Vitumike viwanja vichache, vingine visipoboreshwa

18Jul 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Vitumike viwanja vichache, vingine visipoboreshwa

KABLA hata ya kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2022/23 hapo Agosti 17, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara imevipiga ‘stop’ viwanja saba vilivyokuwa vinatumika kwenye ligi msimu uliopita hadi hapo vitakapofanyiwa marekebisho.

Viwanja hivyo ni Mkwakwani Tanga, Ilulu Lindi, Ushirika Kilimanjaro, Mabatini Pwani, Sokoine Mbeya, Jamhuri Dodoma na Nyankumbu Girls, Geita.

Kwenye taarifa yao inasema, pamoja na kwamba wanasubiri taarifa ya ukaguzi wa viwanja unaofanywa na Kamati ya Leseni za Klabu iliyo chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini imefanya tathmini ya viwanja vilivyotumika kwenye mechi za Ligi Kuu msimu uliomalizika na kubaini mapungufu kadhaa kwenye viwanja hivyo.

Baada ya kuainisha mapungufu hayo, binafsi naiunga mkono Bodi ya Ligi kwa sababu kama ikileta huruma kwenye hili, basi Tanzania itakuwa inacheza Ligi Kuu yake kama vile bonanza, michuano ambayo haifuati sheria wala kanuni yoyote ile.

Pia kama itafumbia macho suala hili, hakuna nguvu yoyote itakayotumika ili kuvikarabati na hata viwanja ambavyo kwa sasa ni vizuri, basi wamiliki wao hawatofanya mkazo kuendelea kuvifanya kuwa bora kwa kuona na wao wataonewa huruma.

Mapungufu 10 ambayo Bodi ya Ligi imeyabainisha ni mengi sana, tena mengine yana vipengele vyake.

Namba moja ni eneo la kuchezea kutokuwa tambarare na kukosa nyasi za kutosha, pili ni ubovu katika uzio wa kutenganisha mashabiki na eneo la kuchezea, tatu jukwaa kuu kukosa ubora, ikiwamo ubovu wa paa.

Nne ni vyumba vya kuvalia nguo za wachezaji na waamuzi kukosa sifa nne ambazo zimeainishwa pia.

Nao ni ukubwa stahili pamoja na feni, AC kwa ajili ya upatikanaji wa hewa ya kutosha, upatikanaji wa majisafi na ya kutosha muda wote, upatikanaji umeme na uwepo wa vyoo safi na vya kisasa.

Kukosekana kwa mabenchi ya ufundi bora na yenye uwezo wa kuruhusu watu wasiopungua 17 kuketi.

Namba tisa ni kukosekana kwa majukwaa kwa ajili ya watazamaji na 10 ni uwepo na mabango, picha za matangazo zisizotambulika na TFF na Bodi ya Ligi.

Ukiangalia mapungufu haya utaona kuwa kuna mapungufu makubwa na matatizo kwenye soka la Tanzania kwa upande wa miundombinu.

Wakati klabu zikisonga mbele kwa kuwekeza na kusajili wachezaji wa gharama za juu, huku waandishi na mashabiki mbalimbali wa soka Afrika wakianza sasa kulifuatilia soka la Tanzania kutokana na kukusanya wachezaji toka kila pande ya Afrika, viwanja vyetu bado vinatushusha thamani.

Wadhamini mbalimbali, wakiwamo wa televisheni ambao wanaonyesha michezo hiyo wamekuwa wakiliheshimisha soka la Tanzania kwa kuonyesha mechi nyingi, lakini wakati mwingine inakuwa aibu kuonyesha mechi ambayo uwanja hauna nyasi, umechimbika, au maji yametuama mechi inachezwa na matope uwanjani.

Bodi ya Ligi imezitaka klabu zinazotaraji kutumia viwanja hivyo kufanya jitihada za makusudi katika kuboresha maeneo yalioainishwa ili kukidhi matakwa ya kanuni na sheria zinazoongoza mpira wa miguu.

Hii ni kwamba kama haitokuwa hivyo, basi itabidi zihame kwa kuchagua viwanja mbadala.

Cha kufanya hapa ni kwamba klabu zishirikiane na wamiliki wa viwanja ili kukarabati sehemu ambazo kwao zina changamoto ili viruhusiwe.

Kwa hali hii ni afadhali hata ligi ikachezwa kwenye viwanja vichache kuliko viwanja vibovu ambavyo vinaharibu ladha ya soka, mifumo wa makocha, ubora na ufundi wa wachezaji miguuni pamoja na ligi yenyewe.

Ni bora ligi iwe inachezwa kila siku, mchana na usiku kwenye viwanja vichache vyenye ubora kama Benjamin Mkapa, Azam Complex, CCM Kirumba, Nyamagana na Kaitaba kuliko ligi ya Tanzania ambayo kwa sasa imekuwa na hadhi kubwa Afrika kuchezwa kwenye viwanja visivyokidhi viwango.

Tunajua kuwa serikali imesema itavitengeneza baadhi ya viwanja, hiyo ni baadaye, lakini kwa muda huu ambao msimu wa Ligi Kuu 2022/23 unataka kuanza ni lazima timu zinazotaka kutumia viwanja hivyo kushirikiana na wamiliki wa viwanja kwa ajili ya kuweka mambo sawa.