Amdharau mama yake mzazi, kisa amefanikiwa kuwa daktari!

09Oct 2022
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
Maisha Ndivyo Yalivyo
Amdharau mama yake mzazi, kisa amefanikiwa kuwa daktari!

KARIBU tena msomaji wangu tuendelee na simulizi ya dada aliyemdharau mamaye, kisa amefanikiwa. Alisahau mahangaiko ya mama yake hata kufikia cheo cha udaktari. Je, ataishia maisha ya aina gani?.

Wiki iliyopita nilieleza jinsi mama alivyopambana kwa kufanya kazi mbalimbali kama kufua nguo za watu, kuuza mbogamboga ili mradi ale na kumsomesha binti yake. Alijitahidi hata akamaliza darasa la saba na akabahatika kupata wafadhili wakamwendeleza hadi chuo kikuu. Akafaulu vizuri na kupata kazi ya udaktari. Kumbuka nilieleza kuwa hakuwa na baba alifariki, hivyo kuwa mwana pekee kwa mama yake.

Mama hakutaka kuolewa tena akaelekeza nguvu kumtunza binti yake. Lakini cha ajabu, hata baada ya kupata kazi hakumkumbuka tena mama yake. Mama akawa anadhani pengine binti yake hayupo hai kwani ilipita miaka 14 bila kujua habari zake.

Binti akawa na marafiki zake huko mjini na fedha zake akawa anafurahia nao hakumtaka tena mama yake. Akapewa nyumba nzuri na walinzi kumlinda pamoja na gari kwani alikuwa daktari mkubwa. Akawa anawaambia rafiki zake kuwa hana baba wala mama wala ndugu. Kumbe mama yupo hai anaishi bado maisha duni!

Hebu leo msomaji wangu tuone nini kiliendelea kwa binti huyu daktari. Siku moja dada huyu akakutana na kijana ambaye walisoma wote shule kule kijijini. Wakafurahi sana kuonana kwani ilishapita miaka 14 tangu waonane.

Dada akamwambia nipo hapa kwenye hospitali, nina cheo cha udaktari na nyumbani kwangu ni pale. Wakaongozana hadi nyumbani kwake, kijana akafurahia mafanikio yake! Wakakumbushana ya shule, wakacheka kisha kijana akaondoka zake.

Ikapita takriban miaka miwili hivi kijana akaenda kijijini kutembelea jamaa zake. Akiwa huko akakutana na mama yake yule dada daktari. Akamshangaa, Jamani mama upo? Mama alikuwa bado katika hali duni kama alivyomwacha zamani.

Yaani hakuna kilichobadilika kwake. Kijana alilia sana akijiuliza inakuwaje nimekutana na binti yake maisha mazuri ya kifahari. Kwa nini mama anaishi maisha mazingira magumu?

Hali hiyo ilimsumbua sana, akamwambia, mama, nilikutana na binti yako. Mama akasema hapana , umekosea, huenda uliona vibaya. Akamwambia, hapana, tumepiga hadi picha kwa simu hii, huyu hapa muone!(akamwonyesha).

Mama anaangalia picha ya mtoto wake, anaona ni kweli ndiye, kawa mdada kapendeza. Akamwambia kwa sasa ni daktari mkubwa kule jijini Dar es Salaam. Mama aliwaza mengi akijiuliza nini kimemfunga binti amsahau wakati wako wao wawili tu?

Mama akamwambia kijana, kwa sababu umesema utarudi mjini Ijumaa, basi ngoja nijiandae twende wote nikamwone kwa macho. Kijana akasema sawa kwa kuwa najua hadi nyumbani kwake tutakwenda kwa neema ya Mungu!

Ijumaa ikawadia wakaondoka hadi nyumbani kwa binti yake. Wakakuta bado hajarudi toka kazini. Walikuwapo walinzi, kijana akawakabidhi na kuwaambia kuwa huyu ni mama mzazi wa daktari. Wakabaki wanashangaa kwa kuwa dokta alishasema hana baba wala mama wala ndugu yoyote.

Baada ya saa kadhaa daktari akafika nyumbani walinzi wakamwambia, bosi kuna mgeni wako. Akamwangalia kwa dharau, mama akafurahi akanyanyuka amsalimie. Binti akarudi nyuma akamwambia ‘do not touch me! ’(usiniguse)!

Mama Kiingereza hajui, akadhani amemwambia karibu, kumbe amemnyanyapaa. Mama anazidi kumkaribia, binti anamwambia, usiniguse, umepotea njia? Mama akashtuka, kumbe ndiyo maneno yako hayo ya kimombo yalikuwa yakimaanisha? Nilidhani unanikaribisha mwanangu kumbe unanifukuza?

Mama akamtaja bintiye kwa majina yake. Akamuuliza nini kimekupata? Nani kakuroga? Naye akamjibu; mimi sina baba wala baba. Mama akamwambia, yaani ulishanizika? Mama alifadhaika sana, akaishiwa nguvu akatafuta sehemu akakaa chini.

Yule dada akaingia zake ndani kwa jeuri bila kujali na kuendelea na shughuli zake. Mama akaanza kuwaza jinsi alivyokuwa anahangaika kukata kuni na kuuza, kufua nguo za watu na kutembeza biashara ya mboga mboga ili aweze kupata mlo wa siku pia kumsomesha binti yake huyu.

Lakini leo amefanikiwa ananiambia usiniguse, tena kwa kimombo ambacho mimi sikusoma, naye anajua hilo? Mama akajitia nguvu kwa Bwana na kumuomba Mungu amsamehe asije akatamka mabaya kwa binti yake.

Mpenzi msomaji, kisa kinaendelea Jumapili ijayo. Je, mama alienda wapi usiku ule? Je, una kisa? Ujumbe 0715268581.