Juhudi za kuwa na idadi ya wanawake katika ngazi za maamuzi likiwamo bunge bado ni tatizo muda wote likibakia kuhusishwa na mfumo dume unaokandamiza wanawake na kuwanyima fursa za kujitutumua na kuonyesha uwezo wao.
Lakini, wakati mwingine shida si mfumo dume pengine hata kuwa na maarifa au ujasiri wa kusimama jukwaani na kujenga hoja. Haya ni mambo ya kujifunza pia, hivyo watu wasidhani kuwa ya kujifunza ni hesabu pekee hata kuongea, kutembea hadharani ni kuweka ajenda zinazoeleweka hadharani.
Kwa mfano, inaelezwa kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, wabunge wa kuchaguliwa katika majimbo walikuwa 264 wanawake wakiwa ni 26 pekee, anasema Seleman Bishangazi, Mkurugenzi wa Kituo cha Sauti Jamii Kipunguni Dar es Salaam, kinachofanyakazi pamoja na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), akihimiza kuwa ni vyema kinamama wakafahamu namna ya kujieleza na kuomba kura majukwaani. Si kwenye siasa lakini katika masuala yanayohusu maisha ya kila siku.
Anazungumza katika mafunzo kwa vitendo ya kuwajengea uwezo wanawake, ili wajiandae kuwania uongozi kwenye uchaguzi ujao, akieleza kuwa hali si shwari kujifunza kuomba kura ni jambo la msingi: "Taarifa ya Umoja wa Mabunge ya Dunia (IPU) ya mwezi Februari, 2022 kuhusu idadi ya wabunge nchini, inaeleza kuwa wabunge wa kuchaguliwa katika majimbo ni 264, wanawake ni wachache mno.”
Taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inasema kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, madiwani waliochaguliwa ni 3,953, huku wanawake waliochaguliwa wakiwa ni 260.
Kutokana na taarifa hiyo juhudi zinahitajika zaidi kuwainua kama kituo hicho kinavyofanya kwa kuanzisha mafunzo kwa vitendo, ili kusaidia wanawake kupata mbinu mbalimbali za jinsi ya kusimama majukwaani kuomba kura kwa wananchi.
Si jambo geni mbinu na elimu mbalimbali zinatumiwa kuwawezesha wanawake kuingia kwenye ulingo wa kisiasa na kuwa viongozi lakini bado mambo hayatengamaa ndiyo maana baadhi ya wadau wa kutetea haki zao wanabuni mikakati mipya.
Mafunzo hayo ya miezi sita, yaliyoanza mwezi uliopita yataendelea hadi Desemba mwaka huu, yakihusisha wanawake kutoka katika kata za Kipunguni na Majohe.
Kazi ya kusaidia wanawake kuwa viongozi na kuifikia ajenda ya ‘50/50’ inahusisha wengi ndiyo maana Women Fund (WFT), wanawezesha mafunzo hayo ya kuwajenga wanawake ili waweze kusimama bila woga na kujinadi kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2024 na 2025.
Bishagazi anasema kwenye mafunzo hayo, wanaandaa mfano wa mikutano ya kampeni na kuwasimamisha wanawake wenye nia ya kutiania kila mmoja kwa wakati wake anajinadi mbele ya wenzake wanaokuwa katika mafunzo hayo.
Ni vyema masuala kama hayo yakafikishwa vijijini na kinamama wakapata fursa kwani huko ndiko waliko wanawake wengi zaidi na wanaohitaji kubadilishwa kuanzia misimamo, mitizamo na mienendo.
Kinachowakwamisha wanawake ni pamoja na kushindwa kujinadi, wanapoomba kura, lakini pia ni waoga wanapoulizwa maswali na kuyajibu hivyo wakisaidiwa kuondokana na hofu hiyo kutasahihisha kasoro zinazowakwamisha.
Hata mimi naamini kwamba kwa njia hii watajengewa ujasiri na kujiamini na kuwahamasisha zaidi kusimama mbele za watu kutetea haki zao si kwenye uchaguzi.



.jpg?itok=nfwjwDzv)






