Ninajiuliza kwanini viongozi wa chama waendelee kuruhusu mipasuko ya makundi kuanzia wanachama hadi viongozi, hasa unapofika wakati wa kugombea uongozi wa ngazi mbalimbali kuanzia kwenye mashina hadi mikoa.
Hapo ndipo, utaona viongozi wanaopaswa kusimamia wanashindwa kuhakikisha kuwa kunakuwapo na siasa bora zenye kundi moja au kupata viongozi watakaoweza kukivusha na kusonga mbele katika utekelezaji wa ilani baada ya uchaguzi.
Kuwapo kwa makundi, fitina, majungu, kuchafuana wenyewe kwa wenyewe iwe wanachama, viongozi au wagombea, kadhalika ubaguzi wa kijinsia, minong’ono ya ukabila, ukanda na udini vyote vinasababisha mpasuko, mgawanyo na makundi ndani ya vyama.
Wanachama wanaosababisha yote hayo ni wale wenye tamaa ya madaraka, au wanaotumiwa na maadui kuviangusha vyama vyao au wanaoamini kuwa ndiyo wenye nguvu wakitaka wapishwe na wale wanyonge.
Inawezekana ni nguvu ya pesa za kuwajaza wanachama waliozoeshwa hivyo na baadhi ya viongozi au wagombea wakati wa uchaguzi au hata kutumiwa na maadui ili kukivuruga chama.
Ukitaka kupata majibu yake bila kificho ni nyakati za uchaguzi ndani ya chama, au kampeni zinapoanza, ukitumika msamiati kwamba wao hawashindani bali wanapanga na kuchagua uongozi wanavyoona au kutaka.
Matatizo yanaibuka wakati wa kuanza mchakato wa uchaguzi kwenye serikali za mitaa, vitongoji na wenyeviti wa vijiji dhidi ya wapinzani wao.
Hali kadhalika, wakati wa uchaguzi mkuu kwenye nafasi za madiwani, wabunge na hata Rais. Ndiyo muda wa kutoana jasho wagombea wakianza kulizwa kwenye kura za maoni na wakati mwingine hata kutishiana vikali, huku wengine chuki zikitawala mioyoni na kushindwa kusalimiana.
Tatizo la rushwa nalo ni miongoni mwa ugonjwa unaochangia mipasuko na makundi na migawanyiko mbalimbali ndani na nje ya vyama.
Mfano, mkoani Mwanza hivi karibuni kumekuwapo na uchaguzi lakini katika baadhi ya maeneo zimeripotiwa figisu na pengine kura zinapigwa hata usiku.
Kuna sehemu uchaguzi ulifutwa kutokana na wagombea wengine kudai kuwa wenzao wameteuliwa badala ya kuchaguliwa na kuhoji sababu ya viongozi kujipangia safu za wanaowataka badala ya kufanyika uchaguzi kama katiba na sheria zinavyoelekeza.
Leo, CCM imetimiza miaka 45 tangu kuzaliwa mwaka 1977, kikiwa ni chama kikongwe bado wanachama wake baadhi wanadaiwa kufanya siasa kwa utaratibu wa bora liende, kama ilivyotokea Mwanza.
Huenda ndiyo sababu Mwalimu Julius Nyerere, Baba wa Taifa, alianzisha vyuo vya siasa ili watu wajifunze siasa bora zenye manufaa kwa chama.
Swali langu kwa wenye vyama ni hili, hivi siasa za makundi na kusalitiana zitaisha lini? Sitaki kuzungumzia yanayotokea CUF wala NCCR-Mageuzi, lakini ni lini mabadiliko yatakuja ili kuwapata viongozi bora badala ya bora viongozi wanaolelewa na kukuzwa na migogoro isiyokwisha?
Migogoro mingi inaripotiwa kwenye vyama na kinachoonekana ni baadhi ya wanachama na viongozi kuwa madalali wa kutafuta fedha ili kujinufaisha.
Rais Samia Suluhu Hassan, ameruhusu demokrasia kuchukua mkondo wake katika vyama vyote ya siasa lengo ni kuleta mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kuondoa itikadi za kibaguzi ndani ya vyama na kuwa na mazingira yanayowapa Watanzania haki ya kushiriki siasa kwa amani, lakini vyama havijatulia na kutumia fursa hiyo.
Ni wakati wa kubadilika na kuwang’oa viongozi wasioleta mabadiliko bali migogoro ndani ya vyama na kusababisha mipasuko na makundi yanayoharibu sifa za vyama.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








