Hafla hiyo ya kuwaapisha mawaziri hao ilifanyika Ikulu, Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali wakiwamo wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Mawaziri walioapishwa ni Innocent Bashungwa ambaye amekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Angelah Kairuki Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kabla ya mabadiliko hayo, Bashungwa alikuwa Waziri wa Nchi TAMISEMI, Dk. Tax Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakati Kairuki ameteuliwa kuwa mbunge na waziri.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Rais Samia aliwahimiza mawaziri hao pamoja na wengine walioko kwenye nafasi mbalimbali kuheshimu viapo, mipaka yao ya utendaji na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kutunza siri za Baraza la Mawaziri na serikali kwa ujumla.
Rais alisema mawaziri hao wameapa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, hivyo wanapaswa kutambua kwamba wanafanya kazi katika nchi yenye pande mbili. Kwa mantiki hiyo wanapaswa kuzingatia mipaka ya kazi zao pamoja na kujishusha na pia wanatakiwa kuheshimu viapo vyao.
Lakini kubwa na pengine alilisisitiza kwa umakini mkubwa ni kutunza siri kama walivyoapa au zile za Baraza la Mawaziri na wanazoambiwa katika utendaji wao wa kila siku. Bila kuuma maneno, Rais alisema baadhi ya wateule wamekuwa wakitoa siri jambo ambalo ni makosa.
Aliweka bayana kuwa mwingine anaagizwa kutekeleza jambo, lakini anatoa siri kwamba haikuwa dhamiri yake kutekeleza suala hilo kwa namna linavyofanyika isipokuwa ametakiwa kufanya hivyo.
Kutokana na utoaji huo wa siri, aliwataka kutambua kwamba jambo linapotolewa kwa ajili ya utekelezaji ni la watu wote na si la aliyotoa maagizo. Kwa maana hiyo, katika jambo hilo, Rais alisisitiza uwajibikaji wa pamoja ndani ya serikali badala ya kiongozi wa ngazi fulani kulifanya kama si lake kwa shingo upande.
Rais, kwa kauli yake hiyo, ametoa somo kwa wateule wa kila ngazi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa weledi pamoja na kutunza siri za ndani ya serikali. Katika kutekeleza majukumu yao, wanatakiwa kufanya kazi kwa kusimamia viapo vyao na kuheshimu miiko ya uongozi ikiwamo kutokutumia nafasi zao vibaya au kwa upendeleo kama walivyoapa viapo vya maadili.
Pamoja na kuheshimu hayo, mawaziri walioteuliwa na kuapishwa pamoja na wale ambao hawakuguswa katika mabadiliko hayo madogo, watambue kwamba Rais amewaamini kwamba wana uwezo wa kumsaidia katika majukumu mbalimbali ya kisekta, hivyo wafanye kwa nguvu, uwezo na maarifa ili kuthibitisha kwamba wana uwezo.
Kadhalika, kwa Bashungwa, Dk. Tax na Kairuki ambao wamepewa wizara za kuzisimamia, wanapaswa kuelewa kuwa majukumu waliyopewa ni mazito kutokana na unyeti wa nchi.
Kutokana na hali hiyo, wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu.










