Kuna kitu nimeanza kukiona ambacho si kizuri kwenye mustakabali wa soka la Tanzania. Nacho ni baadhi ya klabu kuacha idadi kubwa ya wachezaji hasa wa Kitanzania.
Pia kwa sasa klabu hata zile zinazoitwa au kujiita ndogo kuanza kushusha wachezaji wa kigeni. Hapa kuna shida mahala.
Kama vile haitoshi nimemsikia Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo kukiri kupokea maoni mbalimbali ya wadau wa mpira wa miguu kwa ajili ya maboresho ya kanuni za Ligi Kuu msimu ujao wa 2022/23, huku suala ya wachezaji 12 wa kigeni likiwa miongoni mwa maoni hayo.
Kifupi tu ni kwamba wengi waliopeleka mapendekezo wametaka wachezaji wa kigeni wote wacheze.
Kanuni ya msimu uliopita iliruhusu wachezaji wanane tu kuanza kikosi cha kwanza
"Ndiyo, tumepokea maoni, tofauti kutoka kwa wadau ni klabu, kila mmoja anataka kuonyesha ni namna gani nzuri inatakiwa iwe, lakini maoni mengi yameelekeza wachezaji wa kigeni ikiwezekana wapewe nafasi au fursa ya kucheza wote, lakini kama ninavyosema ni mapema sana bado tupo kwenye huo mchakato, tutapeleka kwenye vikao halali vitaamua kwa sababu hili ni jambo la kanuni siyo jambo la Bodi, wala TFF (Shirikisho la Soka Nchini), ni la wadau wenyewe, ambao ni klabu, wenyewe ndiyo wataamua ni namna gani ambavyo wanataka wachezaji wa kigeni, 12 wacheze wote, au wanane kama ilivyokuwa msimu uliopita, sisi tuko tayari kulingana na mahitaji ya wadau wenyewe ambao wana fursa ya kutumia wachezaji hao na kuwamiliki pia," alisema Kasongo.
Binafsi mimi siyo muumini wa kuwatetea wachezaji wa Kitanzania, eti wapunguzwe wachezaji wa kigeni kwa ajili ya kuwabeba wazawa.
Mimi naamini kuwa kila mchezaji acheze kwa uwezo wake, awe mgeni au mzawa.
Iwapo kanuni hii itapita itakuwa mwiba kwa wachezaji wa Kitanzania ambao hawajitumi, kwani makocha watakuwa wakichagua wachezaji wenye uwezo na wenye kujituma mazoezini.
Hapa sasa ndiyo inatakiwa wachezaji wa kizawa wafanye kazi ya ziada kupambana ili kupata namba.
Hii ni kengele ya hatari inaanza kugonga kwa wachezaji wa Kibongo.
Wakati hii inaweza kuwa mwiba kwa wachezaji wa kizawa hasa wa Simba, Yanga na Azam, ambao ndiyo wenye uwezo kusajili wachezaji 12, huku kwenye klabu ndogo nako naona taratibu hata zile timu ambazo zilikuwa hazichukua wageni kutoka nje, zimeanza kufanya hivyo.
Ina maana kuna sehemu ambapo wachezaji wa Kitanzania hawafanyi vema. Ninaamini, kama wangekuwa wako vema, sidhani kama Mtibwa Sugar, au Coastal Union zingeanza kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi.
Tuangalie klabu kama Prisons, Dodoma Jiji na KMC zimeacha wachezaji wengi sana. Ingawa ni kwa sababu mbalimbali, lakini wengi ni kwamba klabu zimewaacha kutokana na kutoridhishwa na viwango vyao.
Kila timu hapo imeacha wachezaji wasiopungua 10. Ukimsikiliza Thobias Kifaru wa Mtibwa na Christina Mwagala wa KMC wameachana na wachezaji hao kutokana na kutokidhi matakwa.
"Unapotaka kujenga timu ni lazima ufanye maamuzi magumu, tumeacha wachezaji wengi kwa sababu tunataka kujenga timu imara." Anasema Mwagala.
"Hao tulioachana nao mikataba yao imemalizika na hatukutaka kuendelea nao, kwa sababu hawa ndiyo waliotufanya kucheza 'play off' kwa misimu miwili mfululizo. Anasema Kifaru.
Hii inaonyesha wengi wameondoka kwa kutoonyesha kipya, na hakuna ubunifu.
Lakini wachezaji hawa hawa wamekwenda kujiunga na klabu zingine. Huyu ametoka huku kwenda huku na huyu ametoka huku kwenda kule.
Ninachowaasa sasa wachezaji wa Kibongo waanze kujitathmini. Wameanza kuonekana ni wa kawaida sana hata kwenye klabu za kawaida. Huko mbele tunakokwenda itakuwa hatari.
Wabadilike na kupambana kwa kuzipigania timu zao. Kutojituma, kuhujumu, na kutopambania timu kinatajwa kuwa ni moja ya sababu ya kutoaminika.
Hii ni nafasi ya mwisho kwao. Haiwezekani straika umalize ligi una mabao matano tu.
Isije baadaye ukazuka mjadala wa kutaka kuonewa huruma huku wenyewe wanashindwa kujitathmini.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








