Baada ya kuchukua mzigo wako, moja kwa moja unakwenda kuweka kwenye mashine maalum, ambayo lazima upitishe kila ulichonacho ikiwamo kompyuta mpakato (laptop).
Ziko aina nyingi za mashine hizi zinazoweza kutunza mizigo ya abiria wanaotoka nje ya mkoa na nchi lengo likiwa kuzuia visivyoruhusiwa kuingia nchini na ndivyo inavyofanyika kwenye mipaka yote nchini.
Ziko pia mashine ambazo mzigo ukishapita unaupokea upande wa pili na kutokana na kasi ya mashine hadi unafika mzigo wako umeshasogezwa mbele zaidi ambako hutegemea aina ya mashine.
Mashine ambazo zinaacha mizigo yenye kuvunjika salama ni ambazo mbele zina meza ambayo inawezesha mizigo kukaa vizuri bila uharibifu.
Tatizo kubwa ni kwa zile ambazo mzigo ukishatoka kwenye mashine unaanguka kwa mteremko mkali ambao hufuatiwa na mizigo mingine ambayo huangukiwa juu yake na kusababisha usumbufu na uharibifu.
Wako baadhi ya wasafiri kwa mashine hizo wameharibu kompyuta zao ambazo ziliangukiwa na mizigo mingine zikavunjika au vifaa vingine ambavyo lazima uvitoe kwenye pochi au begi na kuweka sehemu husika.
Pia wapo wanaokuwa na ndoo za kitoweo, mabegi makubwa ambao panapokuwa na wasafiri wengi yaani ndege imeshusha abiria wengi kwa wakati mmoja, ni lazima kila mmoja aweke mizigo yake kwenye mashine husika.
Ni muhimu kuhakikisha usalama wa mizigo ya watu kwa kubadilishia vifaa vya kupokea kwa kuweka meza mbele yake kuliko kuacha mizigo kuangukiana na kusababisha uharibifu.
Inaweza isionekane tatizo kubwa sana kwa kuwa huenda watu hawalalamiki au wanapoondoka eneo la uwanja ndipo wanagundua uharibifu huo lakini kimsingi ni tatizo kubwa linalokera wengi katika uwanja huo hasa ‘Terminal II’.
Unapotembea duniani mashine za kuchagua mizigo ni ambazo zinatunza mizigo ya wasafiri, nasi tuige hilo kwa manufaa ya kuzidi kutangaza matumizi ya uwanja wetu zaidi.
Mathalani, wageni wengi wanaotoka mikoa mbalimbali wanarudi Dar es Salaam, ni lazima watumie uwanja huo kama wamebeba vifaa vyao vinavyoweza kuvunjika huenda wamepata hasara na kuona uwanja huo siyo salama kwao.
Nawaza kwa sauti kwamba uwanja huo unaweza kuonekana kikwazo, hivyo jambo linaloweza kuboreshwa ni muhimu likafanyika ili kuhakikisha mizigo ya wasafiri inakuwa salama hadi anapotoka nje ya uwanja.
Mtu anapoharibikiwa na kompyuta, simu au kamera kwa sababu ya utaratibu wa mashine husika inakuwa ni hasara kwake na taifa kwa ujumla.
Lakini wanaosafirisha kitoweo wakati mwingine ndoo zinapoanguka chini kwa mteremko mkali kuna uwezekano wa kupasuka, hali itakayompa shida mmiliki.