matokeo chanya zaidi na kusonga mbele.
Tunatambua mashabiki wengi hususan ni wa timu hizo na Watanzania kwa ujumla, wamekata tamaa wakiamini ni vigumu hususan kwa Yanga na Kipanga kwenda ugenini na kupata matokeo, lakini kwa Azam kuweza kupindua meza kwa kushinda zaidi ya mabao matatu katika mechi ya marudiano hapa nchini.
Lakini sisi tunaamini, kinachotakiwa ni maandalizi makubwa ndani ya wiki hii, kwa makocha kutazama wapi walifanya makosa dakika 90 za kwanza na kuyatafutia ufumbuzi lakini wakitumia muda vizuri kwa kuwajenga wachezaji kisaikolojia kwa kuwaaminisha inawezekana kupata matokeo ugenini na hata kwa Azam kushinda nyumbani kwa idadi kubwa ya mabao.
Kikubwa kinachotakiwa ni kuwaonya wachezaji kutobeba kile kinachojadiliwa na mashabiki kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari, ambavyo vinawakatisha tamaa wakiamini kwamba tayari timu zao zimeshatolewa.
Nipashe tunatambua mpira wa miguu una matokeo matatu ambayo yanaweza kupatikana popote iwe uwanja wa nyumbani ama ugenini ambayo ni kushinda, kushindwa na sare, lakini ni mchezo wa makosa na anayekosea huadhibiwa.
Kwa mantiki hiyo, kama Al Hilal iliweza kupata sare Uwanja wa Benjamin Mkapa, hata Yanga ikijipanga na kuweka kando kelele na vifijo vya mashabiki wa wapinzani wao ugenini, inawezekana kabisa kupata matokeo na kutinga hatua ya makundi.
Lakini, kwa Azam FC, hilo linawezekana kwani itakuwa nyumbani dhidi ya Al Akhdar na yenyewe ikifaidika na mashabiki wake na uzoefu wao mkubwa katika uwanja wake wa Azam Complex ukiwabeba, hali kadhalika kwa Kipanga ambayo ililazimishwa sare tasa dhidi ya Club Africain, kwani itakuwa na faida zaidi endapo ikijitahidi kupata bao la ugenini kwa kuwa sare yoyote itaifanya kusonga mbele na kusubiri kupangiwa timu moja kutoka zitakazotolewa kwenye raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ili kucheza mechi ya mtoano kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Hivyo, tunazitakia maandalizi mema Yanga, Azam na Kipanga lakini Simba ambayo hadi tunakwenda mitamboni hatukuwa na matokeo yao.
%%%%%%









