Rais kuonya bodaboda, wenye masikio wasikie

27Jul 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Rais kuonya bodaboda, wenye masikio wasikie

BODABODA ni ujasiriamali unaowaondoa vijana wengi wanaoishi mijini na miji midogo Kwenye uzururaji, maisha vijiweni na aina zote za uhalifu.

Kazi hiyo imewaweka barabarani  kwa ajili ya kutoa huduma ya usafiri kwa abiria ikiwa ni ajira inayowawezesha kumudu maisha yao.

Pamoja na fursa hiyo, kumekuwapo na kasoro zinazowakabili madereva hao wa bodaboda, ikiwamo tuhuma za kusababisha ajali za barabarani zinazopoteza maisha yao na ya abiria au ulemavu wa kudumu.

Wanatuhumiwa kutumika kwenye ujambazi wakiendesha pikipiki zilizoibwa na madereva wake kuuliwa, wapo wanaodaiwa kukwapua mali za watu hasa pochi na mifuko ya wanawake vilevile kunyanyasa wanafunzi kingono.

Ni mambo yanayochangia ajira hiyo kuwa chungu iwapo hawatabadilika. Mienendo yao imemshtua Rais Samia Suluhu Hassan, na kutoa onya dhidi ya  kutumika kwenye ujambazi pamoja na uhalifu ili kulinda heshima yao.

Rais Samia anabainisha kuwa baadhi ya madereva wa bodaboda wamekuwa wakikwapua mizigo ya watu pamoja na vipochi hasa vya wanawake na kupoteza uaminifu mbele ya jamii.

"Ninyi ni maofisa usafirishaji wa kitaifa lakini baadhi yenu wanawaharibia sifa hiyo kwa kutumika kukwapua na kupoteza mizigo ya watu pia, kutumika kwa ujambazi. Niwaombe, jilindeni msipoteze sifa zenu nyie ni watu muhimu sana katika taifa letu,”anasema Rais Samia.

Rais amekerwa na tatizo hilo, hivyo ingefaa kila bodaboda kuachana na mtindo huo ambao unaweza kutishia ajira na maisha.

Ingawa Rais amewaomba waache mtindo huo, ni vyema pia wakatambua kuwa hilo si ombi ni amri, hivyo wangetii na kuendesha shughuli zao kama kawaiada bila kusubiri kushurutishwa.

Anayosema Rais ni kweli, kwa vile unapotajwa usafiri kwa wanyonge bodaboda zinahusika, kusafirisha watu kwa gharama nafuu, hivyo ingependeza kama wangeheshimu ajira hiyo.

Wakumbuke kuwa awali walikuwa wakitozwa faini ya Sh. 30,000 wanapofanya makosa ya barabarani, lakini wakalia kilio chao, wabunge wakawatetea hadi kiwango hicho kikashushwa.

Hatua hiyo ya kushushiwa faini, inaonyesha ni jinsi gani ajira yao inavyoheshimiwa, hivyo na wao waiheshimu kwa kuachana na uhalifu.

Binafsi nilishwahi kukumbana na dereva mporaji  saa 11 alfajiri nikiwa katika kituo cha daladala nikisubiri usafiri, akaja huku akionyesha kama mtu mwema na kuniambia nitoe nauli kidogo anisafirishe ninakokwenda.

Lakini kabla ya kumjibu akakwapua mfuko wangu na kujikuta akiambulia mkanda na kuondoka, lakini baadaye akageuza bodaboda yake akaja na kunirushia mkanda huo na kuondoka zake.

Huo ndiyo mtindo wa baadhi ya madereva wa bodaboda, ingawa baadhi yao hudai kuwa wanaofanya hivyo ni 'deiwaka' si wale wanaoendesha pikipiki na kwamba hupewa ili kujitafutia chochote lakini badala yake wanapora watu.

Kama kweli wanaofanya hivyo ni 'deiwaka', basi walioajiriwa kufanya kazi hiyo wasikubali kuharibiwa sifa kwa huruma za kutaka kuwasaidia marafiki zao wajipaatie riziki kupitia pikipiki hizo na kumbe wanazitumia kuibia  watu.

Udereva wa bodaboda ni ajira, ingekuwa ni njia sahihi iwapo madereva wake wataheshimu ajira hiyo kwa kuepuka kujiingiza katika matendo ya uhalifu yanayohatarisha ajira hiyo.

Onyo la Rais Samia kwao litoshe kuwafanya wabadilike, kwani hayo ndiyo matarajio ya kiongozi huyo wa taifa kwa wananchi wake hasa kwa kundi la waendesha bodaboda.

Vilevile, onyo hilo lingewakumbusha pia kuheshimu sheria ya usalama barabarani,kwani wamekuwa wakitajwa kuwa vinara wa kuvunja sheria hiyo na kusababisha ajali.

Kwa mfano, wanapofika kwenye makutano ya barabara, kwenye taa hata kabla hazijawaruhusu kupita, hulazimisha kuivuka upande wa pili hali ambayo imekuwa ikichangia ajali za barabarani.

Wasikie onyo vingine wanajiweka kwenye hatari ya kuwa na migogoro na sheria.