Pamoja na kwamba Baba wa Taifa hayupo, ninaamini kwamba, fikra, mawazo na falsafa zake bado zinaendelea kuishi katika vichwa vya Watanzania wenye mapenzi mema na nchi yao na kimsingi, alijaliwa kuwa na uwezo wa mawazo na kuyafanyia kazi kwa vitendo na kupata matokeo na pia alikuwa na ujuzi wa kubadili fikra hizo kuwa uhalisia ambao unaweza kuonekana hata leo.
Yapo mawazo na fikra zake nyingi, miongoni mwake ilikuwa ni kutamani kuyaona nayo ni elimu inayolingana na uhitaji wa jamii, huku akitilia mkazo iwe ya kujitegemea, kwa kuwa alikuwa anatambua umuhimu wake.
Kwa waliobahatika kupata elimu ya kujitegemea, watakumbuka kuwa huo ulikuwa ni mwanzo kuhusu mfumo wa elimu ilioendana na uhalisia wa jamii iliyokuwapo wakati na baada ya uhuru.
Hiyo ilitokana na ukweli kwamba, aliamini elimu hiyo ingekuwa ufunguo wa ujenzi wa jamii mpya ya Watanzania ambao walikuwa wamenaswa na makucha ya wakoloni.
Ili kutimiza lengo hilo katika elimu, aliamua kupitia sera ya vijiji vya ujamaa wale wote wanaopata elimu, wanapohitimu warudi vijijini kwao watumie elimu waliopata kuleta maendeleo.
Kwa ujumla ni kwamba, elimu ina jukumu muhimu katika maisha ya kila siku kwani inasaidia kuwafanya vijana kuwa na ujuzi ambao wanaweza kuutumia vizuri na kujiletea maendeleo
Ninadhani Baba wa Taifa aliona mbali alipoanzisha elimu hiyo, ili kwamba mwanafunzi anapohitimu, awe na kitu cha kufanya kupitia elimu aliyopata, ili aweze kunufaika nayo na kuinufaisha jamii yake pia.
Lakini sasa baadhi ya wanafunzi wanasoma na kuhitimu, kisha wanarudi nyumbani kwao kugeuka kuwa mzigo kwa familia zao badala ya kuwa suluhisho la matatizo ya jamii kupitia elimu aliyopata.
Kwa mfumo huo wa elimu ya kujitegemea, alitamani wasomi waitumikie jamii, wakati serikali, baada ya wazazi na walezi kutoa fedha na rasilimali nyingi kuwasomesha, hivyo walikuwa na deni la kulipa kwa kuitumikia jamii.
Wakati huu Tanzania inapoadhimisha kumbukumbu ya miaka 23 ya kifo chake, ni vyema akaenziwe kwa kurejesha elimu ya kujitegemea ili kuwafanya wasomi wa sasa kuwa sehemu ya jamii.
Badala ya kuelimika na kwenda kujichimbia kwingine au kuzunguka kupata ajira, basi wakishapata elimu warudi katika jamii waliyotoka kusaidia kuleta maendeleo na si kujitenga na kujiona hawawezi kushirikiana na jamii yao.
Ikumbukwe kwamba kile ambacho Baba wa Taifa alikusudia kwenye elimu, ni kuitafuta na kupata maarifa ambayo ni suluhisho la matatizo yanayowakabili watu na yeye mwenyewe.
Ukweli ni kwamba mchakato wa elimu ya kujitegemea kwa undani wake unaweza kupata mambo mengi ya kuvutia uhusiano na sifa za kibinadamu, fursa, tamaa na mahitaji kwa ajili ya maendeleo yake na jamii inayomzunguka.
Mtu anaweza kupata ujuzi ikiwamo ualimu akaenda katika jamii akasaidia kuondoa adui ujinga, mwingine anaweza kupata ujuzi wa udaktari na fani nyingine nyingi za kuweza kusaidia kwenye jamii yake.
Hivyo, kwa ujumla wake elimu ya kujitegemea inaweza kupunguza wahitimu kuzunguka na vyeti katika ofisi mbalimbali kutafuta kazi, badala yake watatumia ujuzi waliopata kujiajiri, pongezi serikali kwa kujitahidi kujenga vyuo vya ufundi kila kata, kwani bila kufanya mabadiliko kama hayo, tunaweza kuendelea kuzalisha wasomi wengi ambao haiwezi kuwa na msaada au kutatua matatizo katika jamii yao.