Ilipangwa kucheza dhidi ya Mufulira Wanderers ya Zambia, ambayo ilikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu wakati huo kimpira kuanzia timu yenyewe pamoja na kikosi chao cha timu ya taifa.
Ikiwa na wachezaji wengi wanaochezea timu ya taifa, timu hiyo ilifika nchini Tanzania kucheza na Simba Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam (sasa Uhuru).
Kwenye mechi hiyo Simba ilipokea kipigo cha mabao 4-0 na ilitakiwa kwenda nchini Zambia kwa ajili ya mechi ya marudiano wiki mbili zijazo. Ikumbukwe kuwa wakati huo michuano ya kimataifa ilichezwa kila baada ya wiki mbili, mechi ya nyumbani na ugenini kutokana na miundombinu na usafiri wakati ule.
Kila mmoja alikata tamaa. Siyo viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba, lakini hata watangazaji wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambao walitakiwa kwenda kutangaza mechi hiyo moja kwa moja, hawakujisumbua.
Ni kama kila kitu kilisambaratika. Hata wachezaji walikata tamaa, baadhi yao wakaondoka kwenda nchini Oman kucheza soka la kulipwa.
Siku zilipokaribia, viongozi wachache wa klabu walikusanya wachezaji wakawaweka kambini kwa ajili ya mechi ya marudiano. Hakuna aliyeingia tena gharama ya usafiri wa ndege. Badala yake serikali iligharamia kwa kutoa behewa moja la treni ya TAZARA kwenda nchini Zambia.
Timu ilisafiri kinyonge na wala hakuna aliyeitilia maanani. Mechi ya marudiano ilichezwa mgeni rasmi alikuwa ni Rais wa Kwanza wa nchini hiyo, Kenneth Kaunda.
Kwa namba ambayo haikutarajiwa Simba iliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0, yaliyofungwa na wachezaji wawili tu, Thuwein Ally akifunga 'hat-trick' na George Kulagwa akipachika mawili.
Kaunda hakuamini na ilibidi aulize kama wachezaji wale wa Simba ndiyo wale wale waliocheza Tanzania au kuna mamluki. Akawaambia ndiyo hao hao. Akaondoka uwanjani wakati bado Simba ikiongoza mabao 4-0.
Ushindi huo uliifanya Simba kusonga mbele ya michuano hiyo kwa namna iliyoshangaza Afrika nzima kiasi kwamba hadi leo hii mechi hiyo ipo kwenye moja kati ya matukio ya ajabu na ya kukumbukwa kwenye soka la Afrika na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), huposti tukio hilo kila mwaka ikifika tarehe hiyo.
Nchini Tanzania kwa sababu hakukuwa na teknolojia kama sasa hakuna aliyefahamu hilo mpaka matokeo ya mechi hiyo yalipotangazwa saa mbili usiku kwenye taarifa ya habari na kuifanya nchi nzima kuzizima.
Nimeamua kuanza na tukio hili lililotokea miaka 43 iliyopita kuzikumbusha klabu za Tanzania kuwa kwenye soka lolote linaweza kutokea sehemu yoyote.
Juzi Yanga imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Hilal ya Sudan kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam ikifungwa mabao 3-0 kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Akhdar.
Nilivyofuatilia sehemu mbalimbali za vijiwe vya soka na kwenye mitandao ya kijamii ni kama mashabiki wameshaanza kukata tamaa.
Wanaona ni kama Yanga ambayo inakwenda kucheza ugenini, Khartoum sehemu ambayo ni ngumu sana kutokana na mazingira pamoja na aina ya ushangiliaji wa mashabiki wao.
Wingi wa mabao ambayo Azam imeruhusu inawapa shaka mashabiki kuamini kuwa timu hiyo inaweza kupindua mechi kwa ushindi wa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Kwenye soka lolote linawezekana kama ambavyo mfano huo nilioutoa na unavyojieleza. Kama Simba ilikwenda kushinda ugenini mabao 5-0, kwa nini Azam ishindwe kupata mabao 4-0 nyumbani?
Kwa nini Yanga ishindwe kupata ushindi ugenini dhidi ya Al Hilal? Kila kitu kinawezekana kama mikakati itawekwa na timu zikajipanga. Pamoja kuwa na mashabiki wenye vurugu, lakini kama timu ikiwa bora, Wasudan wanafungika kwao.
Simba iliifunga Al Merreikh nyumbani kwao bao 1-0 mwaka 1994 kwenye Klabu Bingwa Afrika na kusonga mbele, na mwaka huo huo, iliifunga timu hiyo hiyo mabao 2-1 kwenye Kombe la Kagame wakati huo likiitwa Kombe la Afrika Mashariki na Kati lililochezwa nchini humo, ingawa mashabiki wao walivamia uwanja na kuwapiga hadi kuwajeruhi wachezaji wa Simba kiasi cha baadhi kulazwa hospitalini.
Hiyo ni kuonyesha timu ya Tanzania ina uwezo wa kuifunga timu ya Sudan nyumbani kwao kwa sababu imeshatokea huko nyuma na Yanga isihofu kwa hilo.
Kinachotakiwa sasa ni mabenchi ya ufundi kuzitengeneza timu hizo kimbinu na wachezaji kuwa na utayari kwa kwenda kupambana na kukabiliana na mazingira magumu ya kucheza ugenini.
Mashabiki wa soka watulie, kila kitu kinawezekana, haiwezekani ikawa mwisho kabla hujafika mwisho.