Kuongezwa mabasi ya DART kulete ufanisi wa usafiri

05Oct 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kuongezwa mabasi ya DART kulete ufanisi wa usafiri

MAHITAJI ya usafiri wa umma katika miji yoyote hasa ya kibiashara lazima yatakuwa makubwa kutokana na shughuli zinazofanyika kila siku, iwe kibiashara, kiofisi na kijamii.

Kutokana na mahitaji hayo, ndiyo maana wadau wa sekta ya usafiri nchini wakaona fursa ya kuwapo kwa mabasi ya jumuiya ambayo yatasaidia abiria ambao hawana magari binafsi kurahisishiwa usafiri.

Na katika hali hiyo, serikali iliona umuhimu wa kuanzisha mabasi yaendayo kwa haraka ili kuepuka msongamano wa magari na kuwarahisishia abiria kufika sehemu zao za kufanyia shughuli kwa haraka.

Ili kuwezesha sekta hiyo inakuwa endelevu, Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), imesema imejipanga kuongeza mengine 177 ili kuboresha huduma hiyo.

Ahadi hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa DART, Dk. Edwin Mhede, wakati wa kikao cha pamoja baina ya viongozi wa taasisi hiyo, wakuu wa wilaya na wakuu wa polisi wa Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa wakala huo wakati wowote DART itasaini mkataba na mzabuni na baada ya kusaini mabasi hayo yatawasili nchini ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo na kuanza kutoa huduma kwenye sehemu zitakazoainishwa.

Kwetu tunasema hatua hiyo ni nzuri na itarahisisha huduma ya usafiri kwa wananchi wengi.

Pia kutokana na hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko, mabasi hayo yatakapoongezwa yatasaidia idadi ya watu wanaosongamana katika magari hayo kupungua.

Kadhalika tuna imani kuwa njia zilizopangiwa magari hayo kupita zikiwamo zinazoelekea kwenye hospitali kubwa kama kutoka Muhimbili kwenda Mlonganzila zitarahisisha wanaougua au kuuguza waende kwenye hospitali hizo kwa urahisi.

DART iliamua kuitisha mkutano wa wadau kuweka mikakati ya pamoja kuhakikisha kunakuwa na ulinzi na usalama wa kutosha kwenye matumizi ya miundombinu ya magari hayo.

Usafiri huo utapelekwa Kibaha Mkoa wa Pwani na kwa sasa wanahudumia makundi maalum kama ya wazee na wenye changamoto za maumbile.

Kwa sasa mabasi yao yanawahudumia watu 180,000 kwa siku na yatakapowasili mabasi mengine idadi hiyo itaongezeka mara dufu na kupunguza muda wa msafiri kukaa muda mrefu kusubiri basi.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Heri James naye alisema wamekubaliana kusimamia miundombinu ya DART na mabasi yake ili watumiaji wa usafiri huo wasipate shida.

Katika kudhibiti matumizi yasiyotakiwa katika barabara zinazopita magari hayo, Mkuu huyo alisema serikali haitawavumilia watu wanaojaribu kuhujumu miundombinu ya DART kwa kuwa serikali imewekeza fedha nyingi kwa lengo la kuwapunguzia adha ya usafiri wananchi wake.

Serikali haitakubali kuona hasara ya mara kwa mara inayosababishwa na watu kupita kwenye miundombinu ya DART wakati hawatakiwi kufanya hivyo na wakuu wa wilaya wamekubaliana kwa pamoja na polisi kusimamia suala hilo kwa nguvu zote.

Ujio wa magari hayo unasubiriwa kwa hamu ili sekta ya usafiri nchini iendelee kuimarika.