Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Yanga leo watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kucheza dhidi ya Al Hilal kutoka Sudan kuanzia saa 10:00 jioni , katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na saa 2:00 usiku, wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam FC watakuwa ugenini Libya kuwakabili wenyeji Al Akhdar SC, mechi ikitarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Martyrs of Februari.
Kesho kwenye Uwanja wa Estadio 11 de Novembro, nchini Angola, Simba itashuka kuwavaa Primeiro de Agosto kuanzia saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Kwenye mechi zote hizi ambazo mbili zinacheza uganini na moja nyumbani, matarajio ya ushindi wa Watanzania ni makubwa kutokana na jinsi timu hizi zilivyojipanga.
Hii inatokana na usajili mkubwa ambao imefanya pamoja na ukweli kuwa ndiyo kwa sasa zinatawala soka la Tanzania.
Zina wachezaji kutoka pande mbalimbali za Afrika ambao wanatarajia kucheza mechi hizo bila hofu yoyote ile.
Wakati ratiba hii inatoka, Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Wallace Karia, alikaririwa akisema anatamani timu zote zifanye vyema ili kuzilinda nafasi nne ambazo Tanzania imezipata.
Ukweli ni kwamba ni misimu miwili mfululizo sasa Tanzania inapeleka timu nne, mbili katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine mbili kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, lakini hizi si nafasi za kudumu.
Ni nafasi zinazotegemea kufanya vizuri kwa timu zinazoshiriki michuano hiyo ya kimataifa.
Ikumbukwe kufanya vizuri kwa Simba kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ndiko kwa mara ya kwanza kuliifanya Tanzania kuingiza timu nne mwaka 2019, huku zali ikiidondokea KMC ambayo ilicheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza na moja kwa moja ikaenda kucheza kimataifa kabla ya kutolewa na AS Kigali ya Rwnada.
Kutolewa kwa Simba na UD Songo ya Msumbiji mechi ya raundi ya kwanza kuliifanya Tanzania kunyang'anywa tena nafasi ya kuwakilishwa na timu nne kwa sababu kuna klabu za nchi nyingine zilikuwa zimevuna pointi na kuipiku Bongo, lakini msimu uliofuata Wekundu wa Simba walifanya tena vyema na nafasi zikarejea.
Kwa sababu tayari timu, nchi na mashabiki wameshaonja ladha ya kupeleka timu nne, itakuwa ni aibu na simanzi kubwa timu zetu zikatolewa kwenye hatua hii na kuzipa mwanya timu za nyingi zingine kuizidi Tanzania pointi mwakani tukarejea kupeleka timu mbili tu.
Kwa sasa Ligi Kuu Tanzania Bara inatajwa kuwa moja kati ya ligi bora hapa barani Afrika. Kutokana na hali hiyo timu za Simba, Yanga na Azam zina dhima ya kuthibitisha hilo kwa kushinda mechi za leo na kesho, pia kupigana kufa na kupona kusonga mbele ili kuongeza pointi na kuendeleza uwezekano wa kupeleka timu nne msimu ujao.
Ikumbukwe kama Simba na Yanga zikitinga makundi tu, Azam nayo ikapita kwenye hatua hii, si tu Tanzania itaongeza pointi ambazo zitaiwezesha msimu ujao kupeleka timu nne tu, lakini hata misimu miwili mfululizo bila kutegemea matokeo mazuri ya msimu ujao.
Hiki ndicho kinachotakiwa kifanywe kwa timu za Tanzania. Kipindi hiki ambazo timu zinaonekana ziko vizuri ndiyo kipindi cha kukusanya pointi nyingi kiasi kuwa kama nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Misri, Tunisia na Morocco ambao pointi zao hata kama misimu mitatu hakuna timu yoyote itakayoshiriki michuano ya kimataifa, hakuna nchi ya kuzidondosha na kuzipiku zikapeleka timu mbili.
Pia, tunaiombea heri, Kipanga ya Zanzibar ambayo leo inacheza dhidi ya Club Africaine ya Tunisia katika mechi ya hatua ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kipanga ikiwatoa Waarabu hao, itaweka rekodi ya kutinga hatua ya makundi kwa mara ya kwanza.
Kila la heri timu zote za Tanzania kwenye michuano hii mikubwa barani Afrika.