Wawakilishi wetu michuano  CAF fungeni hesabu awali

03Oct 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wawakilishi wetu michuano  CAF fungeni hesabu awali

MWISHONI mwa wiki hii, Jumamosi na Jumapili wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu kwa upande wa soka, Simba, Yanga, Azam FC na Kipanga ya visiwani Zanzibar, watashuka katika viwanja tofauti kuwania tiketi muhimu kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa upande wa Simba na Yanga, zitakuwa nyumbani na ugenini kuiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa dhidi ya Primeiro de Agosto ya Angola na Al Hilal ya Sudan, zikiwania kufuzu hatua ya makundi.

Simba itakuwa ugenini nchini Angola wakati Yanga ikiwa mwenyeji wa Al Hilal kabla ya mechi za marudiano kupigwa Oktoba 16, mwaka huu na timu itakayopata matokeo ya jumla ndiyo itakayofuzu hatua ya makundi na itakayotolewa itaangukia kucheza mechi za mchujo dhidi ya zitakazovuka raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho ili kuwania kucheza hatua ya makundi ya kinyang'anyiro hicho cha pili kwa ubora na utajiri kwa ngazi ya klabu Afrika.

Simba imetinga hatua hiyo kwa kuitoa Nyasa Big Bullets ya Malawi kwa jumla ya mabao 4-0, ikishinda 2-0 ugenini na kupata ushindi kama huo nyumbani, wakati Yanga ikivuna ushindi mnono wa mabao 9-0 dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini kwa kupata ushindi wa 4-0 mechi ya kwanza na marudiano 5-0, zote zikichezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kwa upande wa Azam FC ambayo imeanzia moja kwa moja kwenye raundi ya kwanza, itaanzia ugenini dhidi ya Al-Akhdar Sports Club ya Libya wakati Kipanga FC ambayo itaanzia nyumbani dhidi ya Club Africain ya Tunisia, yenyewe iliitoa Al Hilal Wau ya Sudan Kusini kwa mikwaju ya penalti 4-3 kutokana na matokeo ya bao 1-1 nyumbani na ugenini.

Hivyo, matokeo hayo kwa ujumla yanatupa matumaini makubwa kwa wawakilishi wetu kuweza kusonga mbele kwenye michuano hiyo ya Afrika na kuzidi kulitangaza soka la Tanzania.

Hata hivyo, ili kutekeleza malengo hayo wachezaji hawana budi kuandaliwa kwa lengo la kuingia uwanjani wakiwa na dhamira moja tu ambayo ni kumaliza mchezo katika mechi ya kwanza ili kuepuka kuwa na mlima mrefu wakati wa marudiano.

Tunatambua ugumu wa michuano hii ya Afrika hususan kwa timu inayocheza nyumbani, hivyo kwa wawakilishi wetu, Yanga na Kipanga FC ambao wataanzia nyumbani, njia rahisi ya kujihakikishia kusonga mbele ni kupata ushindi mkubwa na kuhakikisha hawakubali kuruhusu bao nyumbani.

Katika hilo, hata kwa Simba na Azam FC, zinapaswa kujituma ipasavyo ili kushinda na kama ikishindikana kupata sare, jambo ambalo litarahisisha kazi katika mechi za marudiano wiki ijayo.

Tunaamini wawakilishi wetu wana wachezaji wa kiwango cha juu wakuweza kubadili matokeo uwanjani wakati wowote, hivyo kwa muda huu uliosalia kabla ya mechi hizo ni wakati wakurekebisha makosa madogo waliyoyabaini na kuwajenga wachezaji kisaikolojia ndani na nje ya uwanja.

Sote tunatambua fitina zinazofanywa na timu pinzani katika michuano hii hususan zinapokuwa nyumbani, ambapo hutumia nafasi hiyo kuwavuruga wapinzani wao kisaikolojia, hivyo ni wakati wa kuwandaa wachezaji kisaikolojia ili kuweza kukabiliana na fitina hizo hasa kwa Simba na Azam ambazo zitaanzia ugenini.

Lengo letu ni kutaka kuona zote zikifuzu hatua inayofuata na kuendelea kuipeperusha vema bendera ya nchi kimataifa, hivyo hatuna budi kuwatakia wawakilishi wetu maandalizi mema na mafanikio makubwa katika michuano hiyo.