Ujio wa Rais Ruto nchini udumishe udugu

11Oct 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ujio wa Rais Ruto nchini udumishe udugu

RAIS wa Kenya, Dk. William Ruto, amefanya ziara yake nchini Tanzania ikiwa ni taifa la kwanza kwa Afrika Mashariki kulitembelea tangu alipoapishwa rasmi Septemba 13.

Kwetu sisi ni heshima kubwa kuteuliwa kuwa nchi ya kwanza kwa Rais huyo wa awamu ya tano nchini Kenya kuja Tanzania tukiamini kuwa anatuamini na kutuweka kwenye orodha ya ndugu, majirani na washirika muhimu tunaotegemeana.

Rais Ruto alitangazwa kuwa mshindi wa kiti hicho katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga, ambaye baada ya kutangazwa kwa matokeo aliyapinga mahakamani na kuomba yarudiwe kuhesabiwa, lakini ushindi ukabaki kwa Ruto.

Nchi hizi mbili zimekuwa na ushirikiano mkubwa hasa kwa raia wake ambao pamoja na kuwa marafiki, lakini kuwa na fursa ya kufanyakazi.

Kenya ni kaka mkubwa katika ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na mdau mkuu wa kibiashara na Tanzania ambaye amewekeza vitega uchumi vingi nchini na kuwezesha upatikanaji wa bidhaa muhimu kuendelea kuwapo.

Mshirika huyu mkuu kibiashara ana nafasi ya kipekee kwani kuzungumza Kiswahili kunaongeza ujirani baina ya raia wetu na hili ni jambo lingine linalozifanya nchi hizi kuwa na ushirikiano wa kitamaduni na hata maingiliano ya kiutamaduni.

Kwa msisitizo ushirikiano wa kibiashara pia umekuwa mkubwa kutokana na bidhaa zinazotengenezwa kutoka nchi hizo mbili kuuzwa bila tatizo na wafanyabiashara wakifurahia uwekezaji na uzalishaji.

Ukitembelea maduka mengi ya Tanzania lazima utakutana na bidhaa za Kenya na vivyo hivyo kwa upande wa Kenya, bidhaa za Tanzania hasa kwa upande wa vyakula vya nafaka vina soko na vinakubalika.

Matumizi ya lugha ya Kiswahili, kinachozungumzwa na nchi nyingi za Afrika na pia kupitishwa kuwa lugha rasmi kwa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuzipa Tanzania na Kenya jukumu la pamoja na kuiendeleza lugha hiyo kimkakati.

Rais Samia Suluhu Hassan, alipokwenda nchini Kenya kushuhudia uapisho wa Rais Ruto, alibatizwa jina la Shangazi wa Afrika Mashariki, ni kielelezo kuwa anapewa heshima kubwa na marais wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kwa kuwa ndiye mwanamke pekee rais katika nchi hizo, ambaye pamoja na jukumu la kuongoza pia anasimamia uwapo wa biashara huru na yenye tija katika ukanda huu.

Rais Ruto kuiteua Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuizuru Afrika Mashariki, inaweza kuwa ni sababu ya heshima anayompa Rais Samia na kuonyesha nia yake ya kujenga ushirikiano imara kati ya nchi hizo mbili majirani na marafiki.

Katika mazungumzo yao, marais hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana kuondoa vikwazo ambavyo vinakwamisha biashara kati ya mataifa hayo mawili kusonga mbele.

Vile vile, suala la usalama katika mipaka ya majirani hao limepewa kipaumbele kuwa ni jambo muhimu katika kuzifanya nchi hizo zisonge mbele kimaendeleo na kudumisha amani na ushirikiano.

Tunaoumbea udugu na umoja kati ya mataifa haya udumu kwa kuwa bila Tanzania, Kenya haiwezi kuwa mshirika mkuu kibiashara na kiuchumi kadhalika bila Kenya, Tanzania haiwezi kujivunia mafanikio.