Tutambue hizo dalili nane za  mgunda na kuchukua hatua

28Jul 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tutambue hizo dalili nane za  mgunda na kuchukua hatua

MLIPUKO wa ugonjwa wa mgunda ambao sasa umekuwa ni mjadala miongoni mwa Watanzania baada ya kuibuka wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi na kudaiwa kusababisha vifo vya wale waliokumbwa nao.

Ugonjwa huo pia unajadiliwa kwenye vyombo vya habari, ikiwamo mitandao, kutokana na kwamba unaonekana kuwa mpya, ingawa serikali imeweka wazi kuwa si mpya kwa vile umewahi kutoka mkoani Kigoma.

Tayari serikali imeshasema kuwa homa ya Mgunda au Leptospirosis ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria ambapo kwa mujibu wa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, umekuwa ukiathiri wanadamu na wanyama.

Lakini, pamoja na kuwapo kwa mjadala kuhusu ugonjwa huo, ninadhani ni vyema sasa Watanzania wakaelekeza nguvu katika kutambua dalili za ugonjwa huo, ili wachukue tahadhari pale wanapoubaini.

Wizara ya Afya imeshaweka wazi kuwa, ugonjwa huo una dalili nane ambazo ni homa kali, kuumwa kichwa, maumivu makali, uchovu wa misuli, kupata homa ya manjano hasa kwenye macho na macho kuvilia damu.

Dalili nyingine za ugonjwa huo ambazo Watanzania wanatakiwa kuzijua, zinatajwa na Wizara ya Afya kuwa ni kukohoa na kutokwa damu puani na kichefuchefu kinachoambatana na kutapika, kuharisha na tumbo kuuma.

Hivyo, badala ya kuendelea kuujadili ugonjwa huo, ninadhani ingekuwa ni vyema jamii ingejikita, pia kufahamu dalili hizo ili pale unapojitokeza, iwe rahisi kuchukua hatua sahihi za kuhakikisha hauleti maafa.

Kwa kuwa bakteria wanaosababisha ugonjwa huo huenezwa kupitia mkojo wa wanyama walioambukizwa, na kwamba wanaweza kuingia ndani ya maji au udongo na kuishi huko kwa wiki hadi miezi, suala la tahadhari ni la muhimu.

Watanzania ni wakulima na wafugaji na inaelezwa kuwa aina nyingi tofauti za wanyama wa porini na wa nyumbani wakiwamo ng'ombe, nguruwe, farasi, mbwa, jamii ya panya na wanyama wa porini, hubeba bakteria.

Lakini, kwa kuwa inaelezwa kuwa wanyama hao wanapopata maambukizi, wanaweza kuwa hawana dalili za ugonjwa huo na kuendelea kutoa bakteria kwa kuendelea au kila baada ya muda kwa miezi michache hadi miaka kadhaa.

Jambo la muhimu ni kila mmoja, mtu mzima kutambua dalili za ugonjwa huo zilizotolewa na wizara, lakini kuwa makini, kwa kuwa bakteria wanaweza kuingia mwilini kupitia ngozi au utando wa macho, pua au mdomo.

Inaelezwa kuwa hayo yanaweza kutokea ikiwa ngozi ina mikwaruzo, hivyo suala la kuwa makini ni la muhimu kuanzia kuchukua kila aina ya tahadhari na pia kutambua dalili za ugonjwa huo.

Jamii isichukulie kuwa ugonjwa huo ni wa eneo hilo, kwani Waziri wa Afya anasema ulishawahi kuibuka mkoani Kigoma na sasa umetua mkoani Lindi, ambako ni mbali zaidi ya kilomita 1,000 kutoka Kigoma.

Kwa ugonjwa huo, ni vyema kutumia msemo wa Kiswahili kuwa; 'ukiona mwenzio ananyolewa na wewe tia maji', hivyo wakati upo mkoani Lindi, ni vyema wananchi wa maeneo mengine kuchukua tahadhari.

Ikumbukwe kuwa watu wanasafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine, hivyo ni rahisi aliye na ugonjwa huo kupelekea kwingine kirahisi. Njia nzuri ni kujua dalili zake na kuchukua tahadhari.

Ninaamini kwamba, kujua dalili za ugonjwa huo ni hatua muhimu ambayo itamfanya mtu kwenda hospitali au kituo cha kufanyiwa vipimo unapoona mwili wake hakuna usawa, kabla hali haijawa mbaya.

Tunaambiwa na Wizara ya Afya kuwa, awamu ya kwanza ya ugonjwa ambayo ni homa, baridi, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, kutapika, na kuhara, mgonjwa anaweza kupona kwa muda lakini akaugua tena.

Kwa mujibu wa wizara hyo, homa ya Mgunda inatibiwa na dawa aina ya antibiotics, kama vile doxycycline au penicillin, ambayo inapaswa kutolewa mapema katika kipindi cha ugonjwa huo.

Hivyo, kwa maelezo hayo, ni wazi kwamba, suala la kujua dalili za ugonjwa huo lina uzito wake, ambapo bila kuzijua, mtu anaweza kuugua na kudhani mwingine na kumbe ndio wenyewe, kwa hiyo ni vyema kuwa makini.