Timu ya kwanza kupata tiketi hiyo ilikuwa ni ya walemavu inayojulikana zaidi kwa jina la Tembo Warriors na kufuatiwa na Kikosi cha Wasichana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Girls).
Katika kujiandaa na fainali hizo za dunia, Tembo Warriors ilianza kuhudiwa na serikali katika kambi ya hapa nchini na baadaye ikapelekwa mapema Uturuki ili kuendelea kujifua, lakini kupata nafasi ya kucheza michezo ya kimataifa ya kirafiki.
Ikiwa huko iliweza kufanya vyema katika mechi zake za majaribio na baadaye ikaingia rasmi kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Ikishiriki kwa mara ya kwanza, Tembo Warriors imefika hadi hatua ya robo fainali, lakini ikashindwa kufurukuta mbele ya wenzao kutoka Haiti kwa kuchapwa mabao 4-1.
Pamoja na kupoteza mchezo huo, Tembo Warriors ilionyesha kiwango kizuri katika mechi hiyo na zile za hatua ya makundi kama vile inaundwa na wachezaji wenye uzoefu na michuano hiyo ya kimataifa kwa kuwavutia mashabiki na wadau mbalimbali waliokuwa wakiifuatilia timu hiyo.
Tunapenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza Tembo Warriors kwa mafanikio ambayo wameyapata katika mashindano hayo na kuondolewa kwenye fainali za mwaka huu, iwe ni mwanzo wa maandalizi ya kukata tiketi ya kushiriki fainali zijazo.
Ni wazi timu hiyo iliundwa na wachezaji waliokusanywa kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini, lakini umefika wakati viongozi wa chama (TAFF), ambacho kinasimamia mchezo huo kuanzisha ligi za wilaya, mikoa na baadaye Kanda ili kusaka vipaji vipya.
Kwa kuanzisha ligi za wilaya, mikoa na baadaye mashindano ya ngazi ya Taifa, kutasaidia kuzalisha wachezaji wengine ambao wataongeza nguvu katika kikosi cha Tembo Warriors, lakini itatoa nafasi kwa nyota waliopo kujiimarisha na kuwa tayari kupambana kwenye ngazi ya Afrika.
Ili mchezo huo uendelee, ni wakati sahihi kwa TAFF kushirikiana kwa karibu na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kuhakikisha mchezo huo unachezwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Ni wazi kwa kufanya hivyo, Tembo Warriors itaendelea kupata nafasi ya kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa na isionekane mwaka huu imefuzu kwa kubahatisha.
Timu au wachezaji walioandaliwa kuanzia ngazi za awali, huzaa matunda mazuri kutokana na misingi ambayo wanakuwa wamejengewa na hivyo, isionekane kama kwa kufanya mchakato huo, ni kuwaondoa wachezaji walioko sasa, bali ni mwendelezo wa kutaka kuiona Tembo Warriors ikipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika kila michuano ya kimataifa.
Mbali na serikali, huu ni wakati wa makampuni, taasisi na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kujitokeza kuwekeza katika timu hiyo ambayo sasa inahitaji kuajiri wakufunzi na makocha wenye vigezo vya juu kwa lengo la kuwaimarisha wachezaji na kuwafanya wawe tayari kushindana.
Kama ambavyo, Tembo Warriors imefanya, tunaamini pia Serengeti Girls, ambayo imetoka Uingereza kuweka kambi na sasa inaelekea India katika Fainali za Kombe la Dunia, itapeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Maandalizi ya timu zote mbili kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa kiasi kikubwa yamesimamiwa na serikali, kuendelea kujituma kutawafanya wadau wajitokeze kudhamini michezo yao ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuwapa ajira wachezaji, makocha, madaktari na maofisa wengine wanaosimamia shughuli za kila siku za timu hizo.
Wachezaji huu ni wakati wenu wa kuendelea kupambana na kumpa heshima, Rais, Samia Suluhu Hassan, ambaye anataka kuona Tanzania inafanya vyema katika michezo na mashindano yote.